Popular Posts

Friday, March 26, 2010

Wafanyabiashara wa madini watapeliwa

*Wauziwa dhahabu, Almas feki
*Waliotapeliwa watinga wizarani
Na Deogratius Temba

Wafanyabiashara matapeli wanaouza madini feki kwa wafanyabiashara halali limeibuka nchini na kugushi nyaraka za serikali zikiwemo mihuri.
Waliokumbwa na utapeli huo nchini ni wafanyabiashara wa kigeni kutoka nchi za nje wanaonunua madini na wametoa taarifa Wizara ya Nishati na Madini na jeshi la Polisi.
Akizungumza na Tafakari, Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Aloyce Tesha, alisema Wizara imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara waliotapeliwa na tayari imechukua hatua za haraka ikiwemo kulikabidhi suala hilo katika vyombo vya dola.
“Tunayo idadi kubwa ya waliohadhirika na tatizo hilo, kesi zote zipo polisi, wanazishughukilia tumechukua hatua za haraka za kutangaza ili kila mtu ajue kuwa kuna tatizo,” alisema Tesha



Kwa mujibu wa Kamishna wa Madini nchini, Dk. Dalaly Kafumu, matapeli hao wamejifanya wafanyabiashara wa madini halali nchini au kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), na kutapeli wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi.
Alieleza kuwa mbinu wanayoitumia matapeli hao ni kupitia barua pepe, ambayo huituma kwa wafanyabiashara hao wakijitambulisha kuwa ni wakala wa kuuza madini au wafanyabishara wa madini, na kuwavutia waje nchini kununua almasi au dhahabu kwa bei ndogo.
“Katika mawasilianmo yao, matapeli hao hutoa majina ya kampuni hewa ambazo hudai zinamiliki kiasi kikubwa cha dhahabu au almasi hapa nchini. Husema kuwa dhahabu yao imehifadhiwa katika maghala hapa nchini tayari kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi,” alisema Dk. Kafumu.
Dk. Kafumu alisema kutokana na kudanganywa wafanyabiashara wa kigeni huvutiwa na uongo huo na kutumbukia katika mtego wa matapeli hao kwa kuvutiwa na bei ndogo ya madini wanayoitaja na kuja nchi wakitegemea kupata faida kubwa watakapouza madini hayo.
Akifafanua jinsi utapeli huo unavyofanyika Kamishna alisema matapeli hao, wamekuwa wakiwaonyesha wafanyabiashara masanduku yaliyojaa dhahabu na alimas bandia na taarifa za kimaabara bandia kuwa dhahabu hiyo imechunguzwa na kugundulika kuwa na ubora wa hali ya juu.

Aidha, huonyeshwa nyaraka bandia zilizogongwa mihuri ya serikali na idara ya forodha zikionyesha kiasi cha dhahabu na dhamani yake.
“Tena hawa watu wakigundua kuwa mfanyabiashara ameonyesha wasiwasi wa kulipia kabla huambiwa alipie mrahaba(loyalty), ili mzigo ukishafika nchini kwao na kukaguliwa ndio walipie gharama halisi, wakishalipwa mrahaba matapeli hao hutoweka na hawaonekani tena,”alieleza.
Kamishna Dk. Kafumu, alisema Wizara inawataka wafanyabiashara wote wenye nia ya kufanya biashara ya madini kihalali wafike au kutoa taarifa katika ofisi za madini ili kupewa mwongozo kabla ya kuingia mkataba na kampuni yoyote.
Alisema ofisi zinazohusika na suala hilo, ni Makao makuu ya wizara na ofisi za Maafisa madini wa kanda kila mkoa.
Ofisi za madini kanda ziko katika miji ya Dar e ssalaam, Arusha, Mbeya, Mpanda, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, na Singida. Pia ofisi za ofisa madini mkazi ziko Bukoba, Chunya, Dodoma, Geita, Handeni, Kahama, Kigoma, Mererani, Musoma, Morogoro, Songea, Tabora ,Tanga na Tunduru.
Mbali na hilo, Kamishna alisema Wizara pamoja na ofisi zake zitawasaidia wafanyabiashara wote kudhibitisha iwapo kampuni wanazokusudia kufanya nazo biashara zina leseni halali za uchimbaji
mwisho

No comments:

Post a Comment