Popular Posts

Friday, March 5, 2010

Serikali yatamani kununua hisa za BP

Na Deogratius Temba

SIKU mbili baada ya kampuni ya kusambaza mafuta ya Uingereza (BP), kutangaza kutaka kuuza hisa zake zilizopo Tanzania, serikali imesema itakuwa tayari kuzinunua mara kampuni hiyo itakapoamua kufanya hivyo.

Serikali inamiliki asilimia 50 ya hisa za kampuni ya BP Tanzania Limited, na kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Uingereza ina asilimia 50, ambazo kwa sasa imatangaza kuziuza.

Akijibu swali la waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, Waziri wa Nishati na Madini Wiliam Ngeleja, alisema serikali inasubiri wakati utakapofika BP wakitaka kuuza hisa zake inazomiliki itazinunua na kama kutakuwa na ulazima jina la BP litabadilika baada ya kuachia hiza zake.

“Serikali imepokea taarifa kutoka BP, kuwa wanania ya kuuza hiza zao, lakini hawajesema kama ni lini. Wameona soko lao hapa labda siyo nzuri na wameamua kujizatiti katika nchi nyingine, hasa katika kipindi hiki cha ushindani ya kibiashara,” alisema na kuongeza:

“Hakuna mwekezaji kutoka nje atakaye kuja kuichukua kampuni hiyo bila kupitishwa na serikali, na baada ya hisa kuuzwa kuna uwezekano wa jina kubadilika,’alisema Ngeleja.



Waziri Ngeleja alisema mara BP itakapofika nchini kwaajili ya kufanya mashauriano na serikali ofisi yake itaishirikisha wizara za fedha, na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ili mkataba wao uweze kuvunjwa vizuri

Alisema BP haitaweza kuuza hiza hizo bila kuipa serikali taarifa kwani ndiye mbia mwenza, na serikali inapaswa kupewa kipaumbele katika ununuzi wa hiza.

Kampuni hiyo kubwa ya mafuta imekuwa ikifanya biashara hiyo kwa zaidi ya karne moja nchini imetangaza kuondoa hiza zake katika nchi kadhaa za Afrika kwa sababu za kibiashara.

Mtendaji Mkuu wa BP Afrika, Sipho Maseko, alitangaza siku ya Jumanne kuwa uamuzi wa kuondoa hiza zake Tanzania umafikiwa baada ya kufanyika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu wa kibiashara na kuona kuwa nchi hiyo iweke nguvu zaidi katika nchi za Angola, Msumbiji, Afrika ya Kusini, Misri, Algeria, na Libya.

Ukiacha Afrika ya Kusini nchi nyingine ambazo BP ameamua kubaki ni zile zinazozalisha mafuta . Pia mbali na Tanzania BP imejiondoa kuendesha biashara katika nchi za Namibia, Malawi, Zambia na Botswana.

Waziri Ngeleja alisema kununua hiza hizo kutakuwa ni uamuzi wa haraka wa serikali.

Mwisho

No comments:

Post a Comment