Popular Posts

Saturday, May 9, 2009

Serikali itatue migogoro ya wawekezaji na wananchi

KUNA usemi usemao “mgeni njoo wenyeji tupone”, kwa sasa umegeuka kuwa mgeni njoo wenyeji waumie, kwa kipindi kifupi tangu mwaka jana kumetokea matukio ya wananchi kuvamia makazi au maeneo ya mwekezaji kwa hasira na kushambulia au kufanya uharibifu.

Ni aibu kwa taifa , historia haionyeshi Watanzania ni watu wa vurugu, kwani tunasikifika kwa uvumilivu na utulivu lakini nafikiri inawezekana wananchi hao huchukua hatua za kufanya vile baada ya kuchoshwa na vitendo vya wawekezaji na ukatili wao.

Siyo rahisi watu kujitokea tu na kwenda katika shamba au mradi wa mwekezaji na kuanza kushambulia, kuharibu na hata kuumiza baadhi ya wafanyakazi wa mwekezaji kama hakuna sababu, hapa tunahitaji uchunguzi wa kina.

Tumekuwa tukijuliza kwa nini wananchi wanafikia mahali wanachoshwa na wawekezaji? ina maana hawatambui mchango wao katika mazingira wanayoishi?, jibu linaloweza kuniridhisha kidogo, binafsi ni kwamba migogoro kati ya mwekezaji na mwananchi mzawa wa eneo husika huchangiwa na viongozi wetu hasa wa serikali za mitaa.

Kwa mfano, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Dakau, Maembe, Kata ya Okaoni, Wilaya ya Moshi Vijijini, kuwa mwekezaji wa Shamba la VASSO Estate, amekuwa akiwafanyia vitendo vya kinyama ikiwa ni pamoja na kufunga maji ya mabomba na mifereji iliyokuwa ikitiririsha maji maeneo yao tangu za mkoloni.

Siyo siri kwa wenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro wanafahamu utajiri wa maji uliopo katika mkoa huo, hasa katika maeneo ya milimani, lakini wakazi wa kijiji hicho kilichoko mita chache tu kutoka pori la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, sasa anunua maji ya kunywa, na wanahangaika kutokana na mazao yao kukauka na kukosa maji ya kumwagilia.

Kilio cha wakazi hawa ni kwamba maji yako wapi?, je eneo hilo limegeuzwa kuwa jangwani? Ukiingia katika kijiji hicho, utashuhudia kahawa, migomba, yakiwa yamekauka na kuaacha maelfu ya wakazi hao kukosa tegemeo lingine la chakula.

Kutokana na mgogoro wa kugombania maji ya mfereji wa Mure, yanayoanzia katika katika mto Umbwe, baada ya mwekezaji huyo, kuweka mabomba kwaajili ya kuchukulia maji ya kunyeshea Maua katika shamba lake, wananchi waligundua kuwa hawawezi kuyapata tena kwani hayakuwa yakitiririka katika mifereji kama ilivyokuwa awali, na walivyozeoa.

Kwa mujibu wa wakazi hao, watu wasiojulimana , waliamua kubomoa na kuharibu mambomba yote kwa kiasi kikubwa, hali iliyopandisha hasira zaidi kwa mwekezaji na kuamua kuyafunga kabisa.

Ni hasara lakini tumbuke hali kama hii ilitokea pia huko Tarime, kijiji cha Nyamongo, wakati wakazi wa eneo hilo walipovamia eneo mgodi wa North Mara na kuharibu mali ya zaidi ya Sh. bilioni 6.

Leo hii kwa mujibu wa mwekezaji huyo, Fons Nijenihuis, anasema anawadai wananchi hao zaidi ya Sh. milioni 8, kama gharama za uharibifu zilizotokea baada ya kuharibiwa kwa mabomba hayo.

Tayari kuna wananchi wanashilikiliwa na kutokana na kuhusishwa na uharibifu huo, ni hiyo pia inaweza kuongeza chuki kati ya wananchi na mwekezaji, na kupelekea maafa zaidi.

Nilibahatika kuzungumza na mwekazaji, huyo, Fons, ambaye alieleza kuwa hana huruma tena kwa wakazi hao, atapambana nao ili mradi aokoe gharama anazozitumia katika shamba hilo, huku wananchi nao wakieleza kupambana na mwekwezaji na kumwandikia vikatarasi vya kumtisha kuwa wataondoka na kichwa .

Serikali isinyamzie hili, taadhari ni bora kuliko hasara, tusisubiri mpaka wananchi waanze kuuana na wawekezaji kwa kufyatuliwa risasi, au wananchi kufa kwa njaa au mateso.

Kwa Dakau, kitendo kama hicho kinasikitisha, nilizungumza na Diwani wa Okaoni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika kilichokodisha shamba hilo, Martini Mallya hakuweza kueleza kwa kina chanzo cha mgogoro licha ya kuwalaumu wananchi wake kwa kutokuwa na uelewa juu ya masuala hayo.

Diwani huyo, mbaye ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Cyril Chami, anasema wananchi ndiyo wenye makosa, na kumtetea vikali mwekezaji huyo.

Kuna haja ya serikali kuu, kuingilia kati migogoro huu, namingine, kwani sera za nchi hii zinahimiza kukaribisha wawekezaji zaidi ili kuimarisha na kufufua sekta ya uzalishaji iliyolala.

Lakini serikali imekuwa ikisisistiza kuwa mwekezaji alete neema kwa wakazi wa eneo husika, baraka, amani, na furaha, na siyo kilio, mateso na vifo, kama tunaelekea huko ni mbaya, matusi kati ya wawekezaji na wakazi siyo tija ya kumaliza umasikini wetu.

Aidha, umakini wa viongozi wetu kama madiwani, watendaji wa mitaa, utalijenga taifa hili, kujali zaidi maslahi ya taifa na wananchi wake, na kuacha rushwa na maslahi binafsi pembeni, huko Dakau, imani ya wannchi kwa viongozi kama diwani, uongozi wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Kibosho Kati, kijiji, kata, na hata wa kitongoji.

Hii inaonyeha picha gani kwa viongozi wetu? Ina maana ni viongozi wageni na siyo wazawa wanaowapa madaraka au kuwaweka katika nafasi hizo, serikali kuu ifanye hima kuokoa maisha ya wakazi hawa kabla ya matatizo zaidi kujitokeza.


.

No comments:

Post a Comment