Popular Posts

Tuesday, April 28, 2009

Muungano unaumwa, rais Kikwete utafutie dawa


“MUUNGANO una kasoro zake, nilisema tutazimaliza, katika kasoro za muungano sikusudii kuunda tume ya kushughulikia kwasababu kamati zilizowahi kuundwa zimebainisha kasoro za Muungano na namna ya kuzitatua,”hii ni kauli ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete,ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kila mmoja anayefuatilia kwa makini suala la Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa April 26, 1964, ataungana na rais Kikwete kuwa Muungano unakasoro na unaumwa tena upo mahutihuti, na kupingana na wasaidizi wa rais ambao kwa sababu zao wamekuwa wakitamka bayana kuwa Muungano ni safi, hauna shida.

Tukiwa tumesheherekea siku ya Muungno, juzi, tuna kila sababu ya kujiuliza ni kwanini kero za Muungno zinaongezeka?, kwanini rais anakiri, lakini wasaidizi wake wanakataa? Na kulazimisha kuwa hakuna mgogoro, badala ya kumsaidia rais na kutafuta dawa ya matatizo hayo?

Hayati Baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere, aliwahi, kutamka kuwa “afichae maradhi yatamuumbua”, hatuna haja ya kukanusha ukweli, kama mtu anaumwa tuseme ukweli ili apatiwe tiba.

Kwa muda wote huo na kwasababu ya tabia yetu ya kiuficha maradhi kwa kigezo kuw ani dhambi kuulizia masuala ya Muungano, tumkuwa tukijaribu kuitibu tu dalili za maradhi ya Muungano badala ya kutafuta chanzo cha kero za Muungano na hii imesababisha Muungano kuingia ICU.

Zaidi ya mara moja mitafaruku kati ya sehemu hizi mbili za Muungano, yaani bara na Zanzibar, imeutikiza nusra ya kuuvunja lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu umekuwa ukichechemea.
Waasisi wa Muungano huo, Hayati Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume walisimamia Muungano na wakati mwingine ulianza kutetereka na kufikia mahali kutaka kuomba nguvu kutoka nje ya kuulinda Muungano huo,
Changamoto nyingi zimewakumba, malalamiko kuhusu kuwepo kwa Muungano huu yanazidi kukua kila siku, inawezekana ilikuwa kosa kuanzisha Muungano,huo ila kuuvunja ni kosa kubwa zaidi.

Kuna swali ambalo limejaa vichwani mwa wasomi na wanazuyoni leo, wanajiuliza, hivi mawazo ya kuungana yalikuwa ya Hayati Mwalimu Nyerere na Karume?, na kama yalikuwa ya kwao wenyewe kwanini walishindwa kuweka misingi imara ya kuulinda na kuwaweka baadhi ya nyaraka za msingi hadharani ambazo zingeweza kudhibiti mawazo ya baadhi ya watu wanaoupinga Muungano?.

Mwaka huu Sherehe za Muungono zimeangukia siku ya Jumapili, na Muungano huu, wakati Muungano uliasisiwa siku ya Jumapili 26, Aprili, 1964, na hicho kilikuwa kipindi cha siku 104, tangu Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Siku chache baada ya Muungano, rais Karume, alikaririwa na gazeti la Nationalist Freedom, la Tanganyika, akisema ; “Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utatufaidisha sote hautakuwa kikwazo kwa watu wa Zanzibar,”

Binafsi nimekuwa nikijiuliza, ni kitu gani kilimsukuma Karume kutamka maneno hayo? neno “hautakuwa kikwazo kwa watu wa Zanzibar”, ina maana alianza kuhisi kuwa Muungano kamwe hauwezi kuwafurahisha watu wa Zanzibar, licha ya kwamba watanganyika hawaja haja nao.

“neno hautakuwa na kikwazo kwa watu wa Zanzibar” lina maana kubwa linapokuja suala la Uzanzibar na Utanganyika ambao Mwalimu aliukataa lakini mzimu wake ndio unao utafuna Muungano huu hadi leo.

Tumeona tayari dalili zinaonyesha kuwa kero za Muungano, na kasoro zipo Zanzibar tu watanganyika wamelala fofo, wanasema Muungano uwepo usiwepo wao wanasonga mbele.

Kero ya kwanza ilitokea siku chache tu baada ya kuundwa kwake, Jamatatu, April 27, 1964, Nyerere alitangaza baraza la Mawaziri alitoa viti vitano kwenda Zanzibar kutoka kwenye baraza hilo.

Hali ilianza kuonekana siku chache baada ya kukatokea mgogoro wa Zanzibar na Tanganyika kuhusiana na suala la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani(GDR), ambapo Zanzibar ilitangaza kuitambua na kutoa utambulisho wake wa kibalozi, wakati Tangayika ilikataa kuitambua, ikawa inaitambua Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mashariki.

Jumanne, Mei 4, 1964, ikiwa ni siku nane tu baada ya Muungano na baada ya kuundwa kwa baraza la Mawaziri, walikaa na kujadili juu ya suala la kuitambua Ujerumani, hawakuelewana, ipasavyo, Muungano ukaendelea kutingisika, waasisi wakazidi kutafuta msaada wa nje kuumaliza, hasa mataifa ya Marekani na Uingereza ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliochochea nchi hizi kuungana waliingilia kati.

Juni 12, 1964, balozi wa Uingereza mjini Dare es salaam, wakati huo, Wiliam Leonhart, alituma ujumbe kwenda Marekani, ukisema anaomba Serikali ya huko imwombe aliyekuwa rais wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, atumike katika kuimarisha Muungano.

Mdahalo wa kwanza juu mfumo na mmundo wa Muungano, ulianza kwa njia ya maoni juu ya katiba, ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1983/84 hapo ilibainika kuwa kwa mara ya kwanza viongozi wa juu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na rais Aboud Jumbe, na wale wa serikali ya Muungano wakiongozwa na Rais wa jamhuri ya Muungano Mwalimu Nyerere, walikuwa na miotazamo tofauti juu ya Muungano.

Jumbe na timu yake walitaka Muungano uwe na serikali tatu kwa maana ya serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar iliyopo sasa, na serikali ya Muungano itakayokuwa ikishughulikia mambo ya Muungano tu.

Kutokana na ukorofi na ujanja wa akina Jumbe, Jumbe alilazimishwa kujiuzulu nafasi zote za uongozi wa nchi kuanzia urais, umakamu wa rais wa Muungano, na nafasi zote za kichama januari 1984.

Baada ya Jumbe kuondoka, hali haikutulia, kuliibuka tena kundi la wabunge 55, maarufu kama G55,walipojitokeza na kwasilisha Bungeni waraka wa kutaka kurejeshwa kwa serikali ya Muungano, mwaka 1993.

Ni kweli kuwa Bunge lilikuwa limeshapitisha azimio la pamoja la kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika, Augosti 24,1993, kwa maana kuwa kuwepo na serikali tatu, kama alivyotaka Jumbe mwaka 1983.

Lakini mwalimu Nyerere, akaona kuna hatari ya Muungano kuishilia mbali kama atanyamaza, ikapelekea aliyekuwa waziri Mkuu wakati huo, John Malecela, na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba, wakapoteza nyadhifa zao kwa kunyamazia makundi hayo na hoja hizo kuingia Bungeni.

Kama anavyosema rais Kikwete, ambaye anamalizia miaka mitano ya utawala wake, akiwa bado hajaweza kutafauta dawa ya kuutibu Muungano huo uliolazwa ICU, tunaingia kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, tukiwa na majeraha ya Muungano,hakuna suluhisho la matatizo.

Migogoro ya kupinga matokeo ya uchaguzi ni matokeo ya kutokutaka kutibu magonjwa ya Muungano, hayo ni moja ya magonjwa ambayo yanauandama Muungano, tyunael;eka kutibu dalili na kuacha kuangalia chanzo cha ugonjwa.


Matumizi mabaya ya jeshi, au dola visiwani humo, ni tatizo na ni kero mojawapo ya Muungano, huwezi kuongoza watu kwa kuwashambulia kila wanapopiga kura, wakimaliza unawaacha, haya ndiyo yanayowaumiza wapemba na kuuona Muungano kama audi wao, na kuuchukia kabisa.

Ni dhahiri kuwa Muungano hauna shida kwa wapemba kama wakipewa haki ya kufanya uchaguzi na kuchagua viongozi wao kwa uangalifu na umakini na wakamweka mtu wanayempenda madarakani, bila serikali ya Muungano kuingilia kati, au kupeleka jeshi la kupambana na raia, kero zitapungua.

Kero ya kudai kuwa mambo 11 ya Muungano hayako wazi, suala la mafuta, suala la Muhamed Seif Khatib kutaka kuwa rais, siyo la kusababisha Muungano kuvunjika kama viongozi wetu watakaa pamoja na kuangalia masuala ya msingi hasa ya wapemba, na kuwajali, kama watu wasio waasi.

Muungano umejaa magonjwa zaidi ya 22, umefungwa plasta kila mahali, katiba yake yenyewe ina viraka.

Ukiangalia matendo ya watendaji wa serikali hiyo ya Muungano unaweza kulia machozi kwasababu hakuna aliye na usafi wa kuweza kuwasafisha wenzake.

Mgonjwa wetu ni Muungano ana matatizo mengi serikali inapaswa kuangalia vyanzo vya magonjwa ya Muungano na siyo kutibu majeraha pekee, na kuuacha ukiangamia.
0784/ 715/ 686575
deojkt@yahoo.com
Mwisho.

1 comment:

  1. ninashukuru, kwa makala hii ambayo inatufungua macho, kumbe watawala wetu wanajua kuwa muungano uana matatizo lakin wanafunga macho, rais kikwete uoka muunmgano au umalizie mablia
    John bagamoyo

    ReplyDelete