Popular Posts

Saturday, February 27, 2010

Kundi safisha JK laanza kazi rasmi
*Wamo Mrema, Mama yake Zitto Kabwe, Aman Kaborou
*Mrema: Siachi kazi ya usalama wa taifam, nitamtetea JK
*Mama Zitto: Kura za urais JK,upinzani ubunge
Na Deogratius Temba

KATIKA kile kinacho onekana kuanza kwa kampeni kali za kumsafisha rais Jakaya Kikwete, kutokana na shutuma alizotupiwa na baaadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi(CCM), na viongozi wastaafu ndani ya serikali ya awamu ya kwanza, kundi la kumsafisha limeanza kazi rasmi.

Kundi hilo ambalo linaongozwa na Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Wald Amani Kaborou, na na wajumbe kutoka Vyama vya Tanzania Labour (TLP) na NCCR- Mageuzi, limeanza kwa kuwashutumu wanaotaka rais Kikwete atoswe na kuushambulia uongozi wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF) kuwa ni wachochezi.

Wakizungumza katika mkutano wa kwanza uliofanyika katika viwanja vya Temeke Mwisho, jijini Dar es salaam, juzi jioni na kuhudhuriwa na wananchi wachache wasiofikia 100, kundi la wajumbe wa taasisi hiyo ya Aman Forum, walisema ili kuleta amani nchini ni lazima kumchagua tena rais Kikwete kwani amejitahidi kulinda amani ya nchi na kuonyesha mfano mzuri katika nyanja za kimataifa.

Akizungumza na umati huo mdogo Mwenyekiti wa TLP Augustine Mrema, alisema watanzania wanatakiwa wamwelewe vizuri sababu za yeye kuamua kujiunga na taasisi ya Aman Forum, kwani amegundua kuwa nchi ina tatizo hasa inapokuwa kwenye uchaguzi wa urais.

“Kuna kundi la watu lina njama za kumdhuru au kumsambaratisha rais Kikwete, na serikali yake, wajue kuwa wakifanya hivyo hawatakuwa wamevidhuru vyama vya upinzani pekee ni watanzania wote, mimi nimeamua kujiunga na Amani Forum, ili sasa nitangaze vita na kundi hilo,” alisema Mrema na kuongeza:

“ Naomba minielewe, mimi Augustine Mrema nimefundishwa usalama wa Taifa ndiyo ninao utetea ninaitetea dola mimi, siyo Rais Kikwete. Nimeongoza usalama wa taifa katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa, pia nimekuwa mwalimu wa usalama wa taifa, na kazi hii siwezi kuiacha mara moja msinishangae nimefundishwa kufanya kazi hii,” alisema

Mrema, aliyekuwa akizungumza huku idadi ya watu ikiwa ndogo, aliendelea kusema kuwa alisema ameamua kutetea nchi na hajahongwa wala kununuliwa na mtu yoyote.

Mwenyekiti huyo aliwashambulia makada wa CCM na viongozi wastaafu walioshiriki kuchangia hoja katika tamasha la kumuenzi hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, lilinyika katika ukumbi wa Karimejee mwishoni mwa mwaka jana kuwa ni wachochezi na wanatakiwa kukamatwa kwasababu hawana heshima kwa rais wa nchi.

“ Kuna tamasha la Mwalimu Nyerere, makada wa CCM wamelitumia kama kichaka cha kuendesha uhaini hawa walinunuliwa wamesema Kikwete kuwa amezungukwa na wezi, wanamtukana rais? Nyie CCM mnamtusi kiongozi wenu anayewapeperushia bendera?”

Mrema ambaye aliwahi kuibua kashfa ya ufisadi wa kuibiwa kwa sh. Bilioni 900, ambayo ilimuhusisha pia rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alisema miaka minne ya rais Kikwete, amefanya mambo makubwa ikiwepo kuruhusu wasaidizi wake wajiuzulu, kwa kuhusishwa.

“Hivi mnamtaka afanye maamuzi gani mazito, wakati amekubali rafiki yake aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa ajiuzulu? Serikali sii imewajibika? Mnasema mtamtosa kwa kosa gani alilofanya rais Kikwete?

Mrema aliendelea kusema kuwa suala la ufisadi hata Baba wa Taifa alilishindwa kwasababu baadhi ya viongozi waliokuwa wakifanya naye kazi walipohusihwa na ufisadi aliwahamisha au kuwaongezea majukumu badala ya kuwawajibisha.

“Mwingira aliuza ndege ya serikali, mbona Nyerere alimwamisha na kumpa ukuu wa mkoa wa Arusha , Balozi Mustafa Nyang’anyi alinunua Kivuko kibovu mwalimu akampa ubalozi wa Marekani, rais Kikwete amewapeleka watu mahakamani ninyi mnasema mtamtosa,” alisema

Mrema aliyekuwa amefuatana na baadhi ya viongozi wa Chama chake makao makuu akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Hamad Tao, aliendelea kusema kuwa hajanunuliwa, na raia Kikwete, lakini atahakikisha anampigia debe ili ashinde urais Oktoba mwaka huu.

“Watanzania tuache uongo, unafiki na uzandiki, sijanunuliwa na rais Kikwete, mbona Seif anayempigia Rais Karume, debe kuwa aongezewe muda hamsemi amenunuliwa? Ninasema kura zote za urais ziende kwa Rais Kikwete,” aliongeza


Naye Walid Kaborou, ambaye ni mwenyekiti wa Taasisi hiyo, alisema, wanaosimama na kusema kuwa rais Kikwete atoswe wanazungumzia kazi ambayo hawajawahi kuifanya.

“ Hawa hawajawahi kuwa marais leo wanasema rais atoswe, hao Mwalimu Nyerere Foundation kati yao nani aliyewahi kuwa rais? Hao ni wachochezi na kwa uchochezi kama huo hatuwezi kufika,” alisemea Kaborou

Alisema anashangaa kuona watu wanaomwona rais Kikwete akichweka wanasema kuwa anacheza wakati katika utafiti wa taasisi ya Synovate uliofanyika hivi karibuni watanzania zaidi ya asilimia 75 wameonyesha kumkubali rais Kikwete na kuomba aendelee.

“Wewe unayesema aondoke unataka nani awe rais? Akicheka unasema kuwa rais anacheza unataka alie? Wewe ni nani unasema humtaki rais aliye na marafiki ndani ya serikali mimi ninasema kwa nguvu zote kuwa kura zote kwa rais Kikwete na atashinda kwa kishindo,” alimalizia Mbunge huyo ambaye alihamia CCM akitokea upinzani

Akizungumza Mwenyekiti wa walemavu, Shida, Salumu, ambaye ni mama wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema rais Kikwete amefanya kazi nzuri ya kuimarisha amani na kuwatetea walemavu kwahiyo anatakiwa kupigiwa kura zote za urais ili aendelee.

“Ninasema hivi hakuna mtu anayeweza kuwatetea walemavu kama rais Kikwete, amewakamata wauaji wa maalbino, na sasa anatutetea zaidi, kura zote za urais ni kwa rais Kikwete, wapinzani watapata za ubunge tu,” alisema

Awali awakiwakaribisha wajumbe wa Aman Forum, Katibu Mkuu Taasisi hiyo, Risasi Mwaulanga, alisema yeye binafsi anawataka watanzania kuhakikisha wanamchangua tena rais Kikwete ili aweze kuendelea kuimarisha amani iliyopo nchini.

Mwaulanga alisema taasisi hiyo itazunguka ikifanya mikutano nchi nzima na hivi karibuni itafanya mkutano katika viwanja vya Mzense Darajani na baadaye Buguruni mwisho jijini Dar es salaam
Mwisho

No comments:

Post a Comment