Popular Posts

Friday, January 14, 2011

Wanafunzi UDOM, mabomu na virungu vya FFU ni fadhila

Ninasikitika ninapoona wadogo zangu, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), wakilalamikia mateso wanayoyapata kutokana na kukosa mikopo ya elimu ya juu. Moja ya kilio chao ni kutokupewa fedha za kufanya mazoezi ya vitendo na kukosekana kwa maji safi ya kunywa chuoni hapo.
Hii ni dhuluma na aibu kwa Taifa ambalo limeshindwa kuwajali wasomi wake linaowaandaa na watakaotegemewa kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika nchi yao.
Vijana hawa wa vyuo vikuu wamekuwa wakiandamana kila mara wakidai kulipwa stahiki zao kama sheria na taratibu za bodi ya mikopo zinavyoelekeza, fomu za kuomba mikopo zimeeleza waziwazi taratibu zote na masharti ya kupata mikopo lakini serikali ambayo imetengeneza sheria na sera ya mikopo inashindwa kutekeleza mkataba huo ambao inauingia na mkopaji(mwanafunzi).
Katika safu hii leo, nitaeleza kinachowapata wanafunzi wa UDOM na matokeo yake, kwanza tukumbuke kuwa mnamo Juni 13,2010, wanafunzi wa UDOM waliandamana na mabango mengi wakiwa na fedha sh. 1.5 za kumkabidhi aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM Rais Jakaya Kikwete, achukulie fomu na wakitaka awe mgombea pekee katika kinyang’anyiro hicho.
Kwa tabia hiyo waliwachefua sana wananchi na wapenda demokrasia nchini. Watu walijiuliza ni kwanini vijana hawa wasomi wanaamua kuua demokrasaia nchini tena kwa kulazimisha?, je walikuwa wametumwa na mtu yoyote kumpigia debe mgombea mmoja ndani ya chama hili hali wakijua kuwa kuna wanachama wa CCM lukuki walitaka kugombea urais?
Tunajuliza, je wanafunzi hawa hawaelewi kuwa walikuwa wakiibomoa demokrasaia na kuikaba koo? Nimekuwa nikijiuliza wanafunzi hawa hawakuwa na uelewa wa jambo walilokuwa wakilifanya kuwa walikuwa wakiwakosea haki watanzania wenzao?
Bila shaka wanayo majibu wenyewe. Wametangaza kuwa mgombea huyo apite bila kupingwa, wamepiga kelele, uchaguzi umemelizika watawala wameingia madarakani, mwezi mmoja baada ya Serikali kuundwa, Desemba 20,2010 wanafunzi hao hao ambao walisema kuwa watapigana kufa kuhakikisha CCM inashinda walioandamana wakiwa na mabago ya kuwatukana viongozi wandamizi wa CCM na kudai kuwa wanaelekea ofisi ya Waziri Mkuu, hata hivyo kwasababu waliuingiza utawala usio na mapenzi kwao madarakani, walipigwa mabomu na virungu na jeshi la polisi na maandamano yakavunjika.
Huo ndio utawala walioupigania kuhakikisha unaingia madarakani. Huo ndio utawala ambao waliuchangia fedha sh. 1.5, wakati wazazi wao waliowaacha vijijini wanakufa kwa kukosa Aspirini au Panadol. Wadogo zao vijijini wameshindwa kulipa ada ya sh. 20,000/= kwenye shule ya kata na wanarudishwa nyumbani lakini wao wanazipeleka CCM kuchangia fomu.
Leo hii wanaandamana kudai haki zao, yote hayo ni matunda ya kile walichokipanda, hawapaswi kulalamika wala kulia, watapaswa kujua kuwa ‘unachokipanda ndicho unachovuna’.
Wala hatushangia kuwa madai ya UDOM yataendelea kuwa kama madai ya wanafunzi wa vyuo vikuu vingine, watalia na kupigwa mabomu kila mara kwani huu ndiyo utaratibu wa watawala wetu walioshindwa kazi. Kutumia nguvu ya dola kunyamazisha kelele za madai ya haki.
Mwezi mmoja baadaye Januari 10, 2011 wanafunzi hao hao wameandamana tena wakidai fedha za mafunzo na kukosekana kwa maji chuoni kwao. Mara hii wamendamana wakapigwa tena mabomu ya machozi na virungu. Maandamano yakavunjika, wamedai kutaka kumwona rais lakini wameambiwa madai yao hayana sababu ya kmuita rais kwenda Dodoma, fedha zenu za kulipia fomu mngeweza kuzitumia leo kama nauli ya kwenda Dar es salaam kudai fedha Bodi ya Mikopo.
Wanafunzi wa Dodoma huu ndiyo utawala mliouingiza madarakani wenyewe, mlipiga kampeni sasa wamewatosa, hawawezi kuwalipa fadhila kwa mlichokifanya, shukrani yao kwenu ni ngumi na mateke na mabomu ya FFU, hayo ndiyo mavuno yenu.
Wasomi wa vyuo vikuu sasa badilikeni, tizameni wajibu wenu mlio nao kwa jamii inayowazunguka, tazameni wazazi, wenu na majirani zenu miliowaacha vijijini hali walionayo, wanahitaji wewe uliyefika chuko kikuu umpiganie, kama unageuka kuwa mndulakuwili kuwatetea watawala utahukumiwa kwa dhambi hiyo.
Kwahiyo basi, mnachokifanya leo mnapokuwa Chuo Kikuu kinapaswa kuwa msaada kwa wanakijiji wenzenu, muwe na uchungu wa kuajali maisaha ya watu wengine mliowaacha huko, mjue kuwa mnategemewa katika kubadilisha hali zao za maisha.
Mkumbuke kuwa wnaanchi hawakufurahishwa na kitendo cha kuchangisha fedha kwaajili ya uchaguzi Mkuu, huko ni kukosa kujitambua, inawezekanaje kwa msomi wa Chuo kikuu tena anayetegemewa kuleta mapinduzi ya kidemokrasia katika nchi iliyosinzia kidemokrasia kufanya vile?
Kitendo chenu kilikuwa ni ukandamizaji wa demokrasia unaopaswa kupingwa na wana CCM wenyewe, sio kusubiri Dk. Wilibrod Slaa na Zitto Kabwe kuja kutuhubiria hilo. Ninyi kama wasomi mmeshindwa kulisaidia taifa lenu, na kwa mantiki hiyo, jamii hii itawakataa na itajuta kujinyima ili kuwasomesha, wazazi na walezi wenu wanasikitika na kufedheheshwa kwa kupoteza lengo kwenu. Mbadilike na muachane na faraja za siku mmoja wakati wa uchaguzi.
Pesa, pombe, fulana, kofia, kalamu, ahadi za nafasi nzuri na kusahahu machungu na huzuni nyingi mlizozivumilia katika miaka mitano iliyopita ndizo zinazowatesa leo, mabomu ya machozi ni malipo kwenu. Tutaona nawiki ijayo.

No comments:

Post a Comment