Popular Posts

Saturday, January 16, 2010

Tunaandaa vifisadi vitakavyo ridhi madudu yetu

LEO ni siku ya kwanza kwa safu hii kujitokeza tena kwa mwaka huu wa 2010, sina budi kuwatakia wasomaji wangu Heri ya mwaka mpya na kuwaomba radhi kwa kukosekana kwa kipindi cha zaidi ya wiki tatu. Ninamshukuru mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na nguvu ya kurejea tena baada ya mapumziko ya Mwisho wa mwaka.

Huu ni mwaka muhimu na wa kihistoria kwa Tanzania kwasababu tunaingia katika uchaguzi Mkuu wa kuwachagua rais, wabunge na madiwani, hilo linakuwa jambo la kihistoria kwa sababu tunawaweka watu watakao tuongoza madarakani, ambao wanaweza kuyafanya maisha yetu kuwa magumu au kuwa mazuri. Tunahitaji umakini mkubwa kwa hilo.

Leo tunaweza kuangalia jambo ambalo bado linatakiwa kuwekwa katika akili za watanzania na kulitafakari kwa kina. Tunaingia katika uchaguzi Mkuu na hali gani, je tumebadilika au tunakwenda kama tulivyoingia ule wa mwaka 2000 na 2005?. Je tunataka makosa yale yale yajirudie?

Tunayo haja ya kuangalia mapema na kuchambua kwa makini maswali haya, je tunajiandaaje kuingia katika uchaguzi? je rushwa itajirudia? Je nasi wapiga kura(wewe na mimi) tunajiandaa kuifaidi rushwa? Je vyama vinafanya nini leo? Je CCM ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa inabana demokrasia kwa kutumia rushwa imejirekebisha?

Kwa hali ilivyo katika chaguzi za ndani ya Chama cha Mapinduzi(CCM), ni dhahiri kuwa hatuwezi kukitengenisha chama hicho na rushwa za uchaguzi hasa mwaka huu.

Kwao uchaguzi na rushwa ni pete na kidole kwani ili washinde au kushika madaraka ni lazima watumie nguvu ya fedha, hiyo ndiyo imani yao. Na wanaamini hivyo. Juzi nilikuwa katika ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es salaam, katika kutaniana na Mbunge mmoja wa CCM, alinieleza kuwa huwezi kwenda kwa wapiga kura mikono mitupu na ukatengemea kuchaguliwa. Hiyo ndiyo imani ndani ya CCM, “pesa mbele upate ushindi”

Chama kimejijengea umafia wa ajabu, kila mara fikra za viongozi hata wale walioko mdarakabni wanaota ndoto ya kugawa mipesa hata kama hakuna ushindani mkubwa.

Huko nyuma watu wamekuwa wakishauri kuwa labda inawezekana kuikomesha rushwa iliyoko nchini kwa kuwaondoa wanasiasa wote waliokaa madaranai ambao ndiyo wanadaiwa kuwa chanzo cha rushwa. Watu wameshauri labda kikija kizazi kipya ambacho ni cha vijana wasafi wasio na harufu ya rushwa tunaweza kuwa na taifa safi. Kwa sasa ninaikataa falsafa hiyo, sii kweli.

Ni vigumu kwa sasa kuiondokana na rushwa hasa ndani ya CCM, kama ilivyo vigumu kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano. huwezi kukwepa rushwa wakati unawafundisha watoto au kizazi kipya kuitumia.

Uchaguzi wa Chipukizi ngazi ya matawi hadi taifa uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita ni fundisho kubwa, na ni ushahidi kuwa kumbe rushwa imeoteshwa na imeota mizizi imara ndani ya CCM, kwahiyo kuiacha ni vigumu.

Mkutano wa Chipukizi iliyoko chini ya Jumuiya ya Vijana (UVCCM), ulifanyika mjini Morogoro, Desemba 29 mwaka jana, baadhi ya wapambe wa wagombea(watoto) waligawa pesa hadharani na wengine kukutana nao usiku wa manane.

Utoaji wa rushwa kwa wajumbe ulianza siku moja kabla ya uchaguzi huo ambapo wapambe wa wagombea hao watoto wadogo wa miaka 10, walipita kwa wajumbe wakiomba kura na kutoa takrima mbalimbali zikiwamo pesa.

Katika uchaguzi huo ambao watoto wa vigogo ndani ya chama hicho waliibuka washindi, ni ishara mbaya kwa CCM kwa vile sasa hata watoto wadogo wa miaka 10, wanafundishwa kutoa na kupokea rushwa.

Katika uchaguzi huo, Wajumbe wa mkutano waliohudhuria ni wenyeviti wote wa Chipukizi wilaya ambao ni watoto wa miaka 10 hadi 13, na makatibu wa Chipukizi na uhamasishaji wa wilaya ambao huwa ni vijana wakubwa.

Tena mbaya kabisa na aibu ni pale ambapo makatibu wa mikoa wa UVCCM walikubali kutumika na vigogo ndani ya CCM kupanga mkakati wa kuwawezesha watoto wao, kushinda katika uchaguzi huo.


Mbaya tena ni kwamba uchaguzi huo uligubikwa na rushwa kuchafuana majina miongoni mwa kambi hali iliyosababisha watoto wa vigogo kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo. Vitoto vidogo vimefundishwa kuchafuana na kuambiana kashfa za wazazi wao. je hilo ndilo taifa tunaloliandaa? Hao ndiyo viongozi wetu wa baadaye?

Pamoja na watoto (wajumbe) kuweka msimamo wao mwanzoni wa kuhakikisha hawawachagui watoto wa vigogo, msimamo huo ulishindikana kutokana na shinikizo la viongozi wa juu na kulainishwa kwa rushwa.

Baadhi ya wajumbe hao walidai msimamo huo uliwashtua baadhi ya viongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa waliokuwepo mkoani hapo na kuamua kumshauri mmoja wa wagombea wa uchaguzi huo, Halfan Kikwete asitokee katika uchaguzi huo kwa kukwepa aibu ya kushindwa.

Kwa kukumbushia tu, waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Gabriel Makala ambaye ni mtoto wa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Taifa, Amos Makala kuwa Mwenyekiti mpya wa chipukizi taifa baada ya kupata kura 300 kati ya kura 357 zilizopigwa na hivyo kuwashinda wagombea wenzake saba waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mbali na Makala pia mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Halfan Kikwete alichaguliwa kuwa mjumbe wa baraza kuu kutoka Tanzania bara kwa kura 301 bila kuwako ukumbini hali mbayo inawashangaza wafuatiliaji wengi wa siasa hasa uchaguzi huo.

Lakini kinacholeta maswali mengi, na kujenge taswira ya kuwepo kwa shinikizo la wakubwa na hata watoto kufundishwa kutumia rushwa na wakubwa ni kuwepo kwa viongozi wakubwa wa CCM kitaifa ndani ya mkutano huo. Tena wale ambao watoto wao waligombea.

Baadhi ya viongozi hao ambao uchuguzi unaonyesha walikuwepo ni Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emanuel Nchimbi, mshauri wa rais January Makamba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM taifa, Amos Makala pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya, ambao wangepaswa kudhibiti hali hihyo lakini hawakufanya hivyo.

Tujifunze kigtu kutokana na hali hiyo, huku tukitemea hali ya rushwa kuzidi kuwa mbaya kadri siku zinavyokwenda.

0784 686575
deojkt@yahoo.com
Mwisho.

No comments:

Post a Comment