Popular Posts

Monday, November 16, 2009

SAKATA LA MWEKEZAJI TRL

Wizara yakalia maamuzi ya Baraza la Mawaziri

Na Deogratius Temba

SIKU mbili baada ya Baraza la Mawaziri kukaa na kujadili juu ya notisi ya siku 60 iliyotolewa kwa serikali na Menejimenti ya kampuni ya kuendesha huduma za Reli nchini (TRL), Wizara ya Miundombinu imeendelea kuwa kimya bila kutoa ufafanuzi na maamuzi ya serikali juu ya suala hilo.

Suala la notisi ya TRL liliingizwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika juzi Jumatano jioni na kuongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni rais Jakaya Kikwete, kutokana na ahadi iliyotolewa Bungeni Dodoma na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wiki iliyopita kuwa suala hilo litajadaliwa katika baraza la hilo na serikali kutoa majibu kwa wafanyakazi wa TRL na wananchi.

Jana waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walimiminika katika ofisi za Wizara wakitaka kujua maamuzi ya serikali juu ya suala hilo, ambapo hakuna afisa hata mmoja aliyekuwa tayari kulizungumzia kwa madai kuwa hilo ni suala linalohitaji tamko kutoka ngazi za juu.

Msemaji wa Wizara hiyo Martin Ntemo, alipoulizwa kila mara alikuwa akisema kuwa yeye hana majibu anasubiri kuambiwa na wakubwa wake aseme nini.

“Mimi sina kipya, suala hili lilikuwa katika ngazi za juu na waziri Mkuu alishalizungumzia tusubiri wakishakuwa tayari watatueleza, kuna mazungumzo yaendelea,” alisema Ntemo.

Alipotakiwa kueleza kama serikali iliijibu notisi hiyo ya TRL iliyomalizika Novemba 10, alisema suala hilo linaweza kufafanuliwa vizuri zaidi wakati Waziri atakapokuwa tayari kutoa tamko lake.

Waziri wa Miundombinu Dk. Shukuru Kawambwa, alipotafutwa jana ofisini ,kwake hakupatikana na kila mara wasaidizi wake walikuwa wakidai kuwa yupo nje ya ofisi kikazi.

Akijibu maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni katika mkutano wa 17 uliomalizika wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika swali aliloulizwa na Mbunge wa Tabora mjini, Siraju Kaboyonga, aliyetaka kujua hatma ya mkataba wa TRL, alisema Baraza la Mawaziri litakaa kujadili uwezekano wa kuuvunja mkataba huo.

Pamoja na kukiri kupokea kuwa serikali imepokea notisi ya siku 60 kutoka TRL alisema Baraza la Mawaziri litakaa na kuangalia namna ya kuuvunja mkataba huo kisheria na baadaye itawaeleza wananchi msimamo wake na mstakabali wa shirika hilo.

Rites inataka kuvunjwa kwa mkataba ulionda TRL ambao ulipelekea kuvunjwa kwa shirika la Reli nchini (TRL).

Baada ya notisi hiyo kumalizika bila serikali kutoa tamko Novemba 10, mwaka huu wafanyakazi wa TRL walitangaza kutoitambua menejimenti ya TRL hadi serikali itakapo uvunja mkataba huo rasmi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment