Popular Posts

Tuesday, October 13, 2009

TUTAMKUMBUKA NYERERE WETU

Na Deogratius Temba

HATIMAYE ni miaka 10 imepita tangu tuondokewe na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambaragwe Nyerere, katika kitabu cha maandiko matakatifu Biblia Mhubiri 3:1-2 inaeleza kwamba kila jambo na majira yake na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu.

Wakati wa kuzaliwa na wakufa, kwa maana hiyo kila nafsi itaonja mauti hivi ndivyo ilivyotokea kwa mwalimu, wengi tulimpenda na tulitaka aendelee kuwepo lakini hatukuweza kuzuia nyota yake ilizimika angali watanzania wanamengi ya kupata kutoka kwake.

Busara zake, maadili ya uongozi aliyokuwa akisisitiza na jinsi alivyochukizwa na anguko la Azimio la Arusha sitasahau siasa ya ujamaa na kujitegemea tuliyosoma kipindi hicho tukiwa shuleni lakini sera hii haikuweza kudumu kutokana na awamu ya pili kushindwa kuendelea na utekelezaji.

Labda halikuweza kudumu kutokana na anguko la kisoviet lakini bado tutaendelea kuenzi mawazo yake ambayo hadi leo yanaishi ingawa kimwili hatupo nae, swali la kujiuliza je, viongozi wetu wameweza kweli kuzingatia yale aliyokemea Mwalimu kwa uwezo wake wote?

Kwa kweli hapa niseme kuwa viongozi wameamua kuachana kabisa na busara za Nyerere mambo mangapi sasa yanatokea ambayo yapo kinyume kabisa na maadili ya uongozi.

Katika moja ya hotuba zake anasema kuwa Ikulu si mahali pa kukimbilia na kunatakiwa kuogopwa kama ukoma na ukiona mtu anatumia pesa zake ili aweze kuingia Ikulu ni lazima umhoji anakwenda kufanya biashara gani.

Kati ya tuhuma zinazoitesa serikali ya awamu ya nne ni pamoja na kujihusisha na biashara mfano mmojawapo ni makaa ya mawe Kiwira ambapo serikali ya awamu ya nne imeamua kuirudisha mikononi mwake

Ukiangalia mahotel ya kimataifa kila kukicha yanabadilishwa majina ili kutudanganya kuwa ni mwekezaji mpya wakati wananchi wanaelewa kila linalofanyika yote hiyo ni kukwepa kulipia kodi

Na viongozi wengine wamedaiwa kujenga mahotel hadi nje ya nchi wakati wananchi wanateseka na ukosefu wa ajira

Nadhani si vema tujifariji kuwa tunamuenzi Mwalimu kwa kuandika baadhi ya majengo majina yake tunachopaswa kuzingatia ni maadili ya uongozi aliyokuwa akisisitiza kwenye hotuba zake na hata wale aliokuwa nao karibu kuiga mifano yake.

No comments:

Post a Comment