Popular Posts

Tuesday, October 20, 2009

Richmond yaitesa serikali

Na Deogratius Temba

SUALA la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya hatma ya waliohusika na uingiaji wa zabuni wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development (LLC) limezidi kuichanganya serikali na kugubikwa na utata.

Hayo yametokana na na serikali kushindwa kujitokeza jana mbele ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kama ilivyokuwa imepangwa ili kutoa taarifa ambayo ingewasilishwa na Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya kamati hiyo vinavyoendelelea katika ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es salaam, jana kamati ilipanga kupokea taarifa hiyo na kuanza kuijadili kwa muda wa siku mbili.

Badala ya kupokea taarifa hiyo, kamati iliwaita watendaji wa kampuni ya kutafuta gesi na kufufua umeme ya Songas, ili kupata taarifa ya maendeleo ya uzalishaji wa umeme, matengenezo ya mashine ya kuzalisha umeme wa Megawat 20, iliyoharibika katika kituo cha Ubungo pamoja na mipango mingine.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa serikali iliiagiza kamati hiyo kuendelea na shughuli nyingine hadi itakapokuwa tayari kupeleka taarifa ya Richmond.

Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya Bunge kililiambia Tanzania Daima Jumatano kuwa suala hilo limeahirishwa kutokana na ombi kutoka serikalini kuwa Waziri ataiwasilisha taarifa hiyo muda wowote mara itakapokuwa tayari.

“Ni kweli leo (jana) tulikuwa tuipokee taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge lakini haya ni masuala yanayoihusu serikali zaidi, wameomba tuendelee na kazi nyingine wanaweza kuiwasilisha kesho (leo) au kesho Kutwa (Kesho),” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza kuwa kamati na wabunge wengine wameamua kuisubiria serikali, lakini wameitaka iwasilishe taarifa hiyo kabla ya kumalizika kwa vikao vya kamati ambavyo vinatajiwa kumalizika Oktoba 23, mwaka huu.

“Bado kuna muda hizi siku tatu zilizobaki inaweza kuletwa, tuwe na subra usiwe na haraka,”
kilisema Chanzo hicho.

Jana Mwenyekiti wa kamati hiyo Wiliam Shellukindo, aligeuka mbogo kwa waandishi wa habari kwa kuwataka kutouliza maswali nje ya suala la Songas, ambalo walilijadili.

“Nataka kuwaeleza tulichozungumza na watu wa Songasi, lakini nikimaliza nitakaribisha maswali ambayo yatahusiana tu na suala hili la Songas, nje ya hapo sintajibu,” alisema Shelukindo.

Kutokana na msimamo huo wa Shellukindo waandishi wa habari walishindwa kuuliza sababu za Taarifa ya Richmond kutokuwasilishwa mbele ya kamati hiyo na ni lini itawasilishwa.

Alipoanza kujibu maswali alionekana kutokuwa na furaha na ghafla wabunge wa kamati hiyo walianza kunyanyuka na kuwaambia wanahabari kuwa wanashughuli nyingi za kufanya kwa hiyo wanaondoka hawatakuwa na muda wa kujibu maswali mengine zaidi.

Awali Tanzania daima lilielezwa kuwa taarifa hiyo haitawasilishwa kwa kamati hiyo ikiwa jijini Dar es salaama kwa sababu za kiusalama, badala yake wataipokea wakiwa mjini Dodoma na kuijadili endapo watairidhia wataruhusu serikali iiwasilishe Bungeni katika mkutano wa 17, unaotarajiwa kuanza Oktoba 27, mwaka huu.

Taarifa za ndani ambazo Tanzania daima limezipata zimezidi kueleza kuwa serikali imeanza kuhofia kuitoa taarifa hiyo mapema kwani inaweza kuvuja na kutoa mwanya kwa baadhi ya watuhumiwa wa Richmond kujipanga namna ya kujisafisha au kupoteza baadhi ya vilelezo.

“Hofu yetu ni kwamba serikali ikiwasilisha taarifa hii mapema hadi kufikia siku ya kuijadili Bungeni itakuwa imezagaa mno, taarifa kuenea watuhumiwa kujipanga, inatakiwa iwe ya kushtukizia,” alisema Mmoja wa Maafisa wa serikali anayehusika katika ufuatiliaji wa jambo hilo.

Katika mjadala huo uliokamiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, wajumbe pamoja na mambo mengine wataangalia kama Serikali imejibu maswali na maagizo ambayo Bunge liliipa serikali wakati wa mkutano wa 16, mjini Dodoma.

Wakati Bunge likitaka watu zaidi waliohusika wawajibishwe tayari mmoja wa wawakilishi wa kampuni ya Richmond, Naeem Adam Gire, ameshafikishwa katika mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam Januari 13 mwaka huu na kusomewa mashtaka matano ya makosa ya jinai.
Mwisho

No comments:

Post a Comment