Popular Posts

Monday, October 26, 2009

Mtaa wa Mwenyekiti wa CCM mkoa waenda Chadema

Na Deogratius Temba
MTAA wa Korogwe,Kata ya Kahama anapoishi Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja, umechukuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Habari za uhakika toka Kahama zinasema kwamba mjini licha ya kampeni kubwa iliyoambatana na zilizofanywa na Mwenyekiti huyo akiambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zainabu Kawawa mgombea ziligonga mwamba na Leonard Mayala wa Chadema aliibuka kidedea kwa kupata kura 214 dhidi ya Amos Maganga wa CCM aliyeambulia kura 156.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kwamba, kushindwa kwa CCM katika mtaa huo kumetokana na mizengwe iliyofanywa na chama hicho katika zoezi la kura za maoni jambo ambalo liliwakasirisha wananchi hivyo kuamua kukiadhibu chama kwa kupigia kura Chadema.

Habari zaidi toka ndani ya CCM zinadai kwamba, wakati kamati ya siasa ya CCM tawi la Nyasubi na ile ya kata ya Kahama mjini zilipendekeza ateuliwe mgombea anayekubalika, kamati ya siasa ya wilaya ilishinikiza kwa kuyakataa mapendekezo hayo ya vikao hivyo viwili ambavyo ndio mratibu wa kampeni.

Aidha, kutokana na mgongano huo viongozi waandamizi wa CCM wa tawi la Nyansubi, kata ya Kahama mjini na wilaya hawakushiriki kwenye kampeni za kumnadi mgombea Maganga kwa kuhofia kuzomewa na wananchi wenye hasira.

Wakizungumza na Tanzania daima kwa njia ya simu jana kutoka Kahama, baadhi ya wananchi walisema matokeo ya mtaa huo wa Korogwe ni fundisho kwa baadhi ya viongozi wa CCM wilaya na mkoa wa Shinyanga ambao wamekuwa wakitembea na wagombea wao mifukoni.

“ Sisi tuliwaonya viongozi wetu wa chama kuwa wasituchagulie watu waache wananchi watafute viongozi wao wenyewe sasa angalia yametokea haya. Tumeshindwa kwa sababu za kuangalia maslahi binafsi ya viongozi, hata pale ambapo wagombea hao hawana sifa za uongozi wanalazimisha,”alisema Leonard Mashaka.

Naye Juma Saliboko, mkazi wa kitongoji cha Nyihogo amesema, kama CCM haitabadilika na kuendelea kubeba wagombea wasio na sifa wasio takiwa na wananchi itavuna inachokipanda katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010.

Katika hali inayoashirika kazi ngumu kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa 2010, Kata ya Kahama mjini imepoteza mitaa miwili ya Korogwe na Majengo Mashariki baada ya kubwagwa na wagombea wa Chadema.

Hata hivyo, ushindi wa Chadema katika mtaa wa Majengo Mashariki uliingia dosari baada ya wakala wa CCM kukimbia na kura baada ya zoezi la kuhesabu kukamilika akipinga matokeo hali ambayo ilifanya msimamizi wa uchaguzi kubatilisha matokeo na uchaguzi mwingine kufanyika hivi karibuni.

mwisho

No comments:

Post a Comment