Popular Posts

Saturday, June 6, 2009

Wabunge kuwasha moto Dodoma

AHADI za rais Jakaya Kikwete, alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2005 na katika ziara zake mikoani, sasa zinatishia kutopitishwa kwa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010, baada ya wabunge kadhaa kulalamikia kutotengewa fungu la kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, huku ukiwa umebakia mwaka mmoja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao wa 2010.

Uchunguzi wetu kutoka ndani ya vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, vilivyokuwa vikipitia taarifa za makadirio ya mapato na matumizi ya kila wizara na mwelekeo wa bajeti kuu kwa ujumla, umebaini wajumbe wengi kuikataa bajeti kuu kwa madai kuwa haitekelezi ahadi nyingi zilizotolewa na rais Kikwete, na zile zilizoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005.

Miongoni mwa ahadi zilizoibua mjadala mkali ndani ya kikao cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, kilichofanyika Alhamisi iliyopita katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam, ni suala la ujenzi wa barabara mbalimbali nchini.

Wabunge kadhaa wamelalamikia mgawanyo wa fedha za bajeti hiyo kwamba umependelea ujenzi wa barabara zinazopita kwenye majimbo wanakotoka viongozi wa juu serikalini, akiwemo rais Kikwete mwenyewe na baadhi ya mawaziri.

Wabunge waliopinga zaidi ni wale wanaotoka kwenye mikoa yenye wabunge wengi, mikoa ya kanda ya ziwa na kanda ya kati, wakidai kuwa inapendelea eneo moja la nchi na kuwaacha watanzania wengine wakiteseka.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela (CCM), Anthony Dialo, alihoji ujenzi wa barabara ya Bagamoyo kwenda Msata hadi Mikumi, inayotoka nyumbani kwa rais Kikwete, na Waziri wa Miundombinu Dk. Shukuru Kawambwa, pamoja na barabara ya Handeni anakotoka Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi Dk. Abdalah Kigoda.

Barabara nyingine alizozilalamikia ni zile za Kilosa ambazo zimepewa fedha nyingi kutokana na kile alichodai kuwa zipo ndani ya jimbo la waziri Mkulo.

Mbunge wa Mvomero, Murrad Suleiman Saddiq (CCM), yeye alionyesha kukerwa na taarifa hiyo ya Waziri Mkulo, akisema haikugusa baadhi ya ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi wakati wa ziara zake alizofanya katika mikoa yote nchini, mwishoni mwa mwaka jana.

“…Nisipopata majibu nakwenda kwa rais kabla ya bajeti hii haijaenda bungeni. Desemba mwaka jana, rais alikuja Turiani Morogoro, akawaahidi wananchi kuwa katika bajeti ya mwaka ujao, zimetengwa fedha za kuwatengenezea barabara ya Turiani kwenda Magole, nashangaa kwenye bajeti hii haipo,” alisema Murrad.

Taarifa hiyo ya Waziri Mkulo, pia ilipingwa na Mbunge wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga (CCM), ambaye alisema hakuna haja ya kwenda bungeni kujidhalilisha kwa bajeti hiyo wakati imeandaliwa na wataalamu na wasomi wazuri ambao walipaswa kumshauri Waziri Mkulo kabla ya kuandaa ripoti hiyo.

“Tunasema kuwa tumeongeza bajeti kutoka shilingi trilioni 7.2 hadi 9.5, wakati kuna mfumuko wa bei na thamani ya shilingi imeshuka. Je, ongezeko la fedha limekwenda sambamba na hali halisi ya thamani ya pesa?” alihoji Kaboyonga na kuongeza:
„ Kuna vipaumbele vizuri vya uchumi, ambavyo serikali haitaji kama itaviboreshaje ili kuongeza mapato yake, mafano TICTS ameshakuwa kikwazo cha mapato bandarini, ni kwanini swerikali isifungue milango ya uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam, ili huyo TICTS apate mpinzani wake kibiashara?,”aliongeza.

Kamati hiyo ya Fedha na Uchumi inatarajiwa kukutana tena kesho kupitia marekebisho yatakayokuwa yamefanywa na Wizara hiyo, kabla bajeti hiyo haijasomwa rasmi bungeni juni 11 mwaka huu.

Hata hivyo, katika majumuisho yake kwa kamati, Mkullo hakuonyesha kusudio la kufanyia marekebisho mgawo wa fedha za barabara, na badala yake alisisitiza kuwa wafadhili waliotoa fedha hizo, ndio waliotaka fedha zao zielekezwe huko na si serikali.

Mkulo, alizidi kuwaeleza wabu nge wabunge waliokuwa wakilalamika kuwa wanaopaswa kuvisoma vitabu vya bajeti vizuri na kwa makini kwani miradi yote wanayoilalamikia imeainishwa huko na kupewa fedha.

Wakati bajeti hiyo ikiwa hatarini kupita, baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutajwa majina yao, pia wameelezea kuwepo kwa kusudio la kuipinga bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa sababu ya kile walichodai kuwa ni kukithiri kwa ufisadi ndani ya wizara hiyo na taasisi zilizo chini yake.

Baadhi ya wakubwa ndani ya wizara hiyo wanadaiwa kufanya maamuzi yaliyolikosesha shirika la hifadhi za taifa Tanzania [Tanapa], zaidi ya shilingi bilioni 50 katika mwaka huu wa fedha.

Fedha hizo zilikuwa zipatikane kutokana na mapendekezo ya bodi ya wadhamini ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), ya kutaka ada ya mahoteli kwa shirika hilo zipandishwe kutoka kiwango cha sasa cha asilimia zisizozidi 10 ya bei ya malazi na chakula kwa kila mtalii.

Kutokana na uamuzi wa vigogo wa wizara hiyo, Tanapa ambayo kwa mujibu wa mapendekezo hayo ilikuwa ikusanye shilingi zaidi ya bilioni 100 hadi mwisho wa fedha wa mwaka huu, sasa itaambulia bilioni 69 tu.

“Sio kweli kwamba matatizo ya mwaka huu ya Tanapa yametokana na mtikisiko wa uchumi duniani, bali ni uroho wa baadhi ya vigogo wa kufanya maamuzi mabaya. Hadi serikali ya awamu ya tatu inaondoka madarakani shirika hilo lilikuwa na akiba benki ya dola za marekani zisizopungua milioni 20”, alisema ofisa mmoja wa wizara hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili, umebaini kuwa ada nyingine zote ukiacha ambayo kigogo huyo amekataa kupandishwa zimepandishwa kwa asilimia kati ya 100 hadi 300 katika kipindi cha mika 10 iliyopita.

Tofauti na ada nyingine ada ya mahoteli haijawahi kubadilishwa tangu ilipowekwa miaka ya mwazo ya 1990 licha gharama ya malazi katika hoteli hayo ya kitalii kupanda mara kwa mara. Hivi sasa watalii hulipa kati ya dola za marekani kati ya 150 hadi 1000 kwa siku na kati ya hizo dola 10 hulipwa kwa Tanapa.

Inadaiwa kwamba,pamoja na TANAPA kuwa na sababu za msingi,kigogo huyo alikataa mapendekezo ya wataalam wake kwa shinikizo la wafanyabiashara.Licha ya ada hizo kuwa ziliwekwa zaidi ya miaka 15 iliyopita wenye mahoteli wamefanya mabadiliko ya kiwango cha malazi zaidi ya mara tatu kiwango kilichopitishwa na kigogo huyo ni cha kuifanya Tanzania iendelee kukosa mapato.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema kuwa utaratibu umeandaliwa wa kuhakikisha wabunge wanapata nafasi ya kupokea na kujadali taarifa za serikali juu ya utekelezaji wa maazimio 23, yaliyotolewa na wabunge juu ya Kampuni ya kufufua umeme wa tharura ya Richmond.

Dk. Kashililah, alizitaja taarifa nyingine zitakazo walisilishwa na serikali kuwa ni kuhusu hoja binafsi iliyowasilishwa Bungeni na Mbunge wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro, juu ya uuzaji wa Nyumba za serikali, Mkataba wa TICTS, na kampuni ya kuendesha huduma za Reli, (TRL), ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa imeshindwa kuboresha huduma katika sekta hiyo.

Na nyingine ni juu ya mkataba wa kuendesha mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira, ambao unadaiwa kuwa unamilikiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa na mshirika wake wa karibu aliyekuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya tatu Daniel Yona.

No comments:

Post a Comment