Popular Posts

Saturday, February 13, 2010

Wamiliki wa mabasi wagoma kufunga Speed gavana

Na Deogratius Temba

WAMILIKI wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA) wamesema hawatafunga vithibiti mwendo kwenye mabasi yao kama walivyotakiwa kufanya na serikali kwani kifaa hicho kimeshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa ya kupunguza ajali.

Pia wameitaka serikali kuwafutia leseni za udereva, na kuwafunga kifungo cha miaka mitano pamoja na kulipa faini madereva wote watakao bainika kusababisha ajali, pamoja na kutokuwalaumu wamiliki hao kwani wamekuwa hawahusiki na ajali hizo pindi zinapotokea.

Akitoa tamko lao la pamoja jana jijini Dar es salaam, kabla ya kumaliza mkutano wa wamiliki hao, Mwenyekiti wa TABOA, Mohamed Abdula, alisema hadi sasa hakuna basi lenye vidhibiti mwendo kwani wamebaini kuwa chombo hicho kinauzwa fedha nyingi na hakina kazi, licha ya kuwa kinaharibika haraka na kutokuzuia ajali.

“Tumekubaliana kwa pamoja kuwa kifaa hiki hakifai na hakina kazi, hatutakifunga kwenye magari yetu tena, tumekuwa tukimnufaisha mtu mmoja kibiashara tu, lakini hiki si sababu ya kuzuia ajali. unafunga ukifika hapo Kimara kinaharibika,”alisema

Alisema kifaa hicho kinafungwa kwenye gari ili lisiende mwendo wa zaidi ya kilomita 80 kwa saa lakini baadhi ya sehemu magari yamekuwa yakipata ajali yakiwa kwenye mwendo wa chini ya Kilomita 60.

“Hiki ni chombo ambacho wamekianzisha na sasa kimeshindwa kazi, hakitufai na hakikidhi haja, tumekifunga miaka 15 iliyopita lakini bado tunazungumzia ajali zilezile huku ni kupoteza fedha na muda tutafute dawa ya ajali,” alisema Abdula.

Pia wamiliki hao wa mabasi ambao kwa pamoja walikataa wawakilishi wa baadhi ya wamiliki kushiriki katika kikao hicho, walisema serikali ifuatilie kwa umakini dereva anayedhibitika kusababisha ajaili ashitakiwe kutumikia kifu ngo kisichopungua miaka mitano, na alipe faini kubwa ili kuwakomesha.

Alisema Dereva atakayesababisha ajali afutiwe leseni na kutoajiriwa tena katika kampuni yoyote nchini ili iwe fundisho na asiende kusababisha ajali mahali pengine.

Kwa upande mwingine wamiliki hao walikubalina kuwa serikali kupitia Mamlaka ya usimamizi wa barabara (Tanroads) iondoe matuta yaliyopo barabarani na mabasi yote ya abiria yaondolewe kwenye utaratibu wa kupitia kwenye mizani kupima kwani leseni inatolewa kwa kuzingatia idadi ya abiria na siyo uzito.

“Tunaiomba serikali iyatoe mabasi katika orodha ya magari yanayopita kwenye mizani, mizani zinasababisha foleni, magari yanarundikana hapo baadaye yakiachiwa yanaanza kukimbizana, Mizani zinasababisha rushwa sizizo na lazima, tunataka tuziondoe,”alisema

Pia walitaka ratiba ya kuanza safari ya mabasi katika vituo vya mabasi nchini ibadilike iwe kwa magari yote kuondoka kwa muda unaotofautiana tofauti na sasa ambapo hutofautiana kidogo na kusababisha kusindana njiani.

“ Tunaiomba ratiba ya safari ibadilike mabasi yaruhusiwe kutembea usiku ili kupungusa kufukuzana, leo hii ratiba inamalizika saa 5 asubuhi wakati wakiruhusu hadi jioni, tutaiona madereva wakiendesha polepole wakijua kuwa hawatazuiwa njiani” alisema

Kuhusu kutolewa leseni kiholela bila kuzingatia vigezo, TABOA walisema serikali idhibiti utoaji wa leseni na kama kuna askari wa usalama barabarani wanaohusika kuzitoa wadhibitiwe.

Kuhusu askari wanaosimamisha mabasi ghafla barabarani walisema hilo ni la kudhibiti kwani askari wamekuwa na tabia ya kujitokeza kutoka vichakani ghafla na kusimamisha mabasi na kusababisha magari kuanguka kw a kushika breki gafla.

Mwisho

No comments:

Post a Comment