Popular Posts

Saturday, February 27, 2010

Mzuri ya Mara yanazidi mabaya, Tuyazungumze!

Na Martin Malima

Mara ni moja mikoa ishirini na sita ya Tanzania . Mkoa huu uko kasikazini mwa nchi yetu, mpakani na Kenya . Miaka zaidi ya thelathini iliyopita ulikuwa ukitaja Mkoa wa Mara kwanza mtu anaelewa ni nyumbani kwa Mwl. Julius Kambarage Nyerere rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania na pili ni mkoa ambao kuna mbuga kubwa ya Serengeti.

Utambulisho wa mkoa huu kwa hivi karibuni umekuwa ukibadirika na hii inatokana na hali ya kiusalama na vitendo vya kiharifu katika eneo dogo la mkoa huu. Hili ni eneo la Tarime ama wilaya ya Tarime.

Tarime ni moja kati ya wilaya tano za mkoa wa Mara. Wilaya nyingine ni Musoma, Bunda, Serengeti na Rorya. Eneo hili ndilo linalosemwa kuwa ni eneo ‘korofi’ kiusalama. Wenyeji wa wilaya hii ni wakurya na ndio wanaobeba idadi kubwa wa wakaazi wa wilaya hii. Mbali na Tarime wakurya pia wanapatikana katika wilaya za Serengeti na Rorya.

Wakurya ni mojawapo ya makabila mengi yanayopatikana mkoani Mara. Makabila mengine ni Wajita, Wazanaki, wajaruo, wasimbiti, wakabwa, wakwaya na mengine mengi.

Licha ya kuwa na makabila mengi lakini utajapo kuwa wewe ni mwenyeji wa mkoa wa Mara basi watu hukuchukulia kuwa wewe ni mkurya. Hii ni kutokana na historia ya kabila hili, ukubwa wake na matukio ya kusikitisha yanayofanyika katika maeneo machache wanayoishi hususani wilayani Tarime.

Imefikia hatua ambapo jambo lolote la kiharifu litokeapo mkoani Mara watu hulizungumza kikabila ama kiwilaya zaidi. Hata kama tukio limetokea Bunda watasema kwamba limetokea Tarime na wahusika ni wakurya.

Mfano ni mzuri ni wa bwana mmoja alipokuwa akaiyahusisha mauaji ya watu 17 wafamilia moja yaliyotokea eneo la buhare mjini Msoma na hali ya usalaama Tarime kilometa zaidi ya 50 kutoka eneo la tukiio. Bwana huyo aliongeza kuwa walofanya mauaji hayo ni wakurya. Yawezekana ni kweli wamefanya wao lakini hata wachaga na wasukuma wanaweza katika kundi la hao waliofanya hayo mauaji.

Ni ukweli sio pingika kuwa kumekuwa na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kuvunja sheria katika maeneo la Tarime, na kwa sababu hiyo serikali ilianzisha mkoa maalumu wa kipolisi wa Tarime/Rorya.

Ni zaidi ya mwaka sasa tangu mkoa huu uanzishwe. Kwa wale wanaoifahamu Tarime vizuri watakubaliana na ukweli kuwa hali ya usalaama katika eneo hili ilikuwa mbaya.

Na pia ni ukweli usiopingika kuwa hata pasipo nguvu ya takwimu kwamba kanda maalumu ya kipolisi ya Tarime/Rorya chini ya Kamanda Costantine Massawe imejitahidi sana kuirekebisha Tarime.

apigano ya koo na koo, wizi wa mifugo na mauaji ya kihorela ya kulipiza kisasi ndio yanayoifanya Tarime izungumzwe vibaya . Kwa sasa vitendo hivi vimeepungua kwa kiasi kikubwa.


Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa ukweli huu unakwepwa kuzungumzwa na badala yake wanazungumzia historia. Na mbaya zaidi baadhi ya viongozi waandamizi Serikalini na wanasiasa wamekuwa wakiendeleza mazungumzo ya namna hii. Hawa ni wale wanaoifahamu Tarime ya zamani, wale walio nje eneo hilo na wale ambao hawajawahi kufika Tarime. Hawa ndio wanachangia kuipaka matope Tarime kwa kusambaza taarifa za kihistoria.

Imefikia hatua kuonekana kuwa kila mkazi wa Tarime ama Mkurya ni muharifu. Na kwa sababu Tarime imechukuliwa kuwa ndo mkoa mzima wa Mara, wengine wamefikia kuufananisha mkoa mzima na Darfuu. Kauli kama hizi ama mitazamo ya na mna hii inaweza kuwafanya hawa watu wachache wenye tabia za kikatili wajione kuwa ndivyo wanavyopaswa kuwa na itakua ni vigumu kwao kubadirika.

Mbaya zaidi sifa hizi mbaya zimekuwa zikivuka mipaka ya wilaya na kuwa za mkoa mzima. Ebu jaribu kufanya utafiti wako mdogo juu ya mitazamo ya watu kuhusu mkoa wa Mara. Waulize wanapata picha gani wasikiapo mkoa wa Mara?. Niliwauliza watu kumi ambao sio wenyeji wa mkoa wa Mara swali hili. Nane walisema kuw wasikiapo mkoa wa Mara kitu cha kwanza kuja katika akili zao ni uhalifu uliopindukia, mapigano, mauaji na kilimo cha bangi.

Mmoja kati ya hao kumi aliungana na majibu ya watu nane lakini akaongeza kuwa pia hukumbuka raha alizowahi kuzipata alipokuwa mkoani Mara. Mwingine akasema kuwa asikiapo mkoa wa Mara anakumbuka neema zilizoko katika mkoa ule. Kuna ardhi nzuri kwa ajiri ya kilimo, ufugaji, madini, wingi wa chakula na mboga hasa samaki.

Mawazo ya watu kumi yanatoa picha halisi ya jinsi mkoa huu unavyotafasiliwa. Yale yanayo tokea Tarime yanawasilishwa kana kwamba yanatokea katika maeneo yote au wilaya zote za mkoa wa Mara, wakati sivyo.

Chimbuko la mawazo haya ni uwepo wa taarifa zisizo sahihi juu ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla. Hii inatokana na wanaozungumza kutouufahamu vizuri Mkoa wa Mara na kuendelea kuamini taarifa za kihistoria kuhusu Tarime.

Sehemu kubwa ya mkoa wa Mara ni shwari. Wilaya za Musoma, Bunda, Rorya na Serengeti ni tulivu. Lakini inasikitisha kusikia ama kusoma kwenye magazeti kuwa mkoa wa Mara ni ‘hatari kiusalama’.

Ni wakati mahususi sasa kuzungumza uzuri wa Tarime na mkoa wa Mara kwa ujumla. Wana habari waende Mkoani Mara wakatafiti mkoa huo kwa ujumla ili watuambie ukweli juu ya hali ya usalama ya mkoa huo. Watanzania wana haki ya kujua kama ni kweli mkoa huo umejaa machafuko, mauaji na ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa kiwango kinachoripotiwa au ni wilaya moja tu ya Tarime. Kisha waende Tarime wakatafiti juu ya hali ya usalaama ya pale. Watueleze kama hali ilivyokuwa zamani ni ni sawa na ya sasa.

Kuendelea kuizungumza Mara ama Tarime kwa ubaya hakuna tija na kunarudisha nyuma jitihada za kuleta maendeo.

Wasomi na wanaharakati wa kiafrika wamekuwa wakilalamikia jinsi vyombo vya habari vya kimataifa vimekuwa vikilipoti juu ya Bara la Afrika kwamba ni bara lililo jaa machafuko na umasikini wakupindukia. Jitihada za kujiletea maandeleo na amani katika bara la Afrika zimezikipewa nafasi finyu kwenye vyombo hivi na wakati mwingine hakuna kabisa.

Hii haina tofauti na vyombo vya ndani vya habari vinavyolichukulia suala hali la mkoa wa Mara na Tarime. Ni vyombo hivi hivi vimewafanya wananchi waamini kuwa yanayotokea Tarime ndiyo picha halisi ya mkoa wa Mara. Wameshindwa kutuambia ukweli kwamba hali ya usalaama katika wilaya ya Tarime imeboreka tofauti na wakati kabla ya kuwa na kanda maalumu ya kipolisi ya Tarime/Rorya.

Shughuli zote za maendeleo zinaendelea mkoani Mara na Tarime zinaendelea kama ilivyo katika wilaya nyingine katika mikoa mingine zinaendelea kama kawaida.

Wananchi wa Tarime wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kamawalivyo wananchi katika maeneo mengine. Tarime wana uhaba wa walimu, huduma za afya na huduma nyingine za kijamii na wataalamu katika fani mbalimbali.

Kama ilivyokatika maeneo mengine hasa vijijini elimu juu ya haki za binadamu hasa hazi za wanawake na watoto na elimu ya afya inaitajika.

Serikali imekuwa ikijitahidi kwa kushirikiana na wadau binafsi imekuwa ikiboresha hali hii kwa kupeleka wataalamu. Lakini wataalamu gani kwenda ama kukaa Tarime wakati mmekwisha watisha kuwa ‘hakufai?’

Kama tukiendelea kuizungumza Tarime kwa ubaya kuliko uzuri wake ambao ni mwingi hatutapata walimu wakwenda kufanya kazi Tarime. Huduma za afya zitaendelea kudorola kwani watakao kuwa wakipangiwa kwenda katika maeneo haya watakuwa eidha wakigoma kuripoti au kuomba uhamisho. Matokeo yake wananchi wataendelea kuumia kwa kukosa huduma za msingi za kijamii na kitaalamu.

Naomba nisieleweke kuwa napinga mijadara juu ya hari ya usaalama au kuficha ukweli wa yale yanayotokea Tarime na mkoa wa Mara, la hasha. Mkoa wa mara unamapungufu yake kama ilivyo mikoa mingine, lakini tusiegemee madhaifu haya na kusahau mazuri yake ambayo ndio mengi.

Mauhaji yaliyotokea pale buhare hayanatofauti na matukio ya kuchuna ngozi kule wilayani Mbozi mkoani Mbeya na mauaji ya vikongwe kule shinyanga, hayana tofauti na mapigano na mauaji ya kilosa mkoani Morogoro, Manyara na Arusha. Au yanatofauti gani na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera. Licha ya matukio haya yakutisha sifa za mikoa hii imebaki palepale.

Tarime ni sehemu nzuri ya kuishi, kuwekeza na kufanya kazi na ndio maana akina Mushi, Rweyemu, Mwakibinga na Masanja wapo. Ingekuwa ni hatari kama invoelezewa hawa wasingeishi.

Mimi sio mwenyeji wa mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment