Popular Posts

Monday, December 7, 2009

Sumaye ahofia wasomi wa shule za Kata
*Paroko awapasha wasiong’atuka
Na Deogratius Temba

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Feredrick Sumaye, amesema serikali isipochukua hatua za haraka kuangalia mahali pa kuwaweka wanafunzi wanaohitimu elimu ya kidato cha nne, utawala utakuwa mgumu.

Akizungumza katika ibada ya kuweka jiwe la msingi la Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Fransis, kinachomilikiwa na Parokia ya Pugu, chini ya Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es salaam, iliyoko nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, Sumaye, alisema kumekuwepo na kampeni kubwa za kujenga shule za sekindari za kata bila kuandaa mahali pa kuwaweka baada ya kuhitimu.

“Vyuo vya ufundi ndiyo kimbilio kubwa la vijana watakaomaliza kidato cha nne katika shule za kata. Watu wanafikiri kuwa tukisha jenga shule hizi za kata tumemaliza, vijana hawa ukiwaambia wakalime kwa jembe la mkono hawatakubali, biashara hawawezi tutabanana huku huku mitaani, hali itakuwa mbaya na utawala utakuwa mgumu kweli kweli,” alisema Waziri Mkuu huyo mstaafu.

Akizungumza pole pole mbele ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, Mwadhama Polcarp Kadinali Pengo, Sumaye, aliendelea kusema kosa lilofanyika hapa nchini tangu awali ni kutokudhamini elimu ya ufundi, na kuamua kuwekeza zaidi katika elimu ya sekondari tukifikiri kuwa elimu hiyo ndiyo bora zaidi.

“Sisi nchi hii hatukuwekeza katika elimu ya ufundi, viwanda tulivyokuwa navyo vilikufa kwasababu hatukuwa na wataalamu. Tumepuuza kabisa elimu hiyo tukadhani sekondari ni muhimu sana kuliko ufundi,” alisema Sumaye

Alisema nchi zilizoendelea sana kiviwanda ziliwekeza katika elimu hiyo, na nchi isiyo wekeza katika elimu haiwezi kupambana na umasikini.

“Bila mchango wa kanisa Katoliki katika sekta ya elimu sijui kama serikali ingeweza kutoa elimu kwa watu wote hawa. Kama siyo mchango wenu kazi ingekuwa ngumu kweli,” alisema Sumaye.

Aidha alisema eneo hilo la Pugu ambapo Chuo hicho kitajengwa ni muhimu na ni la kihistoria kwahiyo linapaswa kuheshimiwa,kutokana na kuwa ni mahali marehemu Baba wa taifa alipoanzia kazi na harakati za ukombozi za taifa hili kuanzia hapo.

Alisema Chuo hicho ni lazima kiende sambamba na hadhi ya Baba wa taifa, bila kulegalega kwani mgeni atakapofika Pugu anategemea kuiona taswira ya Baba wa taifa mahali hapo hasa watu wakiheshimu na kuzienzi falsafa zake .

Akizungumza paroko wa Parokia ya Pungu, ambayo ndiyo inayosimamia Chuo hicho Padre Leonadro Amandori, aliwataka viongozi wanaong’ang’ania madaraka kumuiga hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuachia madaraka kwa hiari badala ya kusubiri kufukuzwa.

Paroko huyo, alisema jamii hasa viongozi wanapaswa kumuenzi Baba wa taifa kimatendo na siyo kufurahia hotuba zake na kuzisikuiliza tu.

“Tunataka tumuenzi kwa matendo yetu, na siyo kubaki kusikiliza wosia na kuufurahia. Tunataka tumuenzi kwa vitendo. Mimi nilizungumza naye Mwezi Novemba 1985, mara baada ya kustaafu, akaniambia kuwa ameamua kung’atuka kabla ya kung’atuliwa, hii ni kauli ambayo ni fundisho kubwa sana kwa viongozi wang’ang’anizi wa madaraka.,’alisema

Alisema kanisa limeamua kukijenga chuo hicho katika eneo hilo ili nyota ya Baba wa Taifa ing’ae katika eneo hilo na watu wabadilike.

Chuo hicho kilinachangiwa kwa kiasi kikubwa, familia moja kutoka Italia Kaskazini, ambayo imetoa fedha zote ilizolipwa kama fidia na shirika la Bima baada ya watoto wao kufariki kwa ajali ya gari.

Kwa mujibu wa Padre, Amandori, familia hiyo ya wazazi Juliano na Maria Cassano, iliwapoteza watoto wao Rojero na Andrea katika ajali mbili tofauti lakini kiasi cha fedha zote walizolipwa kama fidia wamezitoa kwa ajili ya kujenga Chuo hicho cha Ufundi.
Habari hii imetoka katika gazeti la Tanzania Daima la JUmatatu 7/12/2009
Mwisho

No comments:

Post a Comment