Popular Posts

Wednesday, December 9, 2009

Askofu ahuzunishwa na matusi ndani ya CCM

Na Deogratius Temba

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Wokovu la Kipentekoste chini, Edger Mwamfupe, amewataka makada na viongozi wa Chama cha Mapinduzi(CCM), kuacha mara moja tabia ya kurushiana maneno machafu hadharani kwani ni kuonyesha utovu wa nidhamu na kukosa maadili.

Pia amemtaka rais Jakaya Kikwete, kutojibizana na wanasiasa wenzake wa CCM waliojitokeza kupinga utendaji wake kwani yeye ni kiongozi mkubwa wa taifa hili na hapaswi kupoteza muda wake kujibizana na watu waklati nchi inazidi kuwa masikini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima jana na jijini Dar es salaam, bila kutaja majina ya viongozi hao, askofu Mwamfupe, alisema tabia iliyojitokeza hivi karibuni ya makada wa CCM, kutoa maneno machafu ni y a aibu kwa wenzao na ni ya kitoto, na ya kujidhalilisha wenyewe kwani siasa siyo kutoa matusi hadharani.

“Tunategemea viongozi wa Chama wanapokuja kwa wananchi waje kunadi sera na kuzungumzia namna ya kuondoa kero siyo matusi, nasikitika sana nchi hii itaingia katika machafuko tusipochukua hatua kwa hili,” alisema Askofu Mwamfupe.

Alisema kiongozi anapotoa lugha chafu anaonyesha wazi kuwa amepungukiwa na maadili, na inaonekana wazi kuwa siyo mcha Mungu, kwani hakuna mahali ambapo sera ya chama chochote inaruhusu matusi au lugha chafu.

“Unapoanza kurusha maneno machafu unaonyesha wazi kuwa huna maadili, au hukufunzwa vizuri utotoni, viongozi wetu wanapaswa kuchunga ndimi zao na kujiheshimu, na hata maandiko yanasema hivyo kuwa ulimi ni hatari ni lazima udhibitiwe,” alisema

Alisema kuwa watanzania wanahitaji kufikiria namna ambavyo nchi yao itatoka katika hali ya umasikini na kuipeleka panapotakiwa lakini viongozi wanapopoteza muda kujadaili watu, kurushiana maneno hali hiyo inapoteza mwelekeo wa taifa na kuifanya nchi iendelee kuwa masikini.

Pamoja na kuwa hakutaja majina ya makada wanaonikana hadharani kwa matusi ndani ya CCM lakini ni dhahiri kuwa alikuwa akiwalenga Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake(UWT), Sophia Simba na wenzake ambao hivi karibuni walirushiana maneno ya nguoni wakati wa mkutano wa wabunge wa CCM na Kamati ya Mzee Mwinyi mjini Dodoma.

Aliendelea kusema kuwa hakuna aliye msafi ndani ya CCM, na nilazima lieleweke hivyo kuwa wanaowanyoonyesha wenzao vidole wanatakiwa kuwa kimya wajisahihishe kwanza wao.

“Hata Bwana Yesu alisema aliye mwema kuliko huyo Mwanamke na awe wa kwanza kurusha jiwe, je hao wanaopiga kelele ni wasafi? Hao wema wao wametoka wapi wakati wamekulia katika mazingira na mfumo huo huo inaowafanya wenzao wawe wachafu?” alihoji Askofu huyo.

Akizungumzia kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi, wakati anawasili nchini kuwa atajibu mapigo kwa wanasiasa na makada wa chama hicho waliiomnyooshea vidole kuwa hajafanya kitu na amekumbatia na matajiri katika serikali yake alisema:

“Kama ningekutana na Rais, ningemshauri, asijaribu kujibiana na watu. Kwanza rais ana majukumu makubwa ya kuongoza taifa, nchi ipo katika matatizo ya umeme, maji, umsikini na watu wengi zaidi ya milioni 40 wanamtegema kwanini atumie muda kujibizana na watu?

“Ni kweli kuwa rais amekasirishwa na hali hiyo. hata kama ni wewe unatoka safari unafika tu nyumbani unakutana na matusi, utakasirika lakini kwa kiongozi wa nchi hutakiwi kujibizana na watu, unayapokea matusi hayo unavumilia unaendelea kuchapa kazi, ujiimarishe zaidi katika kuleta m,abadiliko. huo ndiyo uongozi,” alisema.

Akizungumzia malalamiko ya wanasiasa kuwa rais ameweka marafiki zake katika Baraza la Mawaziri na sehemu nyingine nyeti serikalini, alisema kwa hilo rais yeyote hana jinsi ya kujitetea kwani katika awamu zote za uongozi wa taifa hili marais wameingia na marafiki zao.

“Ina maana Hayati Mwalimu Nyerere hakuweka Marafiki zake? Hawa akina Mzindakaya, Rupia, Sykes wametoka wapi, waliingiaje serikalini kama siyo urafiki na rais wa wakati huo ,”alihoji Askofu Mwamfupe.

Habari hii imechapwa pia katika gazeti za Tanzania Daima la Alhamis 10/12/2009
Mwisho.

No comments:

Post a Comment