Popular Posts

Tuesday, December 1, 2009

Ripoti ya Maaskofu, Masheikh katika migodi ya madini nchini -2

Ziara Wilayani Geita na Tarime

Na Deogratius Temba

KAMA tulivyoanza wiki iliyopita ripoti hii ilitoa utangulizi wake na kile ambacho maaskofu wameazimia na lengo la kufanya ziara hiyo.

Wiki hii tuna angalia viongozi hao wa dini wakiwa ndani ya migodi ya madini wakingalia hali halisi ya watanzania wanaofanya kazi humo, pamoja na wale wanaoishi jirani na migodi.

SAFARI yetu, ilitufikisha katika wilaya mbili muhimu katika masuala ya migodi ya madini, kwa lengo la kuweza kusikia na kujionea hali halisi za wananchi wa Geita na Tarime.

Tukiwa njiani kuelekea Geita, msafara wa viongozi wa dini ulipata fursa kwa kujadiliana kwa kina kuhusu maisha ya wenyeji wa Geita. Majadiliano haya yalimshirikisha mzee wa siku nyingi aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa katika miaka ya mwanzoni ya serikali ya awamu ya kwanza kuhusu madini mengi yanayopatikana nchini.

Wakafahamishwa pia kuwa kulikuwa na mikakati ya wakati huo ya kuwa na mpango wa madini ambao ungewalinufaisha wananchi wote, na kwamba mara kwa mara Mwalimu Nyerere alisisitiza kuhusu dhamira yake ya kusubiri kwa muda muafaka na watu watakaochimba madini.

Wilaya ya Geita na mgodi wa dhahabu wa Geita

Katika wilaya ya Geita, tulimtembelea Mkuu wa wilaya kumfahamisha kuhusu ziara yetu pamoja na kupata maelezo rasmi ya msingi kutoka kwa viongozi wa serikali wa eneo husika. Katika ofsi ya Mkuu wa wilaya tulipatiwa maelezo kuhusu maisha ya wakazi wa maeneo mbalimbali yenye shughuli zilizoanzishwa za uchimbaji wa madini. Pia tulielezwa historia ya Mkoa na hali ya kisiasa ya wilaya hiyo.

Kutoka hapo tulikwenda katika ofisi ya mgodi wa dhahabu wa Geita. Tukiwa njiani kueleka huko tuliweza kuona marundo ya vifusi vya mawe na kushuhudia hali halisi ya maisha ya watu wanaoishi karibu na migodi.

Katika mgodi wa dhahabu wa Geita tulipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Derek Walters, tukapelekwa katika ukumbi maalumu ambako tulipatiwa maelezo kuhusu shughuli za mgodi na pamoja na mipango yao ya baadaye. Pamoja na maelezo mengine yaliyotolewa, yafutayo yalikuwa na uzito wa kipekee kwetu.

Kampuni ilikwishatumia mtaji wa kiasi cha sh. bilioni 500, huku bado ikiwa na hofu kuwa ingeweza kupata hasara kwa mwaka unaofuata.

Shughuli za mgodi wa dhahabu, wa Geita katika Tanzania zitaendelea kwa miaka kati ya 25 na 30. kampuni bado inampango wa kufanya utafiti zaidi wa madini na kuanzisha migodi katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini Tanzania.

Swali letu ni kwamba, kama kampuni ina hofu ya kupata hasara kwanini inampango wa kupanua zaidi shughuli zake nchini?

Kampuni ya mgodi wa Dhahabu wa Geita inatoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania, hatukuweza kujua au kuelezwa kama inatoa kiasi gani na hadi sasa imeshatoa mchango kiasi gani.

Kampuni ya Mgodi huo, imewalipa fidia ya dola za Kimarekani kiasi cha Sh. Milioni 1.5 wakazi walioondolewa katika maeneo ya kupisha shughuli za uchimbaji.

Maji yatumikayo huvutwa kutoka katika ziwa Victoria kwa kutumia mitambo maalumu. “mabomba yetu yamepitia Katoma na maji taka humwagwa katika mabwawa maalumu ya maji taka, kwa hali hiyo hakuna uchafuzi wa vyanzo vya maji yanayotumiwa na wakazi wa maeneo haya tunazingatia viwango vya kimataifa katika kila tulifanyalo, na tuko tayari kukaguliwa,”alisema Mkurugenzi huyo.

Kila mwaka Kampuni ya Mgodi wa Dahahabu wa Geita, huilipa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Dola za Kimarekani 250,000. Taarifa hii inapingana na ile tuliyoipokea kutoka halmashauri ya Manispaa ya Geita wao wanakiri kupokea Dola 200,000 tu.

Baada ya mkutano wetu na wamikliki wa migodi, tulikutana na familia 86 zilizoondolewa kwenye maeneo yao kupisha uchimbaji wa madini, halafu tukatembelea maeneo ya Nyarugusu, Nzega na Bulyanhulu kabla ya kurejea Mwanza.


Wilaya ya Tarime na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara

Kundi jingine la viongozi wa dini lilitembelea mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Barrick Gold.

Ziara hii ilitoa picha tofauti na ile iliyoshuhudiwa na kundi la kwanza. Wakati kundi lilokwenda Mwanza lilipata taarifa kutoka kwa viongozi wa serikali na wamiliki wa mgodi, kundi lililokwena Mara lililazimika kukaguliwa sana na pamoja na kutakiwa kukabidhi simu zao za mikononi na kamera kwenye lango kuu la kuingilia mgodini.

Waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara huo hawakuruhusiwa kuingia katika eneo la mgodi. Zoezi nzima la kuchuja nani aingine ni asiingie halikuwa la kibinadamu na lilichukua takribani muda wa dakika 45.

Kutokana na kupoteza muda mwingi katika lango kuu la kuingilia hakukuwa na muda wa kufanya mkutano na kuzungumza na uongozi wa mgodi. Baada ya utambulisho viongozi wakiwemo makatibu wakuu Maaskfu na Masheikh waliokuwemo kwenye msafara huo walieleza kutoridhika kwao na zoezi nzima

Kutoka pale mgodini msafara ulitembelea jamii ya maeneo ya karibu na mgodi huo wakajionea wenyewe na kujadiliana na wenyeji hao kuhusu hali zao pamoja na maisha yao kwa ujumla kabla na baada ya kuanzishwa kwa shughuli za uchimbaji mkubwa wa madini katika eneo lao.

Katika ziara za makundi yote mawili, yalibainika mambo mengi ambayo yalikuwa na adhari zinazofanana kwa jamii mbalimbali. Mambo hayo yataelezwa katika mfululizo wa taarifa hii unaofauta.

Usikose sehemu ya tatu ya taarifa hii wiki ijayo tutaangalia ukuaji wa Uchumi unaozingatia Utu.

0784 /715 686575
Inapatikana pia katika mtandao: www. deotemba.blogspot.com

No comments:

Post a Comment