Popular Posts

Monday, December 7, 2009

MIAKA 48 YA UHURU WA TANGANYIKA,TUNAELEKEA UTUMWANI

Na Deogratius Temba

LEO ni miaka 48, tangu Tanganyika sasa (Tanzania), ilipopata uhuru wake kutoka kwa utawala wa Kiingereza na kufunguliwa katika minyororo ya ukatili,ubeberu, na unyasanyasaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni kwa waafrika.

Taifa lolote linapoadhimisha kumbukumbu hizi linawaweka wananchi wake katika hali ya kutafakari na kutadhimini hali halisi ya kisiasa, kiuchumi na hata kimafanikio ambayo ymetokea kwa kipindi chote hicho. Leo taifa linapaswa kutangaza mafanikio ambayo linajivunia ikiwemo kiwango cha uhuru ambacho wananchi wake wanakipata ukiacha uhuru wa bendera tulionao.

Ieleweke kuwa uhuru wa bendera ni ule ambao nchi ni taifa huru, inapepea bendera lakini nchi hiyo inawezekana watu wake wasiwe huru, kiuchumi, kimawazo, na hata kiakili.

Wakati tunaingia katika uhuru, Desemba 9, 1961, hali ya nchi haikuwa kama ilivyo leo. Tunakiri na tunapaswa kujivunia mahali tulipopiga hatua hali ya Miundombinu imeimarika na imebadilika.

Hoja ya leo, si kujadili mafanikio ambayo yametokea kwani yanaonekana waziwazi na kila mtu anayejua historia anaona ni wapi tumepiga hatua na tulipokwama.

Nia ni kutaka kuonyesha jinsi ambavyo kwa kipindi cha miaka hii 48, taifa linarudi utumwani yaani tunajikabidhi wenyewe katika mikono ya mkoloni na kumwambia tumeshindwa kijiendesha tusaidie, tutawale na tusimamie.

Taifa hili lipo njia panda kutokana na kujirudisha lenyewe katika mikono ya Mkoloni. Matajiri wanasiasa wachafu na wawekezaji wasiozingatia taratibu na ukiukwaji wa taratibu za kazi na mikataba ni sehemu ya ukoloni tena mbaya zaidi ya ule wa awali.

Tanzania ya leo ipo mikononi mwa watu wachache, taifa linaendeshwa na wenye fedha kama huna fedha huwezi kuuliza kitu. Dola si ya umma tena, Binadamu hana uhuru wala haki.

Ushahidi wa kuwa fedha imemeza uhuru wetu wote ni kukua kwa tabaka kati ya masikini na tajiri. Hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, hakutarajia hilo kurejea Tanganyika na hata Tanzania ya leo, maana alijua kuwa ubaguzi, unyanyasaji na mabaya mengine yalikuwa yanamalizika siku ya kukabidhiwa taifa huru lakini hadi leo ni kinyume chake.

Maisha ya mwekezaji yanatofautiana kabisa na ya mzawa ambaye nchi yake ndiyo ina rasimali. Anayemiliki ardhi yenye madini anaishi kwa shida lakini mgeni anaishi kwa raha starehe tena maisha ya kifahari, wakati fedha hizo anazitoa katika ardhi ya Mtanzania huyo huyo anayeishi chini ya pato la Sh. 500 kwa siku.

Akihubiri katika ibada ya Usiku ya Krimas, ya mwisho ya karne ya 20, Mhashamu Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, alisema "Haiwezekani kwa sababu mimi ni mwekezaji, nikahalalisha kuishi kwa dola 150 kwa siku, lakini Mwafrika anayeishi mazingira hayo hayo, mwenye mahitaji hayo hayo, akahalalishwa kuishi kwa senti 80 kwa siku. Kama huu si utumwa mambo leo, tuuite nini?"

Maneno hayo yana kila chembe ya mguso wa nafsi na ukweli ndani yake, Tangu Tanzania ilipopata uhuru,hususan baada ya Azimio la Arusha (1967) njia zote kuu za uchumi zilimilikiwa na Umma.

Hii iliweza kupunguza kasi ya kupanuka kwa matabaka ya walio nacho na wasio nacho. Na kwa namna moja ama nyingine mfumo huu ulisaidia zaidi kwa kiasi kikubwa matunda ya jasho la Watanzania yalibaki Tanzania.

Hivi labda suala la kujiuliza ni kuwa ubinafsishaji na uwekezaji unaongeza ajira kwa Watanzania au la? Unaboresha huduma za kijamii kwa gharama ambazo mwananchi wa chini anaweza kumudu?

Kama alivyosema Askofu Shayo siku kama ya leo hatuwezi tukawa na furaha anayodai kama masuala nyeti yanayohusu haki na amani hayatiliwi mkazo

Kwa mtazamo wangu, sina shaka kuwa hayupo wa kupinga kuwa uvunjaji wa haki ndicho chanzo cha vita katika jamii, umaskini wa kupindukia kwa wachache na utajiri wa kupita kiasi kwa wachache. Hilo pia ndilo chanzo cha ujinga unaozuia maisha ya furaha ya watu wanyonge, magonjwa, udikteta, maafa yatokanayo na siasa na dini na kupitishwa kwa malengo yasiyokidhi mahitaji ya kweli ya jamii , na hata uchu wa madaraka usiokubali mabadiliko.

Wapo wengi miongoni mwetu waliopo jela, wengine wananyimwa haki zao huku wengi wakitumika kama vitega uchumi na zana za kuzalisha mali za wenye uchu wa mali; wasiotaka kugawana kidogo kilichopo pamoja na nguvu kazi zao.

Haitoshi kukaa mchana kutwa; usiku kucha huku tukiimba nyimbo zote na kuvaa mavazi yote yanayoashiria furaha, amani na haki ya Ukombozi(Uhuru), kama hatujui suala la moyo unaotafuta amani ya kweli. Ni dhahiri kuwa kwa mtindo huo haiwezekani kufukia utumwa na ukoloni mamboleo tulio nao.

Kwa hiyo basi, ili tuweze kuishi kwa amani na furaha na kushangilia vizuri nusu karne ya Uhuru wetu, wale wote waliokabidhiwa dhamana ya kuliongoza taifa hili wayaangalie masuala haya kwa kina na wigo mpana. Wawe na sauti thabiti ya kukemea unyanyasaji wa waajiriwa au uovu wowote unaoweza kufanyika kutokana na dhamira mbaya zinazoweza kuwapo miongoni mwa waajiri wa kigeni na hata wa hapa hapa nchini.

Kama hospitali zetu hazina madawa, elimu bado inashuka kiasi cha kutisha licha ya utitiri wa shule za kata na za binafsi zisizoweza kujiendesha badala yake zimekuwa ni biashara tu na bado udhaifu wa watendaji kadhaa serikalini unawapa mwanya wachache kuwa matajiri kupindukia na wengine kugeuka watumwa, nchi inastahili kuimba wimbo na amani na upendo? Je itajikomboa kiuchumi?
Je huku siyo kurudi utumwani?
0784/715 686575
deojkt@yahoo.com
www.deotemba.blospot.com


Mwisho

No comments:

Post a Comment