Popular Posts

Saturday, November 21, 2009

Miaka 10 ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,Matumaini ya Wananchi yametimia?

Na Deogratius Temba
SIKU ya Ijumaa, Novemba 20 mwaka huu, Marais watano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, walikutana mjini Arusha kuhitimisha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa Jumuiya hiyo.

Marais hawa, Paul Kagame (Rwanda) Yoweli Museveni (Uganda) Mwai Kibaki (Kenya), Piere Nkurunzinza (Burundi) na Mwenyeji wao, Jakaya Kikwete wa Tanzania, walihitimisha maadhimisho hayo kwa kusaini mkataba wa nyongeza ( Protocol) wa soko la pamoja kwa nchi hizo.

Mkataba wa nyongeza wa soko la pamoja ni moja ya makubaliano manne yaliyo kwenye kifungu cha tano cha mkataba wa EAC na hadi sasa suala lililotekelezwa ni la ushuru wa forodha na suala la soko la pamoja ni la pili kutakiwa kutekelezwa.

Katika mkataba huo soko la pamoja baraza la mawaziri wa EAC wamekubaliana kuunganisha soko la bidhaa za Afrika Mashariki, kushirikiana katika masuala ya ajira, masuala ya kuhamisha mitaji na masuala ya huduma za kijamii na masuala ya kibiashara.

Hii ni siku ya kihistoria kwa nchi hizi wananchama, kwani itakumbukwa kwa vizazi na vizazi kutokana na umuhimu wa tukio husika na jinsi ambavyo linagusa maisha ya wananachi wote katika nyanja ya kiuchumi.

Kusainiwa kwa mkataba huu wa nyongeza, ni sehemu ya makubaliano ya mkataba wa jumuiya hii, na ni hatua ya kuimarisha mahusiano hasa ya kibiashara ambapo sasa milango inafunguliwa kwa wananchi wa nchi wanachama kuwa huru kufanya biashara bila kuwa na mipaka.

Hatua hiyo ya kuwapo makubaliano ya soko la pamoja ni mwelekeo wa kwenda katika sarafu moja na shirikisho la kisiasa kwa nchi za Afrika Mashariki.

Tangu kuzinduliwa jumuiya hii, Novemba 30 mwaka 1999, kuna hatua ambazo zilipangwa kufikiwa ili kuifanya jumuiya hii isaidie maendeleo kwa nchi wanachama, kuepesha migogoro na vurugu na kujenga ustawi wa kijamii kwa wananchi wake ambao wanakadiriwa kufikia milioni 120.

Binafsi ninaweza kusema kuwa baadhi ya malengo yaliyopangwa yamefikiwa, na baadhi hayakufikiwa na yanaendelea kuzua zua.

Bunge la Afrika ya Mashariki

Bunge la Afrika Mashariki ni moja ya vyombo ambavyo, viliundwa ili kutoa uwakilishi wa wananchi katika maamuzi makubwa ya jumuiya na Bunge hili linaundwa na wabunge 45, tisa kutoka kila nchini.

Miaka 10 ya jumuiya hii, wabunge hawa wamekuwa na mawazo tofauti, wapo ambao wanaoamini kwamba malengo ya jumuiya hiyo katika kipindi hiki yamefikiwa huku wengine wakisema maazimio mengi yanakwenda taratibu sana.

Dk Fortunatus Masha ni mmoja wa wabunge kutoka Tanzania, amekuwa akisema kuwa malengo ya jumuiya hii katika miaka 10 yamefikiwa.

Kuwepo kwa jumuiya hii kumesababisha nchi wanachama, kuaminiana na kumimarisha mahusiano hadi kuweza kuongeza nchi mbili za Rwanda na Burundi katika jumuiya hii.

Moja ya malengo ambayo leo tunaona kuwa yamefanikiwa kwa kipindi cha miaka 10 kuwezesha kuwa ushuru wa forodha unaofanana

Kupitia mkataba wa nyongoza wa Soko la pamoja inawezekana kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zitakazozalisha katika nchi moja kwenda kuuzwa katika nchi nyingine.

Jambo hili litakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kama litatekelezwa kwa unagalifu mkubwa bila kuziumiza nchi masikini kiviwanda. Kuwepo na usawa katika uingizaji wa bidhaa, Jumuiya inagalie uwezekano wa kuziwezesha nchi sizizona viwanda kuwa navyo.

Kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta ya uzalishaji ni muhimu sasa kwa nchi kama Tanzania.

Katika kipindi cha miaka 10 vimeundwa vyombo mbalimbali vya kusaidia maendeleo kwa nchi wanachama ambavyo ni pamoja na Benki ya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Ziwa Viktoria na Taasisi ya Muungano wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki .

Haya ni mambo ya kujivunia, kujivunia hadi kufika Shirikisho la kisiasa. hakuna haja ya kuwa na hofu kwa wafanyabiashara kutokana na tofauti za uchumi kwani bidhaa za Kenya zilikuwa zinatozwa ushuru kwa miaka mitano na sasa muda umekwisha, sasa wanaweza kushindana katika masoko na bidhaa za nchi nyingine bila tatizo.

Changamoto iliyopo


Changamoto kubwa ilinayonekana kuikwamisha Jumuiya ni kuhusu utekelezaji wa yale yanayokubaliwa, kwani kiutaratibu ni kwamba bnaada ya kusaini mktaba wa nyongeza(Protocol), inasubiri kwa mabunge ya kila nchi kuridhia na kupitisha kama azimio.

Pia Bado hakuna sera zilizopitishwa za Ardhi, Uwekezaji, Usafirishaji na masuala ya Rasilimali watu mambo ambayo yamekuwa yakikwamisha kazi za jumuiya.

Iwapo Baraza la Mawaziri na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, watahakikisha sera zote zinakamilika kwa wakati na kujenga mfumo mzuri wa masuala ya fedha na mali za jumuiya, mambo mengi yatafanikiwa.

Ujenzi wa barabara ya lami ya kisasa kutoka Arusha- Namanga hadi Athi River ni moja ya miradi mikubwa ya kujivunia kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia upo mradi wa kuimarisha miradi ya barabara kuu za Mombasa- Katuna -Dar es Salaam hadi Mtukula nchini Uganda, uimarishwaji wa usafiri wa Reli ambapo tayari nchi wanachama zimetenga jumla ya dola 350,000 kwa mradi huo.

Hadi sasa katika Jumuiya hii kuna miradi kadhaa inatekelezwa ambayo ni pamoja na utunzwaji ziwa Victoria, mradi wa kilimo na uhifadhi wa chakula katika nchi wanachama,mradi wa uimarishaji nguvu za umeme katika nchi wanachamana na mradi wa ukuzwaji utalii.
Hata hivyo, pamoja na kusainiwa kwa makubaliano hayo na wakuu wan chi, masuala hayo yataanza kuanza kutumika rasmi Julai mwakani baada ya kila nchi, kuidhinisha katika utaratibu ambao zimejiwekea.

Hii ndiyo changamoto inayotukumba ambapo kila nchi inasheria zake na inataka masuala yote yafanyike kwa mujibu wa sheria za nchi husika na sii za Jumuiya.

Waziri wa masuala ya EAC Dk. Deodarus Kamala, alifafanua kuwa katika itifaki hiyo ya soko la pamoja, kuna suala la uhamiaji ambalo hati za kusafiria zitazingatia maamuzi ya kila nchi na nchi zimepewa uhuru wa kuamua kuondoa au la.

Kwa upande wa suala nyeti la ardhi ambalo limekuwa likizua mjadala mzito, anasema litabaki kufuata sheria za kila nchi na kama kuna mtu anataka kuishi na kumiliki ardhi katika nchi nyingine, taratibu zilizopo katika nchi husika zitafuatwa.

Watanzania wana matumaini makubwa juu ya mafanikio yajayo ya jumuiya hii na hasa katika utekelezaji wa makubaliano yaliyokwisha kufanyika na yale yaliyoainishwa katika katiba ya EAC lakini yamebaki kuridhiwa.
0784/ 715 686575
www.deotemba.blogspot.com

Mwisho

No comments:

Post a Comment