Popular Posts

Thursday, November 19, 2009

Lembeli: Ubunge wangu hauna mkataba na mafisadi

*Hana mpango wa kutoka CCM hata kama ataundiwa zengwe
*Ni Mbunge wa masikini siyo wa matajiri

MBUNGE wa Jimbo la Kahama Mkoani Shinyanga(CCM), James Daudi Lembeli, ni mmoja wa Wabunge waliojipambanua hivi karibuni kuwa wapiganaji wa vita dhidi ya ufisadi nchini.

Lembeli, ambaye kwa sasa ni mwnaharakati na kamanda wa vita hivyo, amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na makundi ya wanasiasa wenzake hasa wabunge na Mawaziri na viongozi wengine ndani ya CCM, ambao wanafanya mbinu za kutetea ufisadi au kufadhili makundi ya vijana ili wawachafue kisiasa wale wasio unga mkono ufisadi.

Katika suala la Ufisadi, Lembeli, ameapa kuhakikisha anapambana na kundi hilo ikiwezekana aukose Ubunge lakini ahakikishe anasimamia penye ukweli.

Kwa ya uchumi na maendeleo ya watu wa Shinyanga, Lembeli anasema kuwa Mkoa wa Shinyanga umezidi kuwa masikini kutokana na watu wachache ambao wanataka kufaidi rasimali za mkoa huo peke yao na kuwaibia wananchi.

Anasema kama Mkoa huo wenye migodi mitatu iliyo hai inayochimbwa hadi leo, hautapata wabunge na madiwani safi wasio wezi, wala rushwa, mafisadi, wananchi wake wataendelea kutaabika na kuwa masikini.

“Shinyanga siyo masikini kama tunavyosikia, umasikini umeletwa na watu wachache wasi na huruma ambao wameiba kwa miaka mingi, bila huruma na hata sasa watataka kuendelea kula. wanataka wananchi waendelee kuwa kimya ili waibe zaidi, sasa ni mwisho wao, mimi na Mpendazoe(Fred) wa Kishapu, hatutaacha hadi kieleweke,” anasema Lembeli.


Katika malalamiko ya wananchi wa Kahama juu ya migodi ya kampuni ya Barrick, Lembeli anasema kinachotakiwa ni kampuni hiyo kuelewa kuwa imewakuta wananchi pale na iheshimu makubaliano wanayofanya. na kusiwe na kuoeneana wala kupunjana kwani wananchi ndiyo wenye ardhi na siku ya mwisho watabaki na nchi yao.

Lembeli anasema kuwa amejikuta akipingwa na watu wengi kutokana na msimamo wake usioyumba wa kutetea maendeleo na masilahi ya wananchi wa jimbo lake ambao kwa muda mrefu walikosa mtu wa kuzungumzia matatizo yao kwa uwazi hasa ndani ya bunge.

Kinachomsukuma ni kwamba kwa muda mrefu watu wa Kahama hawakuwahi kuwa na Mbunge anayeangalia maslahi yao na kuwapigania.

Tangu Lembeli, aingie madarakani Mwaka 2005, amesimama kidete kupiga vita rushwa iliyokuwa imeshamiri halmashauri ya wilaya ya Kahama, amesimamia ujenzi na ukarabati wa barabara hasa ya Kahama mjini ambayo kwa zaidi ya miaka 10 haya kukarabatiwa, amesimamia ujenzi wa soko jipya la Kahama mjini, amewatetea wananchi wa mgodi wa Buzwagi alipobaini wanadhulumiwa haki zao.

Pia anasema kuwa amejitahi kushirikiana na wasafadhili mbalimbali marafiki zake kama Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, na Wabunge wenzake na kupeleka mpango wa Benki ya Ushirika na kukopa vijijini (VICOBA), Kahama ambao ni mahususi kwa ajili ya wananchi masikini kujikwamua kutoka katika umasikini.

Katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari amejitahidi kuhakikisha kuwa wananchi wasio na uwezo hawalazimishwi kulipa fedha za michango ya ujenzi au kukamatwa na mgambo.

Pia amekuwa akiwasaidia watoto wenye wazazi wasiojiweza kuwalipia karo jambo ambalo hakuna kiongozi mwingine katika siku za karibuni amejitokeza kufanya mambo hayo hasa kwa Kahama. “Wengine hawa ni watu wa maneno tu na hawapendi kutokana na kutawaliwa na dhamira ya ubinafsi na ya kutetea masilahi yao” .

Anakiri kuwa ni kweli kuwa ndani ya Chama chake kuna makundi ya watu wachache wasiokubaliana na msimamo wake ila kwa sasa hawatamuweza kwani wananchi wa Kahama wa leo sio wale wa mwaka 1947 kwani wanafahamu kipi ni pumba na kipi ni mchele.

Kuhusu tuhuma ambazo zinajitokeza na kuzagaa nchini zilidai kwamba Lembeli pamoja wa wabunge kadhaa waliokwenda Kahama kumuunga mkono katika sherehe ya uzinduzi wa VICOBA wanajiandaa kuhama CCM na kwenda Chadema, yeye anapuuza na kusema yeye na hata wenzake hawana mpango huo na wote wanaozusha maneno hayo kwa lengo la kuwahadaa wana Kahama wanapoteza muda wao na kusisitiza atagombea tena mwaka 2010 kupitia chama chake cha CCM.

“Tayari nimekwisha wasilisha na kukabidhi ahadi zote zilizotolewa na Mengi ikiwa pamoja na sh. milioni 100 kwa VICOBA, Jimbo la Kahama,sh milioni 30 kwa sungusungu, sh.milioni 10 kwa walemavu wenye ugonjwa wa ngozi na sh milioni tano, kwa kwaya ya vijana wa Ibambala kata ya Ushetu”.

Anasema kuwa yeye amekuwa karibu na wananchi wake, amekuwa askiriki shughuli za maendeleo ya wananchi wake, na kusukuma maendeleo vijijini.

Kinacho mpa nguvu Lembeli hasa katika vita dhidi ya wapinzani wake kisiasa ni ukaribu wake na wananchi wa kipato cha chini hususani wanawake wajasiriamali ambao amekuwa msaada mkubwa kwao kwa kuwaanzishia mfumo wa kuweka na kukopa wa (VICOBA).
mwisho

No comments:

Post a Comment