Popular Posts

Saturday, November 21, 2009

CAG ajiandaa kukagua hesabu za vyama vya siasa

*vyama vyakwepa kumpelekea taarifa za hesbabu
Na Deogratius Temba

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Lodovick Utouh, amesema anasubiri kupokea taarifa za hesabu za vyama vya siasa ambavyo vinapata ruzuku kutoka serikalini ili aanze kuvikagua rasmi.

Utouh, alisema kwa mujibu wa sheria mpya ya vyama vya siasa, vyama vyote vinavyopata ruzuku kutoka serikalini ni yaani vile vyenye wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG inapewa mamlaka ya kugaua hesabu zake.

Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa habari juzi wakati wakitoa ripoti ya uhakiki wa madeni ya walimu, CAG alisema kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992, iliyofanyiwa mabadiliko Februari mwaka huu, ofisi yake imepewa nafasi hiyo.

“Ni kweli kuwa sheria hii mpya inanitaka mimi CAG kukagua hesabu za vyama vyote vya siasa vinavyopata ruzuku. Kisheria ‘mandate’ hiyo inaniruhusu hasa mimi mwenyewe na wasiadizi wangu, au niteue wataalamu wa ukaguzi kutoka mahali popote hata nje ya nchi, kuvikagua vyama hivi,” alisema Utouh

Alisema pamoja na kuwa sheria hiyo imeshapitishwa na inatumika sasa, zoezi hilo limechelewa kuanza kutokana na ofisi yake kutopokea taarifa za hesabu kutoka chama chochote kinachopata ruzuku.

“Zoezi halijaanza bado, hatujaletewa taarifa kutoka kwenye hivyo vyama, zikija tutaanza kazi mara moja sisi wenyewe au kumtafuta mtu atakayefanya kazi hiyo,”alisema Utouh.

Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992, iliyofanyiwa marekebisho mwaka huu, kinabainisha vyanzo vya mapato kwa vyama vya siasa kuwa ni pamoja na ada za wanachama, michango ya hiari, miradi ama hisa katika kampuni, ruzuku ya serikali na michango ama misaada kutoka vyanzo vingine lakini kwa sharti kwamba hesabu zake zinakuwa wazi.

Sehemu ya pili ya kifungu hicho inaelekeza vyama vya siasa kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu michango kutoka nje ya nchi na pia kutoka kwa watu ambao si raia wa Tanzania hata kama wanaishi ama wanafanya biashara halali nchini lakini pia vyama vya siasa vinalazimika kuwasilisha hesabu sahihi kila mwaka.

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amekikiri kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika eneo la fedha kwa vyama vyote vya siasa nchini, ingawa hataji chama chochote cha siasa kwa jina.

Katika kipindi cha bajeti ya miaka mitatu pekee 2005/2006 hadi mwaka 2008/2009, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 72, kama ruzuku kwa vyama vya siasa, fedha ambazo hazijakaguliwa na CAG bali wakaguzi wanaoteuliwa na vyama husika na baadaye kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mwaka 2005/2006 zilitolewa Shilingi bilioni 39, mwaka 2006/2007 Shilingi bilioni 15 na mwaka 2008/2009 zimetengwa Shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika dola.
mwisho

No comments:

Post a Comment