Popular Posts

Monday, October 26, 2009

Zain kusomesha wanafunzi wanane chuo kikuu

KAMPUNI ya simu za mikononi ya Zain, imechagua wanafunzi bora wanane itakaowasomesha katika elimu ya juu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano na Matukio, Tunu Kavishe, alisema wanafunzi hao waliochaguliwa kuingia katika vyuo vikuu vya Tanzania watapatiwa udhamini wa masomo kwa asilimia 100.
Kavishe aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Dickson Mutegeki, Invokavit Munisi, Tunu Mangara, Elizabeth Ngatunga, Naomi Elibariki, Frank Shega, Sophia Nahodha na Dominicus Kayombo.
Alisema washindi hao ambao walifanyiwa usaili wa kitaaluma na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na kuonekana kuwa ni miongoni mwa wanafunzi bora nchini wataungana na wenzao 31 kutoka vyuo mbalimbali amba wameshaorodheshwa kwenye mpango wa kusomeshwa na Zain.
“Idadi hii inafanya wanafunzi tunaowasomesha katika programu hii kufikia 39 hadi sasa,” alisema.
Kavishe alisema mradi huo unaofahamika kama ‘Tujenge Taifa Letu’, umekuwa ukiunga mkono sekta ya elimu ya juu na umekuwa ukitoa vitabu na nyenzo nyingine za elimu kama kompyuta katika shule mbalimbali nchini.
Alisema washindi huchaguliwa na TCU na baada ya wanafunzi wa sekondari kuomba na kufanyiwa udahili wakishinda hupatiwa karo, fedha za malazi na chakula kwa asilimia 100 wanapokuwa chuoni.
Pia wanafunzi hao hupatiwa ajira za muda mfupi wakati wa likizo katika ofisi za Zain, na wakati wa mazoezi ya vitendo hufanya wakati huo huo wakilipwa fedha za kujikimu.
Naye mwanafunzi aliyehitimu Chuo Kikuu cha Mzumbe, mwaka huu aliyefaidika na mpango huo, Noel Mazoya, alisema uzoefu wa kazi alioupata Zain umemsaidia kujifunza masuala ya masoko kwa kiasi kikubwa na tayari amepata ajira katika kampuni hiyo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment