Popular Posts

Monday, November 16, 2009

Serikali yatupia macho makazi ya Mzee Jumbe

Na Deogratius Temba

SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigamboni, Manispaa ya Temeke, Jijini Dar es salaam, yameondoka gizani baada ya Jenereta la dharura kupelekwa kwa ajili ya matumizi mara umeme unapokatika.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya gazeti hili kuripoti wiki kadhaa zilizopita kuwa makazi ya rais huyo mstaafu yamekuwa gizani wakati umeme unapokatika kutokana an mgao wa umeme uliokuwa ukilikumba taifa, bila kuwepo kwa jenereta la dharura na kupelekea familia yake kuwa gizani.

Akizungumza jana na Tanzania Daima, katika mahojiano maalumu ofisini kwake, Msemaji wa Wizara ya Ofisi ya Rais (Utumishi), Zamaradi Kawawa, alikiri ofisi hiyo kuhusika na kuwahudumia wastaafu kwa mujibu wa sheria na kuwa kutoa Jenereta ni juu ya ofisi hiyo.

“ Suala hilo la kuwepo kwa giza tulilifuatilia. Kuna sheria ambayo inatuongoza katika kuwahudumia wastaafu kama hao. Na wanastahili zao kisheria ambayo ni magari, matibabu, walinzi umeme, simu, watumishi wa ndani na magari mawili kwa kila kiongozi. Hayo yote tunawapatia,”alisema Kawawa.

Alisema sheria ya wastaafu wakada za kisisasa wanasimamiwa na sheria namba tatu ya mwaka 1999, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2005, ambayo inaelekeza Wiara hiyo kuwahudumia marais, makamu na mawaziri wakuu.

“Kutokana na hilo, tayari wanalo hilo jenereta na hakuna giza tena katika makazi ya rais huyo, lakini tatizo lile lilitokea kwa bahati mbaya hawakujua kama umeme ungekatika ndiyo maana mliliona tatizo hilo,’alisema

Mwezi uliopita wakati mgao wa umeme ukiendelea kuikumba nchi, Tanzania Daima, lilishuhudia makazi ya Rais huyo ambaye amekuwa akisumbuliwa na maradhi yakiwa gizani wakati yeye akiwa safarini nje ya nchi kupata matibabu.

Mzee Jumbe ambaye alijiuzulu urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 1984, amekuwa akiishi katika makazi yake ya kudumu yaliyoko Mjimwema, Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Tanzania Daima ilipofika katika makazi ya rais mstaafu huyo, lilishuhudia familia hiyo ikitumia taa za chemli kwa ajili ya shughuli za kawaida wakati wa usiku, huku walinzi nao wakiwa na taa na hizo pamoja na tochi.

Mzee Jumbe aliyezaliwa mwaka 1920, Visiwani Zanzibar, alikuwa Rais wa awamu ya pili wa SMZ, kuanzia mwaka 1972 hadi 1984 alipojiuzulu na nafasi yake kuchukuliwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Hata hivyo, Mwinyi mwaka 1985 ulipofanyika uchaguzi mkuu, aliteuliwa kuwania urais wa muungano na kushinda, na nafasi yake Zanzibar, ilichukuliwa na Idrissa Abdul Wakili aliyerithiwa na Dk. Salmin Amour na sasa Aman Abeid Karume.
mwisho

No comments:

Post a Comment