Popular Posts

Monday, October 26, 2009

Mahanga amdai Msemakweli bil. 3/-

IKIWA ni wiki moja tangu mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli, aanike orodha ya vigogo aliodai wameghushi sifa za kuwa na shahada ya uzamivu (PhD), Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Makongoro Mahanga, amemfungulia kesi mwanaharakati huyo na kumtaka amlipe fidia ya sh bilioni tatu kwa kumkashfu.
Dk. Mahanga ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Kennedy Fungamtama, alifungua kesi hiyo Mahakama Kuu jana na imepewa namba 145 ya mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya madai, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe, Muhibu Saidi, Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hilo na Kampuni ya The Guardian Limited.
Dk. Mahanga anadai Oktoba 18 mwaka huu, mdaiwa wa kwanza (Msemakweli) aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kumkashfu na gazeti la Nipashe likachapisha habari hiyo katika ukurasa wa mbele.
Alidai maneno yaliyoandikwa katika gazeti hilo kuwa ‘Dk. Mahanga ameghushi sifa za kuwa na shahahada ya uzamivu (daktari wa falsafa) wakati hajawahi kusoma shahada hiyo wakati wowote na mahali popote duniani’, ni ya uongo na yalikuwa na lengo la kupindisha ukweli.
Alidai maneno yaliyotumika yameonyesha mlalamikaji (Mahanga) alighushi vyeti, hivyo ni mtu asiyemwaminifu na ni mkosaji katika mazingira hayo na hastahili kuendelea kushikilia nafasi ya kisiasa katika ofisi ya umma na Bunge.
Dk. Mahanga aliendelea kudai kuwa Oktoba 19 mwaka huu, mdaiwa wa pili, wa tatu, na wa nne, walimkashfu kwa kuchapisha taarifa hiyo kwenye gazeti.
“Gazeti la Nipashe linachapishwa hapa jijini na kusambazwa hapa nchini na nchi za Afrika Masharikiki, hivyo naomba mahakama hii iliamuru gazeti hilo kuniomba radhi katika ukurasa wa mbele kwa uzito ule ule wa habari waliyoichapisha awali, izuie wadaiwa kuchapisha habari inayohusu mambo binafsi kuhusu mimi, biashara zangu na kazi zangu za kisiasa bila idhini yangu,” alidai Dk. Mahanga.
Wiki iliyopita Msemakweli aliitisha mkutano wake na waandishi wa habari na kudai kuwa amefanya utafiti na kubaini mawaziri sita walighushi vyeti vya taaluma.

Mwisho

No comments:

Post a Comment