Popular Posts

Saturday, September 26, 2009

Wananchi 300 wachomewa makazi yao Uyui Tabora

Na Deogratius Temba, Uyui Tabora

WANANCHI zaidi ya 300, wa kijiji cha cha Nzigala kitongoji cha Nseneki na Utumbili kata ya Nseneki, hawana mahali pa kuishi baada ya makazi yao kuchomwa moto na Jeshi la polisi kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Uyui.

Wananchi hao wanatakiwa kuondoka katika eneo hilo kwa madai kuwa wanaishi katika eneo la hifadhi ya Taifa, eneo ambalo wanaishi kwa zaidi ya miaka ishirini 20 wakiwa wameshiriki katika chaguzi za serikali za vijiji na vitongoji mara tatu toka mwaka 1994.

Kutokana na kuchomewa nyumba hizo, tangu Septemba 14, 2009, watoto wamesimama masomo katika shule ya msingi Nzigala yenye madarasa sita iliyopo katika eneo hili waliloamrishwa kuhama na kuharibiwa makazi yao.

Wananchi wa vitongoji hivi ambao ni wakulima wa zao la mahindi na ufugaji wa ng’ombe, wa jamii ya Kisukuma kutoka mkoa wa Shinyanga wameilalamikia Serikali ya awamu ya nne kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu walivyofanyiwa na kuwaharibia mali zao bila ya kufuata utaratibu wa kisheria.

Walisema mbali na Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kufika katika eneo hilo mwaka akiambatana na viongozi wa wilaya na mkoa, vitendo vya unyanyasaji vimeendelea na hakuna kiongozi anayejitokeza kuonyesha nia ya kulitatua.

Wakizungumzia suala la uhalali wa wao kuishi katika eneo hilo Makamu wa Rais, aliwaondoa hofu na kuwathibitishia kuwa ni eneo lao halali na waishi bila wasiwasi na kubainisha kuwa mpaka wa kijiji chao na hifadhi upo mashariki mwa kitongoji cha Nsekehi darajani.

Wakizungumza na Tanzania Daima, Jumapili, wananchi hao walihoji juu ya kauli mbiu ya serikali kuwa inajali maisha bora kwa watu wake wakati inawaharibia mali zao.

“Je huu ndio muendelezo wa utekelezaji wa Mkakati wa kuapambana na kukuza uchumi nchini( MKUKUTA)?,” alisema Rukenza Mapalamino, aliyechomewa nyumba yake na mifugo.

Katika mkutano wa Chama Cha Wananchi (CUF), unaofanyika mjini Uyui, Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa Taifa, Mbarala Maharagande, alilaani kitendo hicho na kusema kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizaji.

No comments:

Post a Comment