Popular Posts

Saturday, September 26, 2009

Ngeleja akiri IPTL kuizidi nguvu serikali

*Asema IPTL wanapiga chenga vikao
*Mpango wa kubadilisha mitambo wakwama
*Agizo la Rais Kikwete kwa Wizara la puuzwa

Na Deogratius Temba. Sept 2009

MPANGO wa kuibadilisha mitambo ya kampuni ya kuzalisha Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kutoka matumizi ya mafuta kutumia gesi asilia umeshindikana kutokana na serikali kushindwa kufikia muafaka na kampuni hiyo

Kukwama huko kumefikia mwaka mmoja sasa tangu Rais Jakaya Kikwete, alipotoa agizo kwa Waziri wa Nishati na Madini Wiliam Ngeleja, mwaka jana kuhakikisha mitambo hiyo inabadilishwa haraka bila kujali kesi iliyoko mahakamani.

Akizungumza na Tanzania daima katika mahojiano maalum, mwanzoni mwa wiki Ngeleja, alikiri kukwama kwa mpango huo, na kusema kuwa chanzo ni IPTL kutokutoa ushirikiano wa kutosha katika majadiliano yanayoendelea.

“Wao ndiyo Tatizo, walirudi nyuma katika mazungumzo ndiyo maana tumekwama. Ila hatujakata tamaa jambo hili tunalifatilia ili tuweze kutimiza lengo letu. Ni lazima walikubali,” alisema Ngeleja.

Alipoulizwa sababu za kushindwa kutekeleza agizo la Rais alilolitoa Oktoba mwkaa jana wakati akizindua mtambo wa kutengeneza megawati 100 za umeme kwa kutumia gesi asilia, Ubungo, alisema IPTL ni wagumu wa kuitikia wito wanapotakiwa kwenye vikao.

“Hao IPTL ndiyo wagumu. tunaendelea nao hata hivyo kuna mambo yameshafikiwa yanasubiri utekelezaji, kuna akzi inaendelea kufanyika,”aliongeza Waziri Ngeleja.

Rais Kikwete, alimtaka Waziri Ngeleja, asisubiri kesi ikliyoko mahakamani kwani kesi hiyo inaweeza kuchukua zaidi ya miaka 10 na nchi ikaendela kuingia hasara ya kulipia umeme kwa gharama kubwa.

“Ubishi wa kisheria unaweza kuchukua hata miaka 10, ugali wa bei za IPTL ni kutokana na matumizi ya mafuta, tumalize process hizi tusubiri mhakama,” alisema rais Kikwete, ambaye pia alisema hafurahii kasi ya mchakato huo wa kubadilisha mitambo.

Waziri Ngeleja alipoulizwa sababu za kuendelea kufanya majadiliano na IPTL, wakati Rais alitaka kuharakishwa kwa suala hilo bila kujali kesi iliyoko mahakamani, alisema hata hivyo suala hilo halijachelewa sana, kwani kuna hatua zimefikiwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, ambaye kamati yake ndiyo iliyowasilisha mapendekezo yaliyotoa azimio hilo, alisema “uamuzi wowote utakaofikiwa kuhusiana na IPTL unapaswa kuzingatia azimio la Bunge.”

Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) azimio ambalo linahusu IPTL lilitolewa Aprili 29, 2000 likiwa na maelezo ya kuitaka Serikali na wadau wengine wa suala hilo kuzingatia zaidi maslahi ya Taifa katika maamuzi yao.

“Suala la IPTL limalizwe kwa haraka nje ya Mahakama ili kuharakisha ubadilishaji wa mtambo huo ili utumie gesi na hivyo kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawati 100 ambao unatakiwa hivi sasa ambapo kuna nakisi kubwa ya umeme na hivyo kupelekea mgawo unaoumiza uchumi wa nchi,” inaeleza sehemu ya azimio hilo la Bunge na kuendelea;

“Katika kutekeleza hili la IPTL lazima izingatiwe kwamba IPTL iliitapeli nchi na Tanesco wamewalipa wamiliki zaidi ya kiasi cha fedha ambacho walipaswa kulipwa na Tanesco…..Serikali inatakiwa itumie ushahidi wote uliopo kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha kilichopo kwenye akaunti maalumu (Escrow account) ndicho kinatumika kumaliza madeni na kufanyia marekebisho mtambo huo ili utumie gesi bila kuhitajika kwa Serikali kutoa fedha nyingine….”

Suala la utapeli uliofanywa na IPTL liligusiwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusiana na kashfa ya umeme wa Richmond, akisema kwamba Tanesco wanaidai IPTL fedha walizolipa kwa makosa kama gharama za uzalishaji (Capacity Charge).

Mgogoro uliopo baina ya Tanesco na IPTL unatokana na kutokubaliana kwa pande zote mbili kuhusu kiwango cha gharama za uzalishaji kinachotozwa na IPTL.

Katika kauli za Waziri Mkuu Pinda alisema kwa mujibu wa mkataba wa kuuziana umeme kati ya IPTL na Tanesco, inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji kwa asilimia 30 na faida ya asilimia 22.31 uliopaswa kuwekezwa ambao ni dola za Kimarekani 36.54 milioni wakati IPTL ilipoanza kuzalisha umeme na kuanza kuiuzia Tanesco Januari 2002.

Alisema katika uchunguzi uliofanywa na Tanesco na asasi nyingine, imegundulika kwamba mtaji halisi wakati IPTL inaanza kuzalisha umeme ulikuwa Sh 50,000 tu, hivyo mtaji huo ndio unaostahili kutumika kukokotoa gharama za uzalishaji inayolipwa na IPTL na si vinginevyo.

Baada ya uchunguzi wa Tanesco iligundulika ya kuwa hadi Mei, 2008, TANESCO ilikwisha kuilipa IPTL jumla ya Sh. bilioni 221 tangu waanze kuzalishaji Januari, mwaka 2002.


Serikali ya Tanzania ilisitisha malipo kwa IPTL kwa maelezo kwamba kampuni hiyo imeshindwa kuwekeza kama inavyopaswa katika uzalishaji wa umeme na pia imedanganya gharama halisi za mradi jambo ambalo TANESCO inaamini kwamba kimahesabu kampuni hiyo ndio inayopaswa kuwalipa wao.

IPTL kuona hivyo iliamua kufungua kesi katika mahakama moja nchini Marekani ikidai kulipwa zaidi ya Shilingi bilioni 30/-, kesi ambayo imeelezwa bado inaendelea na hivyo TANESCO bado inaona si busara kulipa fedha hizo wakati majadiliano yanaendelea.

Hata hivyo, mmoja wa watu wenye hisa ndogo katika IPTL, mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Markerting Limited, James Rugemalira, amepinga uamuzi huo wa wanahisa wenzake.

Wanahisa wengine wa IPTL ni pamoja na Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad, ya Malaysian ambayo ndio wenye hisa kubwa za asilimia 70 wakati VIP wanashikilia asilimia 30 pekee, na sasa wana kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusiana na mgogoro baina yao, kesi ambayo Rugemalira anasema ni lazima imalizike kabla ya wanahisa kufungua kesi nyingine.

Novemba 15, 2007, IPTL ilifungua kesi katika mahakama moja ya New York, Marekani wakidai kulipwa Dola za Marekani 27,169,882.67 (Karibu Sh bilioni 30/-) kwa madai kwamba TANESCO imekiuka mkataba baina yao uliosainiwa 1995.
mwisho

No comments:

Post a Comment