Popular Posts

Tuesday, September 15, 2009

Tusipodhibiti moto shuleni tutashuka kielimu

MWISHONI mwa wiki iliyopita taifa liliingia katika majonzi na simanzi, baada ya wanafunzi 12 wa shule ya sekondari Idodi ya mkoani Iringa, kuungua moto na kupelekea nakupoteza maisha.

Awali ya yote nachukua nafasi hii kutoa pole kwa wazazi, walezi na ndugu walio wapoteza watoto wao katika ajali hiyo.

Pia pole za dhati ziwaendee pia wanafunzi wote wa shule ya Idodi, kwa kuwapoteza wenzao, na pia kwao wenyewe kwa kuumia na kupata majereha mbalimbali katika miili yao, ni ukweli kuwa wameumia. Pia wamepoteza vifaa vyao vya kusomea, ambavyo inaweza kuwasababishia madhara ya kisaikolojia.

Ni kipindi ambacho haikiwezi kusahaulika na tena kinaweka historia ngumu katika maisha ya watu hasa kwa wanafunzi na wazazi wao.

Hali kadhalika, tukio la kutokea moto katika mazingira ya shule au elimu yanaadhiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa elimu, katika mazingira husika na kwa taifa kwa ujumla.

Moto ni ishara ya hatari (kifo), unapotokea hata kama usipodhurika unaadhirika kisaikolojia, tukio la moto linafanana na kuvamiwa na majambazi, haliwezi kufutika akilini mwa mwadhirika kiurahisi, mbaya zaidi ni pale unapoona wanafunzi wameteketea kabisa na kubakia majivu.

Hali hiyo inazua hofu kubwa si tu kwa wanafunzi bali kwa wazazi, walezi na hata walimu wa shule husika, hivyo basi kuna kila haja kuchukua hatua kudhibiti matukio haya.

Hivi karibuni kumetokea matukio ya moto, ambayo haikufikia kiwango hiki, mwishoni mwa mwaka jana niliandika juu ya madhara ya moto katika mazingira ya shule kutokana ana na baadhi ya shule za wasichana kuungua moto.

Hata hivyo katika safu hii niliilaumu serikali kwa kutotaka kwa dhati kuchukua hatua kudhibiti matukio haya hatari kwa maisha ya binadamu na maendeleo ya elimu ncini.

Mwaka 1994, wanafunzi 40, walipoteza maisha na kuteketea kabisa katika bweni la shule ya sekondari Shauritanga, Rombo Mkoani Kilimanjaro.

Mwezi Agost 2003, ni kipindi ambacho binafsi siwezi kukisahau kwani nilikuwa kidato cha tano katika noja ya shule za misheni, katika kipindi hiki kuliibuka matukio ya kufuatana ya moto katika shule mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro.

Martukio haya, yalijenga picha tofauti katika vichwa vya watu na kufikia mahali watu kufikiri kuwa ilikuwa hujuma iliyolenga kupunguza idadi ya shule binafsi mkoani humo.

Mwezi huo Augost, 2003, iliungua Shule ya Sekondari Marangu, ambapo mabweni ya wasichana ya Manyara na Serengeti yaliteketea na kusababisha msichana mmoja wa kidato cha pili kuteketea wakati mamia waliweza kuokolewa na wavulana.

Wakati huo, shule za Machame, Useri, Shauritanga na nyingine zilitishiwa tena na matukio hayo. Tukio hilo lilisababisha serikali kuingilia kati na kuwataka wakuu wa shule kuimarisha ulinzi pamoja na kuwapatia silaha za moto kwa ajili ya kujilinda.


Haya ni matukio yaliyowajengea wanafunzi na wadau wote wa elimu, masikitiko makubwa miongoni mwa jamii hasa katika sekta ya elimu.Tukio hilo halikutumika kama darasa ili kudhibiti matukio mengine yasitokee.

Mwaka jana mabweni ya shule ya wasichana Mkalamo, Wilaya ya Korogwe, liliteketea pamoja na vifaa vyao, hili lilikuwa tukio la pili kutokea shuleni hapo.

Mabweni ya shule ya Sekondari ya masista ya Bingwa, inayomilikiwa na Umoja wa Jumuiya za mashirika ya Masista wa Kanisa katoliki nchini, Shule ya Sekondari Binti Musa iliyoko Kiwalani, Dar es salaam, Sekondari ya Mawenzi Moshi, Machame nayo iliungua mara mbili mfululizo.

Shule nyingine ni Kikatiti, ya Wilayani Arumeru, kwa shule za Machame na Lugoba utashaga kuwa zimeungua mara mbili mfululizo, lakini hakukuwa na udhibiti, wala hakuna taadhari iliyochukuliwa.

Kama tutataka kujenga elimu safi, kuweka misingi imara ya kuwawezesha wanafunzi kuelewa, ni lazima mazingira ya kusomea yawe salama, matukio hatari yatafanya kiwango cha elimu kushuka.

Kuharibika kwa miundombinu ya elimu, ni dhahiri kuwa inarudisha maendeleo ya elimu nyuma, matukio ya kutisha yanasababisha watu kuogopa kuwaweka watoto wao mashuleni.

Mwisho tunawaombea kwa dhati roho za wadogo zetu waliopoteza maisha ili Mwenyezi Mungu awapokee katika ufalme wake, hali kadhalika tunawaombea wanafunzi, walionusurika ili waimarike katika kipindi hiki kigumu katika msiba.

Pia katika kutafakari matukio haya wakati wanafunzi wakiwa na picha hiyo mbaya akilini mwao wanatakiwa kuelewa kuwa maisha ni mpando mkali, na safari ya kielemu unakumbana na mengi hasa unapokuwa nje ya mazingira ambayo umezaliwa.

Wanafunzi wanahitaji kulipokea suala hilo, kwa moyo mkunjuvu wavumilie na waendelee na masomo yao bila kukata tamaa. Wakijua kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha yao.

Hilo walijifunze, walione na waliishi ili kujiimarisha kimaisha katika kupamabana na changamoto za maisha licha ya kuwa ni vigumu kulipokea.

No comments:

Post a Comment