Popular Posts

Tuesday, September 15, 2009

KUFUATIA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA(1)

Watanzania tujiandae kuchagua viongozi bora, safi na waadilifu

KATIKA safu tangu ilipoanza Oktoba mwaka jana, nimekuwa nikiandika mambo mengi ambayo yamekuwa yakilenga mstakabali wa taifa hili kisiasa, kiuchumi na hata kijamii, maana tumekuwa tukijadili hata masuala ya kiroho na kimaadili.

Kwa namna yoyote ile huwezi kumzungumzia binadamu bila kugusa mwili na roho yake. Kwahiyo kujadili suala la kiroho katika ulimwengu huu wa leo siyo udini kama baadhi ya watu wanavyoweza kufikiri.

Mada nyingi zilihusu siasa, uchumi na maadili yetu sisi kama watanzania na binadamu tunaoishi katika dunia ambayo ina mamlaka tunapaswa kuzingatia sheria, haki , utawala bora na heshima kwa binadamu wote.

Nimeandika mengi ambayo yameifanya safu hii kujikusanyia wapenzi lukuki, ambao pia wamekuwa wakitoa maoni na michango mbalimbali ya kimawazo namna ya kuiboressha safu hii.

Maoni mengi ya wasomaji yalikuwa mwanzo wa kutoa tafakuri ya wiki inayofuata. Maoni na mchango wa kuboresha ilikuwa ni darasa kwa mwandishi na jamii nzima ambayo haikuweza kutoa maoni.

Leo kama nilivyoahidi, siku za nyuma, nilitaka kabla ya kuingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Ocktoba, tupeane somo, ambalo litakwenda mfululizo hadi uchaguzi utakapomalizika.

NI wazi kuwa Watanzania wapo katika kipindi kigumu kidogo tofauti na mataifa mengine na hata wakati mwingine ambapo Tanzania imekuwepo. Tunahitaji elimu, mwanga na mawazo mapya ambayo yatayuongoza kama wapiga kura katika kuwachagua vongozi wetu.

Jamii ya watanzania kama wanafamilia wanatakiwa kutambua kuwa serikali, kwa mujibu wa katiba yetu ya jamhuri ya Muugnao wa Tanzania toleo la mwaka 1977 na marekebisho yake yote 14, ni kuanzia ngazi yakijiji au mtaa.

Hatuna serikali kuu kama hakuna serikali ya mtaa, au kijiji, hatuna serikali safi kama huku chini kumechafuka. Hatuna uadilifu na amani kama tumeweka viongozi wa serikali za mitaa wanywa gongo, wavuta bangi, wahuni, majambazi, vibaka, au walarushwa.

Uadilifu ni suala la msingi sana, tunauhitaji katika ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa. Hali tuliyonayo leo ya watawala, mawaziri, wabunge na wakurugenzi wasio waadilifu ni matunda ya kuwa na uongozi mbovu kuanzia ngazi za chini kabisa yaani mitaani.

Nina imani kuwa safu hii inasomwa na watanzania ambao ndiyo wanaounda mitaa na vijiji na ndiyo wapiga kura katika ngazi hiyo, na pia ndiyo wanaopiga kura katika kuwachagua viongozi wakuu wa nchi kama Rais , wabunge na Madiwani.Kwa hiyo somo hili ni muhimu kwetu sote

Leo nitaanza na utangulizi tu, hebu tuangalie, serikali ya mtaa ni nini?, hii ni Halamsahauri ya kijiji au mtaa (Village Council) inayohusisha Mwenyekiti wa kijiji/mtaa au kitongoji pamoja na viongozi wengine wanaochanguliwa na mkutano MKuu wa kijiji.

Mkutano Mkuu wa kijiji ambao huwachagua viongozi, huundwa na wanawake na wanaume wote wakazi wa kijiji au mtaa husika wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Vijiji, au mitaa vinapata pia mapato na wana bajeti zao, kama ilivyo kwa serikali kuu, wanazo pia ruzuku kutoka serikali kuu kupitia Wilayani ambapo hugawanywa kulindana na mahitaji ya kijiji katika mipango yake ya maendeleo. Hili linahitaji kuwa na viongozi wadilifu na waaminifu tena ikiwezekana wacha Mungu.

Fedha kupitia mkakati wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini Tanzania(Mkukuta) zipo pia vijijini na hili linahitaji uadilifu mkubwa ili kila mwananchi hata asiye jua kusoma na kuandika ajue haki zake na apate mgawo wa fedha hizo.

Kutokana na kufanya makosa na kwachagua viongozi wasio waadilifu au waelewa katika mitaa na vijiji vyetu tumekuwa tukiendelea kuwa masikini kila siku, viongozi wasio na uwezo wa kuibua miradi ya maendeleo ni tatizo na ni chimbuko la kukua kwa umasikini nchini.

Fedha kama za Mfuko wa Jamii wa Maendeleo (Tasaf) zinatolewa katika kila kijiji, katika kuondoa umasikini kama tu, viongozi watakaa na kuibua miradi ya maendeleo, hasa ile inayolenga kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini.lakini tusipowachagua viongozi wazuri tunazikosa fedha hizo.

Pengine tunaweza kuwa na viongozi weleji au wajuaji kutafuta fedha wakatutafutia fedha hizo lakini zikawa zinaishia katika mifuko yao na kushibisha matumbo yao. Viongozi wa mitaa wasio waaminifu wanakula na wakurugenzi wa halamsahauri na makatibu tarafa ambao ndiyo watendaji na kuamua kutafuna fedha za wananchi.

Tukiwa na uongozi imara uanochukia ufisadi, wasio wala rushwa na waadilifu, wanaanzisha vita kila mara na wakurugezni wa halmashauri wasio waaminifu.


Tumepiga vita ufisadi katika ngazi ya ubunge na serikali kuu, lakini jukumu kubwa kabisa la kuhakikisha nchi inakuwa safi na ya watu wadilifu wasio wamezaji wa haki za watu, binadamu wote w3awe sawa na wapata haki zao bila kubaguliwa kimatabaka. Ni lazima tuandae mazingira safi huku chini.

Viongozi hawa wa Mitaa, ndiyo wanaounda mikutano mkuu ya vyama kama wajumbe pia ambao wanahusika katika uteuzi wa wagombea wa udiwani na ubunge, kama tutakuwana viongozi wachafu wasio waaminifu tutapata hasara kwani wabunge wengi watakuwa wa jinsi hiyo.

Kama kweli watanzania wenzangu tumedhamiria kwa dhati kusafisha taifa hili, na kulifanya liwe mahali salama pa kuishi, na kila mmoja apende, basi uchaguzi huu wa serikali za mitaa tujitokeze kwa wingi na kushiriki katika michakato yote ya kuwaandaa wagombea na kupiga kura.na hii itazuia mafisadi kuchaguana wenyewe au kupandikiza mawakala wao

Kama chama kinaandaa watu wake kwa kugawa rushwa tujue kuwa kinatundalia mkaa wa kutukaanga wenyewe. Niliwahi kuandika mara kadhaa kuwa kama utawala wa Chama cha Mapinduzi(CCM), au chama kingine chochote umetuchosha hapa ndipo mahali pake kuondoka.

Tuonyeshe katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa kuwa uongozi wa aina hii hatakiwi na siyo endelevu katika Tanzania hii ya leo. Kama CCM wanalalamikiwa kuwa ni mafisadi basi katika uchaguzi wa serikali za mitaa tuwaambie basi.

Kama Mbunge au waziri analalamkikiwa kuwa ni fisadi, na tunaona anakambi yake kijijini /mtaani hapo, basi hatakiwi na kambi yake haifai inatakiwa kupigwa chini ili wajirekebishe.

Uchaguzi huu wa serikali za mitaa ni mwanzo na ni njia ya kuingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Tujipange na wala tusiudharau wale tunaowaona wanachukia ufisadi tuwape sasa ili baadaye tupate madiwani safi na wabunge safi na hata rais safi.

Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa wao ndiyo wenye nchi, taifa ni lao, wao ndiyo waajiri wa kila mwanasiasa, na kama wasipolitambua hilo wataendelea kuteseka kutokana na mateso wanayosababishiwa na watu wengine.

Hili ni somo, ambalo limenza leo, na tutaendelea nalo hadi uchaguzi utapofanyika, nimeamua kufanya kazi hii, kama mwanaharakati kutokana na hali ilivyo watanznaioa tuungane pamoja kukomesha ufisadi. Vita ni yetu wote tukliamua tutashinda. Tuelemishane ili vita ambayo tumekuwa tuliipigana kila mara ya kufukuza mafisdi ifanikiwe.

Azimio la Arusha lilianza hivi hivi, kufukuza wahujumu uchumi ilikuwa kazi nzito lakini ilipoungwa mkono na watanzania wengine Marehemu Edward Sokoine aliishinda.

Daima tutasimamia ukweli na uwazi pale ambapo tunaona kuwa watu wanaibiwa, na hasa pale tunapotambua kuwa watu hawajaelewa vizuri ni jukumu letu sote kuwaaambia watu upi ni mchele na upi ni mpunga.

Ninawatakiwa watanznia wenzxangu maandalizi mema ya uchaguzi wa seriklai za mtaa mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment