Popular Posts

Monday, July 27, 2009

WAISLAMU

Kwa heri OIC, mahakama ya kadhi, tuonane 2015

KATIKA hoja zilizoitikiza serikali ya Chama cha Mapinduzi(CCM), katika kipindi hiki hasa awamu ya nne ni suala la Mahakama ya Kadhi na nchi kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu(OIC).

Hoja hizi ziliibuka na kuleta mjadala mkubwa na pengine kupelekea kutaka kusababisha chuki na uhasama miongoni mwa wananchi kutokana na seikali kutaka kuliingiza katika katiba ya nchi.

Suala hili lilitaka kuingia katika katiba kutokana na kuwepo katika ilani ya uchaguzi ya CCM, ya mwaka 2005, ambapo chama kilishidwa kutekeleza ahadi hiyo kiliyokuwa kimeiahidi kwa nguvu zote wakati wa kampeni.

Bila shaka mhakama ya kadhi, na OIC viliingizwa kwa lengo la kuwarubuni waislamu, ili wakipe chama kura,kwa sababu ni vigumu kuwapata waislamu kati vilabu vya pombe za kienyeji na baa na kuwapa rushwa ya pombe.

Ulevi na rushwa ya waislamu ili waichague CCM ilikuwa ni Kadhi na OIC, Waislamu wakalewa wakakubali kutoa kura, sasa ahadi imeshindikana kutimizwa.

Itakumbukwa kuwa kazi kubwa kwa CCM ilikuwa kuingia madarakani hasa katika nafasi ya urais, chama kiliamini kuwa kama kitampata rais kiulaini basi kazi imakwisha, ujanja uliotumika ni kuwalewesha mvinyo wa Mahakama ya Kadhi na OIC, sambasamba na wasio waislamu kupewa vizawadi kutokana na umasikini wao ambao wamekirimiwa wakakubali kuuza haki zao za kura kwa watu wasio stahili nafasi hizo.

Suala la takrima, lilikuwa ni vyakula, vinywaji, fedha za zawadi za nguo na vitu vingine.

Kwa sasa suala la waislamu kupatiwa Kadhi ni kama limemalizika, hata kama waislamu watakuwa wananung’unika kimoyo moyo, lakini litabaki kuwauma, bila kutegemea masaada tena.

Kitendo cha serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutamka wazi kuwa serikali haina tatizo na uanzishwaji wa mahakama hiyo iwapo mfumo wake haitaihusisha, ni dalili tosha kuwa imejitoa.

Kujitoa kwa serikali kunakuja wakati wananchi wakiwa wamefikia hatua ya kurushiana maneno na wabunge kugawanyika kwa itikadi za kidini, kutokana na baadhi ya watu kupendekeza suala hilo lifanywe kwa mfumo huo na kuonekana kama wanawanyanyasa waislamu.

Hoja ya tangu awali kutoka kila upande ukiacha wahitaji (Waislamu) ilikuwa ni suala hilo, liundwe bila kuingiliaana na dola.

Waziri Mkuu Pinda, amesema kuwa rais Jakaya Kikwete, alimweleza kuwa serikali haina tatizo kuhusu uanzishwaji wa Mahakama hiyo, ili mradi isiendeshwe na serikali ili kuepuka kuwepo kwa mgongano wa kidola, hapo amemaliza kazi.

Ina maana basi watanzania wamepoteza muda, nguvu, akili, na hata fedha katika kulipigania suala hilo, jibu la waziri Mkuu Pinda, na rais Kikwete, lilitosha kutoka tangu mwaka juzi wakati hoja hizo zilipoanza kutikiza Bungeni na nje ya Bunge.

Kwa hali hiyo basi, serikali imewataka Masheikh, kupanga namna ya kuanzisha mahakama hiyo, kitu ambacho wao wenyewe walikipinga, na walikataa awali, na kama wamekubali ina maana wamepoteza muda.

Kuna haja ya kuihoji serikali, kama kulikuwa na uwezekano wa kuwaeleza waislamu mapema msimamo wake.

Nafikiri hata kauli za rais zimekuja kwa kujikaza ‘kiume’
Kwani tangu awali wakati mijadala ikiwa moto, ilionekana wazi kuwa hawakuwa tayari kutamka bayana kuwa haiitaki Mahakama hiyo, lakini suala likawa ni kuogopa mgogoro baina ya serikali na Waislamu.

Lakini likabakia kutengeneza chuki miongoni mwa waislamu ambazo zilipandwa na baadhi ya watu kuwa wakristo ndiyo wanachochcea kucheleweshwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Kwa kauli hiyo ya wazi kutokana serikalini, ambayo tunaisema imechelewa, na kuchclewa kwake kumewapotezea muda Watanzania, rais amejitahidi kuitamka, ni kauli ngumu na nzito hasa kipindi hiki ambacho nchi inaingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwisho wa mwaka huu na ule mkuu wa mwaka 2010.

Kwa mantiki hiyo basi suala OIC na Mahakama ya kadhi, halipo tena katika ilani ya uchaguzi, limefutwa rasmi, kwani utekelezaji wake utafanyika ndani ya utaratibu mwingine.

Kwa upande wa OIC, serikali nayo imejitutumua na kujikaza kutamka kuwa Tanzania haiwezi kujiunga wakati bado nchi wanachama wanakaa kubadili katiba na muundo wa Taasisi hiyo, kwa hiyo wanachama wapya kama Tanzania hawawezi kujiunga nayo kwa sasa.
Mchakato huo wa ndani ya OIC wenyewe kutengeneza muundo wake upya unatakiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka 2012.

Muda huo utafikia kipindi ambacho tayari Tanzania itakuwa imemaliza uchaguzi Mkuu viongozi wa nchi watakuwa wengine.

Hapo ugumu au wazo la CCM kutokukubalika na waislamu litaamauliwa na wao wenyewe kama wameridhika na majibu hususani hitimisho la madai yao haya mawili.

Hili la OIC kwa sasa linaonekana ni la kiufundi zaidi na linahitaji mawasiliano ya nje ya yaani ya kimataifa, mpaka pale OIC watakapo tuambia kuwa wamemaliza kuubadili muundo wao na kutengeneza katiba mpya.

Bila shaka masuala haya yataibuka tena katika ilani ya CCM, au ahadi za kampeni mwaka 2015, wakati ambapo serikali ya awamu ya nne itakuwa imemaliza muda wake.

Tujue kuwa mwaka 2015, ni kipindi ambacho nafasi ya urais inakuwa ngumu na changamoto zake ni kubwa, masuala kama ya OIC na Kadhi yanaweza kujitokeza kwa urahisi ili kuwafanya baadhi ya watu au vyama vipate ridhaa ya waislamu kurudi madarakani.

No comments:

Post a Comment