Popular Posts

Friday, September 9, 2011

Watanzania vijana masikini tuungane kudai haki ya ajira

Na Deogratius Temba
TAFAKURI ya wiki iliyopita iliangalia suala la ajira kwa vijana wa kike na kiume. Kundi la vijana ambalo ndilo nguvu kazi ya taifa linateseka kutokana na kukosekana kwa fursa za ajira. Kundi la vijana linakimbia kutoka vijijini kuja mijini kutafuta ajira kwa sababu mazingira ya kijijini hayaruhusu kujiajiri wala kuajiriwa.
Hali ilivyo kijijini, hapa mjini ni mbaya zaidi. Ajira kwa vijana wasio na elimu inazidi kuwa mbaya, waliojiajiri wanateseka nao, waliosoma wamehitimu lakini hawajui waelekee wapi mategemeo yao ni sifuri. Ajira sizizo rasmi ndio zinaongeza takwimu za serikali kuwa kuna ajira milioni na zaidi nchini, lakini tunajiuliza huyo aliyejiajiri tunamwezesha kwa kiasi gani?
Katika mjadala wangu juu ya tatizo la ajira na hali ilivyo kwa vijana wa taifa hili katikan safu hii, wiki iliyopita nilieleza juu ya jumuiko kubwa au kusanyiko la wanaharakati wa masuala ya usawa wa Jinsia, haki za binadamu, maendeleo na demokrasia (FemAct), kuanzia tarehe 13 hadi 16, septemba mwaka huu katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Mabibo Dar es salaam. Kwa bahati mbaya sikueleza Tamasha linafanyika wapi na lini, wasomaji wengi wamenipigia simu kuuliza hilo.
Tamasha litatupa nafasi sisi vijana wa kike na kiume, kina baba na Kina mama hasa tulioko pembezoni kudai haki yetu ya kuwa na ajira stamilifu na kutaka serikali itekeleza wajibu wake kwetu. Ni fursa ambayo tutaweza kukutana na kubadilisha mawazo, kujegeana uwezo, kujadiliana na hata kupaaza sauti zetu. Vijana wasio na ajira, wasomi na wasio wasomi wanaweza kukutana kwa urahisi na bila kuwa na itikadi za kichama, kidini au kijamii. Tatizo la ajira na maisha endelevu ni msiba wetu sote katika taifa hili, tusipodai leo na kujenga mazingira mazuri vizazi vijavyo vitatulaumu.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kazi na ajira, nafasi za ajira zimeongezeka, katika sekta isiyo rasimu lakini hawataji ni ajira zipi, za kuokota makopo, kufagia barabarani, kuokota vyuma chakavu, au ni zipi. Takwimu zao zinasema kuwa sehemu kubwa zaidi ya watu wenye umri wa kufanya kazi (miaka 10 na kuendelea) inashiriki katika kazi za kiuchumi kuliko ilivyokuwa miaka kumi iliyopita. Huenda hii imetokana zaidi na kuongeza kwa mara ya kwanza shughuli za kuchota maji na kukusanya kuni kwa matumizi ya kawaida kuwa ni kazi za kiuchumi hasa hapa mjini na vijijini.
Usawa wa kijinsia kwenye ajira
Tofauti kati ya kiwango cha ushiriki wa wanawake na ushiriki wa wanaume katika kazi za kiuchumi imeongezeka. Kiwango cha ushiriki wa wanaume cha asilimia 81 ni alama 8 juu zaidi kikilinganishwa na kiwango cha wanawake, ikilinganishwa na tofauti ya alama 1 tu mwaka 1990/91 wakati kiwango cha ushiriki wa wanaume kilikuwa asilimia 73 wakati huo. Kwa hali ya kawaida taifa ambalo halina usawa wa kijinsia katika shughuli zake ni taifa linaloelekea kubaya. Hali hii inazaa matabaka na unyanyasaji kuongezeka.
Aina ya ajira.
Kuna aina nne za ajira ambazo ni; ajira ya malipo, waajiri pamoja na ajira binafsi (acha kilimo), ajira binafsi katika kilimo na wafanyakazi wa kifamilia wasiolipwa, yanaonyesha kupungua kwa ajira ya malipo na pia ajira binafsi katika kilimo. Kwa mujibu wa ripoti ya kazi na ajira ya shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO) kwa Tanzania, Ajira ya malipo imepungua kwa asilimia 3 na ajira binafsi katika kilimo kwa asilimia 5. Mwaka 1990/91 mchango wa ajira ya malipo ulikuwa asilimia 9.0 na ajira binafsi katika kilimo asilimia 84. Kwa upande mwingine ajira binafsi (ambayo si kilimo) katika Sekta Isiyo Rasmi na ajira ya kifamilia isiyo ya malipo zimeongezeka. Tuelewe kuwa ajira za kifamilia zisizo na malipo ni zile za kuwatunza wagonjwa, wazee, watoto na kazi nyingine za familia, ambazo hatuzichukulii kama kazi wakati wanaozifanya wanauwezo wa kufanya ajira za malipo.
Ajira ya kisekta.
Ajira katika Sekta ya Umma inazidi kusinyaa kwa nusu ya kiwango chake miaka kumi iliyopita. Mchango wa ajira Serikalini umeshuka kutoka asilimia 3 hadi 2, pia mchango wa ajira katika Mashirika ya Umma umeshuka kutoka asilimia 2 hadi 0.5. Mchango wa ajira ya Sekta ya Kilimo vile vile umedondoka kutoka asilimia 84 hadi 70 kwa kipindi cha miaka 20. Mabadiliko haya yanaonyesha kuwa vianzio vikuu vya ukuaji wa ajira vinaanza kubadilika na kuhamia kwenye Sekta Binafsi (acha kilimo), rasmi na isiyo rasmi. Mchango wa sekta hizi umeongezeka kutoka asilimia 2.8 hadi 6.5 kwa Sekta rasmi na asimia 8.5 hadi 10.8 kwa sekta isiyo rasmi.
Ajira katika Sekta Isiyo Rasmi.
Ajira katika sekta isiyo rasmi imeendelea kukua katika kipindi chote. Matokeo yanaonyesha kuwa kaya mbili katika kila kaya tatu zinajishughulisha na kazi kwenye sekta hii, ikilinganishwa na kaya moja katika kila kaya nne mwaka 1990/91. Idadi ya kaya zinazojishughulisha na kazi kwenye sekta isiyo rasmi imeongezeka kwa maeneo yote, vijijini na mijini, ingawa kasi imekuwa kubwa zaidi kwa maeneo ya mijini. Karibu asilimia 65 ya kaya za mijini na zaidi ya robo ya kaya za vijijini zinajishughulisha katika sekta hii ikilinganishwa na viwango vya asilimia 42 na 21 kwa mtiririko huo, mwaka 1990/91.
Katika uchambuzi huu, nimetumia takwimu za kulinganisha hali tulionayo leo tangu mwaka 1990 wakati tulipoanzisha mfumo wa soko huria. Ni miaka 20 Tanzania imekuwa katika mfumo huu, hali ya kipato na ajira kwa masikini inaongezeka. Tutakutraka kwenye tamasha la Jinsia mambibo na kujadili kwa kina suala hili. Itaendelea wiki ijayo ambapo tutaangalia kiwango cha ukosefu wa ajira kwa Tanzania. Jumapili njema!!

No comments:

Post a Comment