Popular Posts

Wednesday, May 26, 2010

Migodi ya madini kurudishwa kwa wazawa

Na Deogratius Temba
Serikali imesema nia ya kutengeneza sheria mpya ya madini ya mwaka 2010, ambayo inasubiri kutiwa saini na rais muda wowote kuanzia sasa ni kutaka baadaye migodi yote ya madini irudi mikononi mwa Watanzania.

Kamishna wa madini nchini, Dk. Peter Kafumu, amesema hatua ya kuandaa sheria hiyo inayo onyesha kuwajali wawekezaji wa ndani kuliko wa nje ni kuhakikisha baadaye Watanzania wenye mitaji ya kifedha wanawekeza zaidi katika sekta hiyo.

“Mtazamo wa serikali kwa sasa ni migodi hii baadaye kabisa irudi mikononi kwetu, wale Watanzania wenye fedha waichukue. Watanzania wamekuwa wakishindwa kutokana na uhaba wa teknolojia na mitaji tunataka tuliangalie hilo,”amesema.

Akizungumzia sera mpya ya madini ya mwaka 2009 iliyopelekea kutengenzwa kwa sheria mpya amesema “Tunajaribu sana kuimarisha sekta hii, kitu kikubwa kwenye sera mpya ni kuunganisha uchumi wa madini na sekta nyingine nchini”.


Kuhusu faida ya moja kwa moja kwa Mtanzania inayotoka kwenye madini Dk. Kafumu, anasema kimtazamo Mtanzania wa kawaida haoni faida ya madini, lakini ukweli ni kwamba ipo na tena ni kubwa.

“Sera hii inaweka wazi namna ya kuwaelendeleza wachimbaji wadogo kuliko wakubwa, utekelezaji wa sera unawapa mikopo hawa watu. Kama mtu mmoja mmoja Watanzania wenye uwezo wamejitokeza kuwekeza katika madini, wanafanya utafiti na tunawatia moyo Watanzania wengi zaidi kujitokeza kuwekeza katika sekta hii,” amesema.

Amefafanua kuwa suala la uwekezaji wa madini ni gumu kidogo ndiyo maana Watanzania wengi hawapendi kuwekeza kwenye sekta hiyo kwani unawekeza fedha lakini hujui kama utapata lini madini.

Sheria ya madini ya 1998, na kanuni za madini za 1999, ambayo ilitengenezewa sera mwaka 2009 ndizo chimbuko la kuzaliwa kwa sheria hiyo mpya ya mwaka 2010.

Akielezea tofauti ya sheria ya mwaka 1998 na hii mpya anasema sheria mpya imezingatia kuongeza uhamasishaji wa uwekezaji katika madini kutoka nje kama ilivyokuwa ikifanyika katika sheria iliyopita.

Pia kuongeza zaidi fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine za uzalishaji, ikimaanisha wamiliki wa migodi waweze kununua zaidi huduma zao katika maduka ya ndani, mchele, nyama na umeme.

“Suala la kuongeza funganisho kifungu cha 42 (1) (f) kinazungumza vizuri sana, mtu akipewa leseni, anapewa na sharti la kununua vitu ndani, na kama havipo ndipo atoke nje ya nchi, kuhusu ushiriki wa wananchi, makampuni ya madini yametakiwa kujisajili katika soko la hisa la Dar es salaam(DSE), Ili kila mwananchi aweze kumiliki hisa katika mgodi, Hili tutazungumza nao ili kuangalia namna ya kuliweka vizuri kwa uelewano mzuri.

Pia sheria hii mpya inachochea kuongeza uwezo wa kuongoza sekta ya madini kwani awali ilikuwa inakua kwa kasi na kuiacha serikali nyuma.

“Sisi serikali tulikuwa tumebaki nyuma, tukajikuta sekta inakua kuliko nguvu yetu ya kuiongoza, sasa nimekuwa na wasaidizi wa kamishna 14, na wakala wameangeozwa. Pia tumeanzisha Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), anayochukua nafasi ya kampuni ya ukaguzi wa madini ya Alex Stewart (Assayers).

Ameongeza kuwa sheria mpya ya madini imeongeza ushiriki wa serikali katika sekta hiyo licha ya kwamba haileti mtazamo mzuri kwa wawekezaji wakifikiri kuwa Tanzania inataka kurejesha seara ya uchumi wa kijamaa.

Aidha Kamishna huyo anaeleza kuwa kuwepo kwa sheria hiyo mpya kunaongeza viwango vya mrahaba unaotakiwa kulipwa na wawekezaji serikalini.

Katika eneo lingine ambalo sheria hiyo mpya inagusa ni mfumo bora wa utoaji wa fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha upanuzi au kuanzishwa kwa mgodi.

Dk. Kafumu anaeleza: “ Awali tulikuwa tukitumia sheria ya ardhi kulipa fidia sasa sheria mpya imetoa maelekezo ya kutosha tumeona tuwe na mpango wa kuwahamisha wananchi hao, kwa kuwajengea nyumba mpya na kuwawezesha wakae, na wasihamishwe kwa nguvu na kulalamika, tunampa makazi kabisa ya uhakika, na akihama asipate shinda. Mtu anapewa milioni 500, halafu kesho anarudi kulalamika kuwa alipunjwa sasa tunampa makazi mazuri.

mwisho

No comments:

Post a Comment