Na Deogratius Temba
‘Naiomba jamii itambue kuwa wanawake wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi na wapo wenye sifa nzuri hata kuliko wanaume. wapewe nafasi ya kuonyesha vipaji na uwezo wao” hii ni kauli ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza na Mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).
Mahiza siyo mgeni katika masikio ya watu wengi hapa nchini hasa kutokana na kazi anayoifanya ya Unaibu waziri wa elimu unaomfanya kuwa karibu na watu wengi hasa walimu, wadau wa elimu na wanafunzi.
Mbali na nafasi hizo za uongozi pia Mahiza, amekuwa mwalimu kwa kipindi kirefu nafasi iliyomfanya kuwa karibu na watanzania wengi ambao leowamefanikiwa kuwa katika nyanja mbalimbali hapa nchini.
Katika mahaojiano maalumu niliyofanya naye ofisini kwake hivi karibuni Mahiza, anaeleza kwa ujasiri mkubwa jinsi anavyojiamini katika utumishi wake wa umma na kisiasa.
Mahiza ni mbunge wa viti maalumu, ambaye ameingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005, katika mahojiano anajibu hivi:
Mwanadishi: Umeingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005, na kupewa unaibu Waziri unaionaje kazi ya Ubunge.
Mahiza: Ubunge ni kazi nzito na ina majukumu magumu na siyo rahisi kama watu wengi wanavyofikiri. Kazi kubwa ya mbunge ni kujitoa kwa ajili ya wananchi, nchi na taifa lako. Hapo utakuwa mwakilishi wa wananchi.
Majukumu mengine ya mbunge kwa wananchi wake nilazima ayatimize. Kwasababu anakula kiapo cha kuwawakilisha na kuwatetea ni lazima ayatimize.
Mwandishi: Kwa muda huu umejifunza nini katika ubunge wako?
Mahiza: Kwanza nimetambua majukumu yangu kama mbunge, pili wananchi wanapenda mbunge mkweli, muwazi, na mwenye kujituma.
Mwandishi: Umejifunza nini kwenye Unaibu waziri?
Mahiza: Nimegundua kuwa uwaziri una majukumu makubwa zaidi ya kuitumikia jamii. Ukiwa waziri unatakiwakutembea zaidi kwenda kwenda maeneo ya kazi kuliko kukaa ofisini, unahitaji kuona hali halisi zaidi kuliko kusoma kwenye mafaili, unahitaji kuzungumza zaidi kuliko kusoma na kuzungumza sana na watendaji wa ngazi zote ili kupata uhalisia wa jambo.
Mwandishi: Umejisikiaje kuwa Naibu Waziri kwenye wizara ambayo inahusiana na taalamu yako?
Mahiza: Kwanza nimejikuta nikiumia sana kutokana na kufanya kazi na walimu ambao ni wenzangu, na wakati mwingi nikashindwa kuwatimizia mahitaji yao yote.
Mwandishi: Changamoto gani umezipata katika ubunge wako?
Mahiza: Katika ubunge wangu nimekumbana changamoto ya kutopatikana kwa huduma za kijamii za kutosha. Wananchi wanahitaji maji safi,barabara , madawa na vituo vya afya, zote hizo ni fedha na mbunge hana fedha serikali nayo haina fedha za kutosha.
Mwandishi: Unazichukuliaje changamoto za walimu nchini?
Mahiza: Ninaona tabu kweli. Nimekuwa mwalimu ninajua mahitaji ya walimu, ningepanda wote wawe na nyumba nzuri za kuishi, walipwe mishahara mizuri, ningetaka pia kuwepo na vitabu lakini hakuna. Ningetaka walimu wote wapate huduma nzuri.
Ninaona taabu kweli, ningefurahi nikikutana na walimu wakipata huduma nzurina kufanya kazi katika mazingira mazuri. Hii ni changamoto kubwa pia katika Unaibu waziri wangu.
Mwandishi: CCM kimetangaza ukomo wa ubunge wa viti maalumu kuwa ni vipindi viwili, wewe umelipokeaje hilo?
Mahiza: Nimelipokea vizuri, afadhali iwe hivyo. Viti maalumu ni mahali pa kujijengea uwezo, na kupata uzoefu wa uongozi tu lakini baadaye ukishapata nguvu unakwenda kupambana jimboni.
Mwandishi: Umejipangaje kukabaliana na hilo?
Mahiza: Nimeamua ninakwenda jimboni kugombea kipindi kimoja nilichokaa bungeni kwa tiketi hii kinatosha, nimepata uzoefu wa kutosha.
Mwanidshi: Unakwenda kugombea jimbo gani?
Mahiza: Jimnbo la Mkinga, mkoani Tanga, ninajiamini, ninaenda kuomba ridhaa ya wananchi, endapo watanikubalia ninawaahidi utumishi uliotukuka.
Mwandishi: Je utaweza kupambana na wanaume?
Mahiza: Ninaweza, ninajiamini na nina sifa, nimejipima na nimejitadhimini nikaona ninaweza.
Mwandishi: Unaweza kupambana na mfumo dume ambao unawasumbua wanawake wengi?
Mahiza: Nikueleze ukweli, na watanzania wengine wanielewe hususani wanawake wenzangu, mfumo dume unaondoka tu kama sisi wanawake tutajitoa, tukiogopa hautaondoka. Ni sisi kupambana nao.Wapo wanawake ambao wanauwezo wapewe sifa waonyeshe vipaji vyao, baadhi yao wana uwezo kuliko hata wanaume. mimi binafsi nikipewa ridhaa ninaweza.
Mwandishi: Rais Jakaya Kikwete, ametia saini sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha katika chaguzi, je wewe unalisemeaje hilo?
Mahiza:Sheria nimeipenda sana, itatusaidia sote sio akina mama pekee, matumizi ya fedha ni lazima yadhibitiwe ili kila mtu awe huru kugombea. Ninawaasa watanzania wote waisome sheria hiyo vizuri waitafsiri kwa mujibu wa kanuni zake.
Mwandishi: Unaweza kueleza uliingiaje katika siasa?
Mahiza: Ni wakati ulifika! Nilijiamualia tu baada ya kuona kuwa ninaweza kusimama na kuwatumikia watanzania kama mwanasiasa. Kwanza nilipata ujasiri mkubwa kutokana na nafasi niliyokuwa nayo ya Uenyekiti wa wakuu wa shule wa nchi za Afrika ya Mashariki, nikasema kwanini nisiwe kiongozi?.
Mwandishi: Katika familia au ukoo yupo mwanasiasa ambaye unafuata nyayo zake?
Mahiza: Hapana, ni mimi pekee nimeanza kuingia katika siasa ila wapo wanaoelekea kunifuata.
Naibu Waziri Mahiza, ni mtoto wa Mzee Saidi Bakari, amezaliwa Augost 12, 1954, katika Kijiji cha Moa, Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga. Ameolewa na Bakari Abdalah Mahiza, na wana watoto watano, wavulana watatu, na wasichana wawili.
Kazi alizowahi kuzifanya Mahiza hadi kufikia kuwa mwanasiasa, ni Ualimu, na kujiushughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara huku akifuga pia wanyama kama Mbuzi, Ng’ombe na kuku.
Mwantumu Mahiza, amesoma katika Chuo Kikuu cha Delhi India, mwaka 2000 hadi 2001, ambapo alipata Mafunzo ya Uongozi , Utawala na Mipango ya Elimu. mwaka 1998 hadi 1999, amesoma katika Chuo cha Ualimu Beitl Bell- Israel, ambapo alisomea elimu ya Saikolojia kwa watoto.
Mwaka 1997, Mahiza alisoma tena Israel na kupata mafunzo ya ukuzaji wa mitaala na 1990 hadi 1991, alisoma Chuo Kikuu chaOslo nchini Norway, alipopata Mafunzo ya ualimu , elimu maalumu kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Mwaka 1985 hadi 1986, Mahiza alisoma Chuo cha Ualimu Dar es salaam, ambapo alipata Stashahada ya michezo. Wakati mwaka 1972 hadi 1973, alitunukiwa Stashahda ya Ualimu katika chuo ualimu Korogwe Tanga.
Mahiza alisoma katika shule ya sekondari ya Ifakara Morogoro, na elimu ya msingi aliipata katika shule ya msingi Zingibar Moa Mkinga Tanga.
Mahojiano haya yamefanyika ofisini kwake Machi 18, 2010.
Elimu ni kujifunza! Tunajifunza kwa kusoma! Karibu katika Blog hii ili tufundishane na kubadilishana Mawazo
Popular Posts
-
*alikubali kushindwa kwa siasa za Kijamaa *hakujilimbikizia mali Na Deogratius Temba WAKATI taifa linaadhimisha miaka 10 ya kifo cha mwasisi...
-
Na Deogratius Temba KWARESMA ni kipindi cha mfungo kwa waumini Wakatoliki. Mfungo huu ni wa siku hamsini. Kipindi hiki kinaanza na ibada ya ...
-
KAMPALA Uganda Dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ARVs, zikitumika sambasamba na dawa mseto aina ya (co-Trimoxazole), ...
-
Na Deogratius Temba. NI takribani miaka mitano tangu ililipo ibuika suala la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua sh. Bilioni ...
-
*Ilizamishwa ziwani na wakaoloni baadaye ikafufuka *Ina Umri wa miaka 98, mwaka 2013 itavunja rekodi ya dunia Na Deogratius Temba MV Liemba ...
-
Na Deogratius Temba SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigambo...
-
*Ni ajali iliyoweka historia kwa kuua *Bado usalama wa ziwani haujaimarika Na Deogratius Temba MEI 21, mwaka huu taifa limetimiza miaka 14 ...
-
, tutaendanayo mpaka uchaguzi Mkuu 2010 Na Deogratius Temba MWISHONI mwa wiki iliyopita Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha mapinduzi, (CCM), w...
-
TITLE OF THE PROJECT The effect of Water Conflict between Investor of VASSO Estate and Villagers in Kibosho Dakau, Moshi Kilimanjaro JOURNAL...
-
Taasisi ya mafunzo ya Jinsia (GTI) inayomilikiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) inaendelea na mafunzo ya kuwanoa wanaharakati kuanzia ...
No comments:
Post a Comment