Popular Posts

Tuesday, March 16, 2010

MATUKIO MAKUBWA KUTOKA MAHAKAMANI 2009

Na Happiness Katabazi

MKURUGENZI wa mashitaka(DDP),Eliezer Feleshi, kwaniaba ya serikali ya awamu ya nne chini ya rais Jakaya Kikwete, ameweka historia itakayoendelea kukumbukwa na taifa hili, kufuatia uamuzi wake wa kuwafunguliwa kesi za jinai baadhi ya waliokuwa vigogo serikali na watu maarufu kwenye jamii.

Ibara ya 59B(1) ya Katiba ya Nchi, inatamka kuwa kutakuwa na ofisi ya DPP na Ibara ya 59(2) inaeleza kazi za DPP na Ibara ya 59(3) inataja majukumu ya kiongozi huyo likiwemo jukumu la ufunguaji mashtaka kiongozi huyo.

Pia anaweza kuteua watu wa kuzifanya, Ibara ya 59(4) inasema: “DPP katika kutekeleza majukumu hayo hatakiwi kuingiliwa na mtu yeyote ili mradi majukumu anayoyafanya yawe ni ya maslahi ya umma, haki na azuie ukiukwaji wa misingi ya kisheria.”

Misingi hiyo iliyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kuhusu DPP pia imeainishwa kwenye kifungu cha 6 na 8 cha Sheria ya Kusimamia Mashtaka nchini ya mwaka 2008.

Kutokana na hatua hiyo ya DPP kuwafungulia kesi watu wa kada hizo, imeleta mwamko kwa wengine kuanza kudai haki zao, hakika hili ni jambo jema kwa taifa letu ambalo tumeridhia liongozwe kwa misingi ya sheria.

Ieleweke kuwa, DPP kumfunguliwa kesi mshitakiwa siyo hoja, hoja ni upande wa Jamhuri, mwisho wa siku uthibitishe pasipo shaka kesi yao ili washitakiwa waliowashitaki watiwe hatiani kwa makosa hayo na sivinginevyo.

Kwa utangulizi huo mdogo, fuatana na mwandishi wa habari za Mahakama, ili aweze kukujuza baadhi ya matukio makubwa ya kesi zilizotokea mwaka huu.
Hakimu awanya wanahabari kuripoti habari za EPA

Januari 14:
Kinara wa Richmond Kortini
HATIMAYE serikali ilimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mtu anayetajwa kuwa kinara wa kashfa ya Richmond.Mtuhumiwa huyo, Naeema Adam Gile, alipandishwa kizimbani, kwa tuhuma za kughushi na kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa serikali.Hadi sasa upande wa mashitaka umekuwa ukidai upelelezi haujakamilika hali iliyopelekea mahakama hiyo hivi karibuni iuamuru upande wa mashitaka Februali mwaka huu,itakapokuja kwaajili ya kutajwa ije ieleze mahakama upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua gani.

Januari 20, 2009
Mahakama yaficha ukweli

KATIKA hali ya kushangaza, aliyekuwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya, amewapiga marufuku wanahabari kuripoti mwenendo wa kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Shaaban Maranda na wenzake watatu.

“Tumeshangazwa na uamuzi wa Hakimu Lyamuya, kwani siku zote tunashinda hapa mahakamani tunaripoti kesi mbalimbali ikiwemo kesi hizi za EPA, na moja ya kesi za EPA anaiendesha yeye, hajawahi kutuambia tusiripoti, lakini leo (jana) ushahidi unaanza kutolewa anatuambia hatuna kibali cha kuripoti, kwa kweli tumeshindwa kumwelewa....tuna mashaka hapa kuna kitu, si bure, tena tunaomba uongozi wa mahakama nchini na serikali kuingilia kati suala hili, kwani maneno mengi yamesemwa kuhusu kesi za EPA kwamba ni za kiinimacho, CCM inajiandalia mazingira ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2010, na fedha za walipa kodi zimetumika kuhakikisha watuhumiwa wa EPA wanafikishwa mahakamani, sasa kesi zinaanza kusikilizwa, sisi wanahabari ambao tuna jukumu mahususi la kuhabarisha umma kinachoendelea katika kesi hizo tunaambiwa tusiandike habari’walihoji wanahabari wanaoripoti habari za mahakama

Liyumba afunguliwa mashtaka ya matumizi mabaya pesa za umma
Januari 27, 2009:
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, wamefunguliwa mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kusababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, baada ya kuidhinisha ujenzi wa minara Pacha ya BoT bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Zombe aanza kujitetea
Februali 10, 2009
ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauji ya watu wanne,alianza kujitetea na kuieleza Mahakama Kuu na kuanza kumwaga machozi kizimbani.

Zombe alimwaga machozi mara kadhaa wakati akijitetea mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Masatti kuhusiana na tuhuma hizo zinazomkabili yeye pamoja na askari wenzake tisa.

Liyumba apata dhamana ya utata
Februali 17, 2009
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala (BoT)Amatus Liyumba, amepata dhamana ya sh milioni882, huku serikali ikilalamika nje ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoridhika na hatua hiyo

Machi 12,2009
Raia 37 wa kigeni mahakamani kwa uvuvi haramuRAIA 37 wa waliokamatwa kwenye meli ya Tawaliq 1 iliyokuwa ikifanya uvuvi haramu katika kina kirefu cha bahari ya Hindi eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , wamefikishwa mahakama ya Kisutu na kusomewa mashitaka mawili ya uvuvi haramu, walikuwa wamevua tani 70.

Machi 30,2009
Chenge kortini kwa kuendesha gari kwa uzembe
ALIYEKUWA Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge afikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni akikabiliwa na mashitaka ya kuendesha gari kwa uzembe hivyo kusababishia mauaji ya watu wawili na hadi sasa kesi hiyo inaendelea upelelezi umekamilika.

Machi 26,2009
Shahidi kesi ya Mahalu atao ushahidi kwa njia ya video

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin, ulifunga ushahidi wake, ambapo siku huyo shahidi wa mwisho ambaye ni mwanasheria nchini Italia alitoa ushahidi wake kwa kutumia video ambapo siku hiyo mahakama ya Kisutu iliama na kuamia Jengo la IFM na kusikiliza kesi hiyo.

Watatu Kortini kwa kuiba bil.1/-kwa njia ya mtandao
Mei 4, 2009
WATU watatu walipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka 209 kwa tuhuma za kuiba sh bilioni moja kwa njia ya mtandao wa kompyuta, mali ya Benki ya National Microfinance Bank (NMB).
Washitakiwa hao ni karani wa benki hiyo, Mtoro Midole (42), Daudi Kindamba (47) na John Kikopa (46), ambao wote ni wafanyabiashara na wakazi wa jijini.

MwanaHALISI latakiwa kumlipa Rostam bil.3/-
Mei 12, 2009

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ililiamuru gazeti la kila wiki la MwanaHALISI na washitakiwa wengine kumlipa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz fidia ya sh bilioni tatu kwa kuandika habari za kumkashifu na za uongo zilizomhusisha na umiliki wa kampuni ya Richmond.

Mbali na hilo, Mahakama Kuu katika hukumu yake ambayo inaweza kuibua mjadala mkubwa katika taaluma ya uandishi wa habari kwa siku zijazo, imeliamuru gazeti hilo, kuandika habari yenye uzito ule ule katika ukurasa wa kwanza kukanusha habari hiyo dhidi ya Rostam.

Mei 13,2009
Mahakama yakataa ombi la Dowans

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara, Dar es Salaam, ililifukuza ombi la Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, lililokuwa likiitaka mahakama hiyo ifute maombi ya Shirika la Umeme (TANESCO) la kutaka mitambo hiyo isiuzwe kwa sababu yalikuwa na dosari za kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Robert Makaramba, ambapo alisema amefikia uamuzi wa kutupa maombi hayo kwa sababu Dowans imeshindwa kuishawishi mahakama ni vipi Tanesco ilitumia vifungu vya sheria visivyo sahihi kuwasilisha ombi lake katika mahakama hiyo.

Mei 27,2009
Liyumba afutiwa kesi
HAKIMU Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, afutiwa kesi baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa imekosewa, lakini muda mfupi baadaye walikamatwa tena mahakamani hapo.

Mei 28,2009
Liyumba asomewa mashtaka mapya

KUKAMATWA na kuachiwa kwa huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, iliendelea tena baada ya mshitakiwa huyo kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka mapya.

Mei 31,2009
Serikali yaweweseka mgombea binafsi

KWA mara pili tena, serikali imekata rufaa dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Democrat (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, katika Mahakama ya Rufani nchini, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ulioruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu.

Juni 8,2009
Korti kuu yambana Mahalu

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeyatupa maombi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala wa Fedha, Grace Martin, wanaokabiliwa na kesi ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh bilioni 2.

Katika maombi hayo, washitakiwa hao walitaka mahakama hiyo iwaachilie huru kwa sababu mwenendo mzima wa kesi yao ya msingi, una dosari za kisheria.

Juni 9,2009
Korti Kuu yasikiliza Rufaa ya DPP vs Liyumba
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imesikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, kupinga uamuzi wa kulegezewa masharti ya dhamana

Juni 10,2009
Maranda ana kesi ya kujibu –Mahakama
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Rajabu Maranda na mpwawe, Farijala Hussein, wanaokabiliwa na kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), wana kesi ya kujibu.

Mei 30,2009
Liyumba alegezewa masharti ya dhamana

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu ililegeza masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ambaye anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.Sasa atapata dhamana kwa kuwasilisha hati ya mali au fedha taslimu sh milioni 300 badala ya Bilioni 112.

Julai 21,2009
Vigogo sita kortini kwa tuhuma za kusafirisha pembe za ndovu
VIGOGO sita wa makampuni binafsi ya kupakia na kusafirisha mizigo nchini, walifikishwa walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu wakikabiliwa na kesi za uhujumu uchumi, kwa kusafirisha nje ya nchi jumla ya kilo 11,061 za pembe za ndovu zenye thamani ya sh 791,514,020 za meno ya tembo kwenda Hai Pong, Vietnam, na Manilla Philippiness, zenye thamani ya sh 684,827,000 mali ya Serikali ya Tanzania.

Mbele ya Hakimu Mkazi Anisetha Wambura, Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila, aliyekuwa akisaidiana na Michael Lwena, Shadrack Kimaro na Abubakar Mrisha, alidai kuwa kesi hiyo inamkabili Eladius Colonerio (39) ambaye ni Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd, Gabriel Balua (33), Meneja Usafirishaji wa nje na ndani ya nchi wa kampuni hiyo, na Shaban Yabulula (44) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kigoma M. N Enterprises (T) Ltd.

Agosti 17,2009
Zombe ashinda kesi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwaachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa sita, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, amebaini kuwa serikali imeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo.

“Katika kesi hii upande wa mashitaka licha ya kuleta mashahidi 37 na vielelezo 23, umeshindwa kuithibitishia mahakama kuwa ni kweli washitakiwa wote ndio waliowaua marehemu na kwa sababu hiyo nawaachia huru washitakiwa wote.Na kwa kuwa mahakama hii imewaona washitakiwa si wauaji, hivyo kuanzia sasa naliagiza Jeshi la Polisi liende kuwasaka wauaji wa marehemu wale, na Zombe na wenzake waachiliwe huru,” alisema Jaji Massati na kuuacha umati wa watu ukiwa umeshangaa.

Jaji Massati, alisema kamwe mahakama haiwezi kumhukumu mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria. Baada ya Jaji Massati kutamka kuwaachia huru washtakiwa hao, Zombe na Christopher Bageni (aliyekuwa mshitakiwa wa pili) walikumbatiana kizimbani kwa furaha na wananchi waliokuwa wamefurika katika ukumbi namba moja mahakamani hapo wakionekana kushangilia na wengine kuhuzunika.

Septemba 10,2009
IGP Mahita aumbuka

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemwamuru aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Omar Mahita kulipa malimbikizo ya gharama za matunzo ya kumhudumia mtoto Juma Omar Mahita (12) baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa mtoto huyo ni wake.

Oktoba 2,2009
Mtoto wa Keenja mbaroni kwa dawa za kulevya
MTOTO wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Charles Keenja (CCM), Agatha Keenja, alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na kosa la kukutwa na dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 6.6 zinazokadiriwa kuwa na thamani y ash 60,000.

Oktba 2,2009
Jeetu aitikisa Serikali
MAHAKAMA ya Kisutu ilitoa uamuzi wa kusimamisha usikilizaji wa kesi tatu zinazomkabili mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Patel na wenzake,hadi pale kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao Mahakama Kuu itakapomalizika.

Novemba 2,2009
Kesi ya Mramba yaanza kuunguruma

KESI ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba,aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Hazina, Gray Mgonja, ilianza kuunguruma kwa mara ya kwanza ambapo shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka , Nyero Matihiza (48), alitoa ushahidi wake na kudai kuwa ushauri wake wa kitaalamu alioutoa ulipuuzwa na viongozi wake.

Novemba 2,2009
DPP afuta kesi ya mfanyabishara Merey na wenzake
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Merey Ally Saleh, maarufu kwa jina la Merey Balhabou na mwenzake, Abdallah Said Abdallah, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa dola milioni 1.08 (zaidi ya sh bilioni moja) , wamefutiwa mashitaka.Washitakiwa hao wamefutiwa mashitaka baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuwasilisha hati ya kuwafutia mashitaka washitakiwa hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Merey na mwenzake, wameachiwa huru chini ya kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambacho kinampa mamlaka DPP kuwaondolea mashitaka watuhumiwa.

Novemba 31,2009
Rufani ya ‘Babu seya’ yashindwa kusikilizwa
MAHAKAMA ya Rufani nchini, ilishindwa kusikiliza rufaa ya mwanamuziki mahiri wa dansi hapa nchini, Nguza Viking maarufu kwa jina la ‘Babu Seya’ na wanae watatu Papii Kocha Nguza,Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao wanatatewa wakili wa kujitegemea Mabere Marando.Kwa sababu pande zote mbili katika kesi hizo hazikuwa tayari kuanza kusikiliza rufaa hiyo.
Babu Seya alionewa-Wakili

Desemba 3, 2009
Babu Seya alionewa-Wakili

MAHAKAMA ya Rufani nchini, ilisikiliza rasmi rufaa ya Mwanamuziki mahiri wa dansi nchini, Nguza Viking maarufu “Babu Seya’ na wanawe watatu.

Wakili wake Mabere Marando aliomba mahakama iwaachirie uhuru warufani hao kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa imepangwa.Sambamba na hilo, mawakili hao Marando na Hamidu Mbwezeleni, walieleza kuwa tangu waanze kazi ya uwakili miaka 30 iliyopita, hawajawahi kuona hukumu ya ovyo kama hiyo.

Mawakili hao walieleza hayo mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Nataria Kimaro, walipokuwa wakiwasilisha sababu za kupinga rufaa ya Mahakama Kuu iliyolewa na Jaji Msaafu, Thomas Mihayo na hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Addy Lyamuya ambao wote walitia hatiani kwa makosa ya kubaka.Siku hiyo mamia ya watu wa kada mbalimba walifurika mahakamani hapo kwaajili ya kusikiliza rufaa hiyo.

Desemba 15,2009
Viongozi wa DECI kortini tena
HATIMAYE waliokuwa wakurugenzi wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) iliyokuwa ikijihusisha na shughuli za kuvuna na kupanda fedha, kwa mara nyingine tena walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na kusomewa mashitaka ya wizi wa sh milioni 118 mali ya DECI (Tz) Ltd.Washitakiwa hao ni Dominick Kagendi, Jackson Sifael Mtaresi, Timetheo ole Lating’ye na Samuel Sifael Mtaresi wanaotetewa na wakili wa kujitegemea, Hudson Ndusyepo.

Desemba 21,2009
Vigogo wa DECI wanyimwa dhamana

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewanyima dhamana Wakurugenzi wa taasisi ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci) wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa sh milioni 18 kutokana na kukiuka masharti ya dhamana waliyopewa awali.

Nawatakia wasomaji wote mwaka mpya wenye mafanikio na afya njema.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,(toleo maalum la matukio makubwa yaliyojitokeza mwaka huu, Desemba 31 mwaka 2009

No comments:

Post a Comment