*sheria inaandaa viongozi matajiri
*Masikini hawezi kusaidiwa kugombea
*matajiri wa CCM kundelea kuneemeka
Na Deogratius Temba
TUMEBAKIZA miezi takribani tisa ili kuingia katika uchaguzi Mkuu wa kuwachangua viongozi wakuu wa taifa hili ambao ni rais, Wabunge na madiwani.
Uchaguzi huu unakuwa ni wa tano tangu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini mwaka 1992, na ni takribani miaka 18 tangu tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi nchini.
Tutakumbuka kuwa lengo la kuanzisha mfumo huu haikuwa kutengeneza au kuongeza matabaka ya kiuongozi au kiutawala, ilikuwa ni kukuza demokrasia na kuongeza wigo wa kuondoa uongozi wa mtu mmoja yaani chama kimoja kuendelea kutawala na kumsimamisha mtu huyo huyo.
Serikali ilipokubali mfumo huu, iliendelea kutumia sheria iliyokuwa imetungwa kabla ya ujio wake, mwaka 1985. Pia uchaguzi wa kuwatafuta viongozi wa serikali za mitaa pamoja na kuwa ulianza kufanyika chini ya mfumo mpya wa vyama vingi bado uliendelea kuwa kwenye sheria ya zamani ya mwaka 1979. kwa kawaida hizi zilihitaji marekebisho tangu awali.
Sasa Serikali imeamua kupeleka Bungeni Muswada wa sheria mpya ya kufanyia marekebisho sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 sura ya 343, na sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa ya mwaka 1979 sura 292, ambapo wabunge watapata nafasi ya kuujadili na hatmaye kama watakubali kuupitisha utapelekwa kwa rais kwaajili ya kupitishwa kuwa sheria.
Muswada juu ya maboresho hayo ulishatolewa na ofisi ya Waziri Mkuu na kuchapwa kwenye gazeti la serikali la Desemba 11 mwaka na gazeti la serikali la kila siku la Daily News la Desemba 22, liliuchapa Muswada huo kwa lugha ya kiingereza. Sote tunajua tatizo la Watanzania hata wale waliosoma hatupendi lugha ya Kiingereza na wengi pia hatuiwezi.
Muswada unapochapwa kwenye gazeti la umma, ili wausome watu halafu ukawa kwa lugha ya kiingereza ni dhahiri kuwa hakuna nia ya dhati ya kutaka kila mtu auelewe, hivyo hivyo kwa ujumbe mwingine wowote. Mwanzoni mwa wi,ki iliyopita wadau wachache wamealikwa na serikali kushiriki katika kikao cha kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria na Katiba kuujadili, lakini tunajiuliza kundi hilo linatosha na je ndilo litakao ufaidi muswada au sheria hiyo?
Binafsi nimeupitia muswada husika pamoja na kuwa umeonesha njia ya kutaka kudhibiti rushwa katika uchaguzi, na matumizi mabaya ya fedha ndani ya uchaguzi bado nauona kama ni mlango wa ushindi kwa wote wenye uwezo.ni sheria inayoleta neema kwa matajiri hasa walioko ndani ya CCM.
Tunakokwenda kama hali itabaki kuwa hivyo. na muswada ukapita na kuanza kutumika kama sheria katika uchaguzi huu mkuu basi tujue kuwa uongozi wa nchi hii utakuwa mali ya matajiri. wenye nacho watakuwa wakishinda kuiulaini kwasababu tayari wanazo fedha zao wenyewe na siyo za mtu.
Unaweza kuwa ndiyo mwanzo na mwisho wa masikini kushiriki katika chaguzi ingawa. Kwenye muswada husika tayari kuna vipengele na vifungu vingi ambavyo vinaumiza wapizani na masikini.
Binafsi mimi siyo kada wa vyama hivi vya upinzani, ukiacha uanaharakati wangu, lakini ukiangalia wagombea wengi wanaojitokeza kupitia vyama hivyo ni masikini, na hata leo rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, anakiri kuwa matumizi makubwa ya fedha yapo ndani ya chama chake.
Pamoja na upungufu mkubwa uliopo katika miswada hiyo kama ilivyoelezwa ni wazi kuwa serikali itatumia wingi wa wabunge wake bungeni ili kuupitisha. Hili liko wazi maana tumeshuhudia miswada kama hiyo mara nyingi ikipita kwa makofi,
Huku nyuma tutakumbuka jinsi ambavyo CCM, kilitumia wingi wa wabunge wake kupitisha sheria ya takrima, hakitashindwa kuupitisha huu unaokibeba katika chaguzi.
Muswada huo unaonekana wazi kuvibana vyama vya upinzani ambavyo kwa kawaida havina fedha, kutokana na kuvitaka kumtaja mtu binafsi aliyevichangia na kiasi alichotoa.
Kwa kuangalia vipengele vichache ambavyo vinaonyesha wazi kuubana upinzani na masikini ambao wanataka nafasi za uongozi hasa wale wanaotarajia kuomba fedha kutoka kwa marafiki zao, tunaweza kuona jinsi ambavyo ubunge na udiwani unabakia kuwa nafasi ya wateule wachache na wanaohitajika na matajiri wachache.
Ibara ya 8 kifungu cha kwanza cha sheria hii kinasema “Utakuwa ni wajibu w a kila chama cha siasa kufanya na kugharamia chaguzi za chama chake kwa kutumia fedha zake za ambazo zitatoka katika vyanzo vyake vilivyoainishwa katika sheria ya vyama vya siasa.
Katika kifungu cha 11(1) na 19 unavitaka vyama kutoa taarifa za mtu binafsi anayechangia zaidi ya sh. 500,000 au chama au shirika linalochangia ziadi y a sh. Mil.1. je ni kweli kuwa wachagiaji wote watapenda kutajwa? Hapo imevinyima vyama vyote masikini na wagombea masikini uwezo wa kusimama kushindana.
Ibara ya 11(4) nayo imekataza mtu kupokea mchango wa gharama za kampeni kutoka kwa mtu au asasi moja kwa moja isipokuwa kupitia chama, na kusema kuwa hii inaandaa mazingira ya kuzika kwa mitafaruku ndani ya vyama hasa visyo na uwezo wa kifedha
Katika kifungu cha 12(1) na (3) wa muswada huo, unamzuia asasi , shirika au kampuni kuingiza nchini fedha toka nje(a) ndani ya siku 90 kabla ya uchaguzi mkuu au (b).
Udhaifu kwenye katiba ya Jamhuri
Nchi nyingi duniani hata za Afrika mara baada ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi, ziliunda katiba mpya ili kuwa na misingi na mifumo mipya ya kujiongoza. Kw a mfano Nigeria ilibadilisha katiba yake mwaka 1999, Ghana 1992, na Afrika ya Kusini, mwaka 1994.
Tanzania hata baada ya kuwa katika mfumo wa vyama vingi kwa takribani miaka 18 sasa, bado katiba inayotumika ni ile ya mwaka 1977, ambayo kama tunavyojua iklianzishwa na chombo kilichoitwa ‘Tume ya Katiba’ iliyokuwa na wajumbe 20 Akiwemo Spika wa zamani wa Bunge na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa.
Hadi leo katiba ya nchi imefanyiwa marekebisho na kubandikwa viraka mara 14, toleo tunalolitumia la mwaka 2005, ndilo lenye mabadiliko ya 14, je kuna kitu gani tunachokiogopa?
Sheria nyingi kandamizi na sizizotoa uhuru ambazo zinapingwa na nyingine kutakiwa kufutwa zinabebwa na katiba iliyopitwa na wakati, tukikubali kuibadilisha sheria hizo nazo zitafutwa.
Maeneo mengine kama uwepo wa Tume ya Uchaguzi isiyo huru, kwasababu iliyopo inaundwa na ibara ya 74 ya katiba ya nchi, kwahiyo kwa viongozi wa vyama vya upinzani na wanaharakati wanaodai Tume huru ya uchaguzi wajue kuwa haitawezekana bila kuifanyia mabadiliko katiba au kuifuta ibara ya 74 ya katiba (kitu ambacho hakitakiwi) kazi ni kutengeneza katiba mpya.
Suala la mgombea Binafsi
Suala hili pamoja na kuwa Mahakama Kuu ililiruhusu baada ya Mchungaji Mtikila kushinda kesi yake, bado katiba ya nchi hailiruhusu imektaa katika ibara ya 39(1) kimeeleza kuwa “Mtu hata chaguliwa kushika kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ispokuwa tu kama….(c) ni mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa,” hapo hakuna suala la mgombea binafsi, katiba imelikataa.
Pia madaraka makubwa anayopewa rais ni tatizo kwa Tanzania. binafsi sitaki kuikataa katiba iliyopo kuwa haina sifa za kuwa katiba, ila haiendani na wakati tulionao, kama itaendelea kuwepo migogoro ya kuwa kuna uvunjivu w a haki na kubinywa kwa demokrasia haitaisha kamwe.
Nini kifanyike kwa uchaguzi wa 2010
Kwa upande wa uchaguzi unaokuja kama tuinataka kuwepo na amani, tuondokane na malalamiko ambayo yamekuwa yakijirudia kila baada ya chaguzi kubwa na ndogo, ni lazima tufanye yafuatayo kwa haraka.
Kufuta kifungu cha 7,7A na 8 cha sheria ya uchaguzi sura ya 343 na badala yake kuipa tume ya uchaguzi mamlaka ya kuteua maafisa na wafanyakazi wake kama itakavyoona inafaa badala ya kutegemea au kusubiri kuteuliwa na mamlaka nyingine ambayo ni rais.
Matumizi ya maafisa wa serikali, wakurugenzi wa halmahsauri kwenye uchaguzi hauzingatii uhuru, na haki na hilo ni chanzo cha vurugu katika chaguzi kila matokeo yanapotangazwa. Kufuta ibara ya 39 (1) © na 67(1)(b) ya katiba ili kuruhusu mgombea binafsi kama ilivyoamriwa na mahakama kuu.
Kurekebisha Ibara ya 74 ya katiba ili kumpa Mwenyekiti wa NEC nguvu ya kuteua wajumbe wa Tume yeye, kama ilivyo kwa majaji na tume yao, na kuhakikisha kuna usalama wa kutosha wa watumbe wa tume(security of Tenure), tofauti na sasa ambavyo rais anaweza kumfukuza mjumbe wa Tume muda wowote na kwasababu zake anazoona yeye.
Kuiwezesha tume kuteua makamishna wa tume katika kila wilaya ili wakurugenzi wa halmashauri wasitumike tena. Kuwazuia watumishi wa serikali kama wakuu wa mikoa, Wilaya, maafisa watendaji, kujihusisha na shughuli za uchaguzi.
Pia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ipewe uhuru wa kutosha isiwe chini ya mamlaka za juu za kisiasa maana atapendelea chama kinachotawala kwa wakati huo.
Msajili huyo aajiriwe na tume ya utumishi wa mahakama ana ikiwezekana awe ni mtu mwenye hadhi ya jaji wa mahakama kuu au mahakama ya rufaa. Na awe ni mtu ambaye wakati wowote anasifa za kuweza kuteuliwa kuwa jaji wa ngazi hizo.
0784 / 715 686575
www.deotemba.blogspot.com
Mwisho.
Elimu ni kujifunza! Tunajifunza kwa kusoma! Karibu katika Blog hii ili tufundishane na kubadilishana Mawazo
Popular Posts
-
*alikubali kushindwa kwa siasa za Kijamaa *hakujilimbikizia mali Na Deogratius Temba WAKATI taifa linaadhimisha miaka 10 ya kifo cha mwasisi...
-
Na Deogratius Temba KWARESMA ni kipindi cha mfungo kwa waumini Wakatoliki. Mfungo huu ni wa siku hamsini. Kipindi hiki kinaanza na ibada ya ...
-
KAMPALA Uganda Dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ARVs, zikitumika sambasamba na dawa mseto aina ya (co-Trimoxazole), ...
-
Na Deogratius Temba. NI takribani miaka mitano tangu ililipo ibuika suala la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua sh. Bilioni ...
-
*Ilizamishwa ziwani na wakaoloni baadaye ikafufuka *Ina Umri wa miaka 98, mwaka 2013 itavunja rekodi ya dunia Na Deogratius Temba MV Liemba ...
-
Na Deogratius Temba SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigambo...
-
*Ni ajali iliyoweka historia kwa kuua *Bado usalama wa ziwani haujaimarika Na Deogratius Temba MEI 21, mwaka huu taifa limetimiza miaka 14 ...
-
, tutaendanayo mpaka uchaguzi Mkuu 2010 Na Deogratius Temba MWISHONI mwa wiki iliyopita Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha mapinduzi, (CCM), w...
-
TITLE OF THE PROJECT The effect of Water Conflict between Investor of VASSO Estate and Villagers in Kibosho Dakau, Moshi Kilimanjaro JOURNAL...
-
Taasisi ya mafunzo ya Jinsia (GTI) inayomilikiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) inaendelea na mafunzo ya kuwanoa wanaharakati kuanzia ...
No comments:
Post a Comment