Popular Posts

Wednesday, November 18, 2009

Rostam apigwa kombora

*Kimaro asema anaweweseka kutaka mitambo Dowans inunuliwe


Na Deogratius Temba

KAULI aliyoyatoa Mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz, akiliomba Bunge tena liunde kamati huru kuchunguza upya sakata la kuhusika kwake na kampuni ya Richmond Development LLC ili apate nafasi ya kusikilizwa, imepingwa vikali na baadhi ya wabunge wa chama chake.

Wabunge hao walisema Rostam anaweweseka na kashfa ya Richmond na kumtaka akasome vizuri kanuni za Bunge ili ajue kwamba suala likishaamuliwa na Bunge, haliwezi kuundiwa tume nyingine nje ya Bunge.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, mbunge wa Vunjo Aloyce Kimaro, James Lembeli (Kahama) na Lucas Selelii( Nzega), walisema Bunge likishahitimisha hoja, haliwezi kurudi nyuma kuijadili upya na kwamba Rostam anapaswa kufuata kanuni za Bunge.

Kimaro alisema hakuna sheria wala kanuni ya Bunge inayotamka kuwa kamati teule ya Bunge ikifanya kazi yake na Bunge likairidhia inaweza kuundiwa tena kamati nyingine nje ya Bunge.

“Bunge limeshamaliza kazi yake hakuna cha kurudia hapo, wala kanuni za Bunge haziruhusu kufanya vile nafikiri hajakisoma kitabu cha kanuni za Bunge ndio maana anaweweseka vinginevyo asingesema hayo.

“Ninawashauri watanzania kutojiingiza katika mjadala huo, umeshafungwa na Bunge likatoa mapendekezo yake na sasa tunaisubiri serikali itekeleze na siyo mtu mwingine aje tena Bungeni kuleta hoja hiyo hiyo, hapana sisi tunapiga hatua nyingine mbele,” alisema.

Alisema kama kuna watu hawakuridhika na kazi iliyofanywa na kamati teule ya Bunge iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harizon Mwakembe, wasifikiri kuwa kuna huruma tena au wakipiga kelele watapata msamaha.

“Tena wasifikiri kuwa kwa kupiga kelele vile serikali inaweza kuifikiria tena Dowans, hilo limepita na serikali haitaununua mtambo huo kwani hata sheria hairuhusu. Sheria ya Umeme ya mwaka 2008, imeeleza waziwazi kuwa kama kuna watu waliohusika kudai ‘capacity charge’ wasipewe nafasi ya kuiuzia Tanesco umeme,”alisema Kimaro.

Alidai kuwa kinachomsumbua Rostam hadi kufikia kuliuomba Bunge liunde kamati upya ni kutaka mitambo ya Dowans inunuliwe.

“Mimi ninataka kujua kinachomkera au kinachomfanya aweweseke ni nini? Awaeleze watanzania waelewe atumie muda huu kuueleza umma kama ana maslahi gani na Dowans au iliyokuwa kampuni ya Richmond na siyo kulitakia Bunge kazi ambayo siyo yake,” aliongeza Kimaro.

Naye Lembeli, alisema Bunge ni kwa ajili ya watanzania wote na maamuzi yaliyotoka ni ya wananchi wote.

Alisema Rostam hajaonewa na kamati kwani kamati ilitoa ripoti na wabunge wote wa CCM wakaiunga mkono kwa pamoja kwa hiyo kamati ilifanya kazi yake.

“Tatizo siyo kuonewa wala kamati teule ya Bunge, Rostam atafute kanuni za bunge azisome na aelewe zinasema je, kwanza asiionee kamati, sisi wabunge ndiyo tuliopitisha ripoti kama tungeona ina makosa na kubaini kuna mtu ameonewa, tungeikataa.

“Anapotumia muda mwingi kudai kuwa iundwe kamati upya mara jopo la majaji, kuchunguza upya mbona alishajitokeza mara kadhaa kwenye vyombo vya habari akadai kuwa hausiki? Kwani hilo halitoshi?, Mbona maelezo anayoyatoa kwenye magazeti kuwa hakuhusika hayaelezi kama alionewa? Na alionewa wapi?,” alisema Lembeli.

Akizungumzia suala hilo, Selelii, amabye alikuwa mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo teule alisema ndoto za Rostam ni za mchana na hazitekelezeki katika bunge hili na kwa kutumia kanuni hizi za Bunge zilizopo.

“Hizo ni ndoto tena za mchana, hakuna kitu kama hicho Bunge lilisha fanya kazi yake na kuimaliza, anachokitaka yeye hakiwezekani kwa Bunge la Tanzania, na kama ni kwa Bunge la hapa Tanzania basi siyo kwa kanuni hizi tulizonazo,” alisema

Alisisitiza kuwa siku zote mtu anayetuhumiw akwa kukosa hawezi kukubali kosa hata kama atachapwa namna gani kwa hiyo huo ni ujanja ambao unatumika kujinaua na tuhuma hizo.

Selelii, alimtaka Rostam achukue ripoti ya kamati hiyo, aangalie vipengele vyote vinavyomtaja kuwa ni anahusika na Richmond na Dowans, halafu aende kwenye hoja moja kwa moja bila kuzunguka.

“Kama kweli Rostam ana uhakika na hayo malalamiko ambayo anayatoa kila mara na hata kupitia baadhi ya vyombo vya habari, arejee kwenye ripoti yetu ya kamati, asome maeneo yote yanayomgusa na kumhusisha na Richmond na Dowans, halafu ajenge hoja,”alisema Selelii.

Hivi karibuni Rostam alikaririwa na chombo kimoja cha habari akidai kuwa analiomba Bunge liunde jopo la majaji watatu kuchunguza upya sakata hilo ili kutoa hukumu ya haki.


Siku chache baada ya Rostam kuomba Bunge liunde jopo hilo la majaji, Spika wa Bunge Samwel Sitta, alisisitiza kuwa haingii akilini, kwa Rostam kutaka uchunguzi wa suala hilo ufanywe na majaji.

"Kwanza, labda nikwambie tu, maamuzi yaliyofikiwa na Bunge katika Richmond hayawezi kuchunguzwa upya na mhimili mwingine wowote wa Dola," alisisitiza na kuongeza:

"Tunazungumzia kumaliza suala la Richmond si kuanza upya, kama ana pesa zake (Rostam) za kulipa majaji, ni huko huko, lakini hilo haliwezekaniĆ¢”.

Spika alisema ushahidi mbalimbali ulionyesha uhusiano wa mawasiliano ya mbunge huyo na Richmond kisha Dowans.
"Hivi mnataka ushahidi upi zaidi, ushahidi wa mawasiliano ulionyesha jinsi mtu huyu alivyokuwa akiratibu Richmond kisha Dowans," aliongeza Spika.

Rostam ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, lakini amekuwa akitajwa kama mmoja wa vigogo walioshiriki katika kufanikisha Richmond kupewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura katika mazingira tata.

Mkataba na kampuni hiyo yenye taarifa tata za kutoka Costa Rica na Marekani, ulisainiwa na Tanesco Juni 23, 2006.

Lakini baada ya kusakamwa kwa muda mrefu, alipopata nafasi katika kikao cha kamati ya Mzee Mwinyi na wabunge wa CCM, iliripotiwa kuwa Rostam aliongelea kuundwa kwa tume huru kuchunguza kashfa nzima ya Richmond kwa madai ile ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe, ilipotosha.

"Ripoti ya Richmond imeidhalilisha serikali kwa maslahi ya kisiasa. Ili mambo yaishe ni vema uchunguzi huru ukafanyika. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwachanganya wananchi," alisema Rostam.

"Msimamo wangu tangu kamati teule ya Bunge itoe taarifa yake bungeni, uko pale pale. Ripoti ilijaa upotoshaji na uongo. Nilitaka kuongea bungeni nikazuiwa."

Kamati teule ya Bunge ilisema katika taarifa yake kuwa Rostam aliitwa ili aeleze uhusiano wake na Richmond kutokana na kampuni hiyo kutumia anuani ya barua pepe na fax ya Caspian na sababu za kuitafutia Richmond kampuni ya ushauri wa mambo ya habari, lakini mbunge huyo wa Igunga hakujitokeza.

Rostam alijieleza katika mchango wake wa maandishi wakati wa kujadili ripoti ya Richmond kuwa Kamati ya Mwakyembe ilimuita kumhoji Desemba 24, wakati ikijua kuwa siku hiyo asingeweza kupatikana kwa sababu ya siku kuu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment