Popular Posts

Monday, June 1, 2009

Mtikisiko wa uchumi Duniani waikumba Tanzania

kikwete kuhutubia Bunge
*Ni kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani
*IMF yatoa mamilioni kuisaidia
*yaonya usimamizi imara wa fedha
*TRL,TICTS zaendelea kuwachefua wabunge
*Mkulo akana kuifahamu TICTS

Na Deogratius Temba

KUTOKANA na mtikisiko wa uchumi unaoikumba dunia, Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kulihutubia Bunge la jamuhri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa 15, wa Bajeti unaoanza wiki ijayo.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2008/09, katika semina ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alisema Rais, anaweza kulazimika kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri na baadaye kuhutubia Bunge ili kutolea ufafanuzi suala la mtikisiko wa uchumi na adhari zake kwa Tanzania.

“Kama mnavyojua baada ya dunia kukumbwa na mtikisiko wa uchumi, Rais aliliunda Tume ya wataalamu wa uchumi, inayo ongozwa na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Beno Ndullu, nimewapa muda wakutosha kutokana na unyeti wa taarifa hiyo, sasa watawalisilisha kwangu Juni 4, mwaka huu na siku hiyo hiyo nitampeleka rais ili aisome,” alisema.

Alisema hiyo ni taarifa ya serikali, baada ya rais kuisoma atashauriana na Baraza la Mawaziri, na baadaye anaweza kuomba kulizungumzia suala hilo Bungeni.

“Rais anaweza kuomba kuzungumza Bungeni, baada ya kushauriana na Mawaziri, aeleze hatua zilizochukuliwa nini kinatarajiwa kufanyika, maeneo ya kiuchumi au sekta zilizoadhirika na adhari za mtikisiko huo kwa Tanzania

Taarifa hiyo ya Gavana Ndullu, inaonyesha maeneo yote mabayo yameadhirika mazao yaliyopoteza bei au kutokununuliwa kabisa katika soko la kimataifa, na sekta nyingine zilizoadhrika au zilizoko hatarini kuadhrika,” alisema Waziri Mkulo.

Akizungumzia suala la uchumi wa taifa Mkulo, alisema hali ya uchumi wa nchi kwa sasa siyo shwari kwani uchumi umeshuka kwa pato la taifa kutoka asilimia 7.8 mpaka asilimia 5.7.

“Awali tulijarajia hadi kufikia Juni mwaka huu tungekuwa asilimia 7. lakini tayari tumeshashuka mpaka 5.7, hatuwezi kurudi tena huko juu kutokana na kwamba huu sio msimu wa mavuno, mahitaji ya fedha ni makubwa kuliko kipato, na hatuhuzi mazao nje ya nchi kwa sasa,” alisema

Mkulo, alisema ili kukabiliana na mtikisiko wa uchumi sambamba na kuanguka kwa uchumi wa taifa, serikali imejikita zaidi katika kutoa kipaumbele katika sekta vyanzo vya uchumi ambavyo ni imara na endelevu.

Mkulo alisema sekta ya Kilimo ndiyo iliyoadhirika zaidi na mtikisiko huo kutokana na wawekezaji wengi katika sekta hiyo kuwa wamekopa mitaji katika nchi zao, ambazo imeguswa na mtikisiko huo.

Wakati Taarifa hiyo ya ki-utaalamu ikisubiriwa kuwasilishwa kwa rais Kkwete, mwishoni mwa wiki hii Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Fedha Ulimwenguni (IMF), limetoa Dola za kimarekani Milioni 336, kama mpango wa miezi 12, wa kuinusuru Tanzania na mtikisiko huo wa uchumi.

Taarifa iliyoandikwa na Mkurugezni Mkazi wa IMF, nchini David Robinson, na kupatikana jijini Dar es salaam, jana ilisema kuwa fedha hizo zinztolewa kwa awamu na tayari dola Milioni 244, zimeshaingizwa serikalini.

“Fedha hizi zitazisaidia Tanzania katika akiba ya fedha za kigeni, ambayo imeshuka kwa asilimia 26, kutokana na kushuka kwa sekta ya utalii na zao la Pamba, na kufilisika kwa wawekezaji kutoka nje.

Tanznaia ipo kwenye nafasi nzuri katika sera ya kuwezesha wajasiriamali wadogo kiuchumi kwa zaidi ya miaka 10, na hii imesadia kuimarisha uchumi wa ndani na kudhibiti milipuko ya mfuko wa bei kila mara pamoja na kupunguza umasikini,” alisema Robnson, na kuongeza:

Mtikisiko wa uchumi wa dunia unakuja ukiwa na madhara makubwa kwa Tanzania ni kweli uchumi wa Taifa, mazao utalii, zimekatika kutokana na wawekezaji wa kimatifa kufilisika,” aliongeza.

Taarifa hiyo ya IMF, ilizidi kueleza kuwa Benki za Tanzania zipo imara kimitaji, lakini hazitoi mikopo, hali hii ya kushuka kwa uchumi unaweza kuziadhiri Benki mara moja, hatua za haraka za kitaalamu zinapaswa kuchukuliwa.

IMF imeshauri kuwa mpango unaoendelea wa kuimarisha Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini(MKUKUTA), kufanyia kazi kwa makini, kwa kuimarisha kilimo, miundombinu, na usimamizi imara wa sekta za kifedha na nchi kuepuka madeni yasiyo ya lazima.

Kwa upande wa Mkulo, yeye alisema kuwa sekta ya fedha nchini yaani mabenki na taasisi nyingine ni imara kutokana na kutokuwa na muunganiko wa moja kwa moja na mabenki ya kimtaifa yalkiyoadhrika katika mataifa yaliyoendelea.

Mkulo alikiri kuwa vyanzo vya mapato nchini havijapewa kipaumbele ndiyo maana kumekuwepo na kuzorota kwa ufanisi katika Bandari ya Dar es salaam, alisema serikali inatajaria kuboresha miundombinu ya Bandari, njia ya Baraabra ya Reli ya kati, reli ili kuongeza ufanishi katika kusafirisiha mizigo kutoka Dar es salaam, kwenda nchi jirani za DRC, Burundi, Rwanda, na Uganda.

Akichangia ripoti hiyo, Mbunge wa Mvomero(CCM), Suleiman Saddick, alimtaka waziri aeleze msimamo wa serikali hususani wizara yake juu ya kushindwa kufanya kazi kwa kampuni ya Kimataifa ya Kupakua na kupakia Makontena Bandarini (TICTS), ambayo imeshindwa kufanya kazi kama ilivyokubaliana kwenye mkataba.

Pia alimtaka Waziri kusema kama ni lini serikali itauvunja mkataba wa kampuni hiyo ambao umeongezwa kinyemela, ili kunusuru mapato ya taifa.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkulo, alisema Wizara yake haihusiki na mkataba wa TICTS, wala uchukuaji wa makontena bandarini.

„Kwa uaminifu mkubwa naomba nisilizunguzie suala hilo la TICTS, kwani ni la Wizara ya Miundombinu, mimi ninachoweza kufanya kwasababu nimesikia kilio chenu, nitashauriana na waziri wa Miundombinu Dk. Kawambwa, halafu nitalipeleka Bungeni kwenye ripoti yangu ya hali ya uchumi,” alisema.

Aidha, alisema kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha inaboresha huduma za bandari hasa bandari ya Dar es salaam ili kuongeza ufanisi katika njia za reli kuanzia Dar es salaaam, Isaka, Burundi na Rwanda, ili iweze kubeba mizigo mingi zaidi.

Mbunge wa Tabora Mjini(CCM), Siraji Kaboyonga, alihoji ni kwanini Kenya wanapata fedha nyingi kupitia katika sekta ya usafirishaji kutoka Bandari ya Mombasa ambayo inakua kwa kasi na kuwaingizia fedha nyingi kwa kutumia njia ya Reli wakati Tanzania kiwango cha utendaji kinashuka.

Alisema Kenya wanatumia njia za reli kuanzia Mombasa kwenda Uganda, Burundi na Rwanda, ambapo hupitisha mizigo yenye uzito wa tani milioni 15, wakati njia ya Reli kwa Tanzania inayoanzia bandari ya Dar es salaam, kwenda katika nchi hizo zinapitisha mizigo Tani Milioni 2, kwa mwaka

Waziri Mkulo alikiri kuzorota kwa huduma za barabara za reli kwenda katika nchi hizo na kudai kuwa kikwazo kikubwa ni kampuni iliyopewa jukumu la kutoa huduma ya Usafiri ya RITES kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Alisema kampuni ya RITES iliyo pewa Jukumu la kuendesha kampuni ya TRL, imeshindwa kufanya kazi licha ya serikali kuendelea kuiwezesha kifedha, alisema serikali haitaweza kuipa kampuni hiyo fedha nyingine za kuliendesha shirika hilo kwani imeshindwa kueleza matumizi ya dola milioni 7, walizopewa awali zilivyotumika.

„Tatizo siyo fedha, ni kwamba zile tulizowapa awali walizitumiaje?, hakuna mchanganuo wa wazi ni suala dogo kama ulipewa fedha za kuendesha kampuni unatakiwa ueleze ulizitumiaje, hatuwezi kuwapa tena kwasababu wakishindwa kulipa mwisho wa siku atalipa mlipa kodi wa nchi hii,”alisema

Tangu kuanza kwa mikutano ya kamati za kudumu za Bunge, wajumbe wa kamati hiyo, wamekuwa wakihoji uhalali wa mikataba ya kampuni za TICTS na TRL, ambazo zimeshindwa kutekeleza masharti ya mikataba baina yake na serikali.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment