Popular Posts

Monday, June 1, 2009

MENGI ATAJA MAWAZIRI WAOMWANDAMA

Serikali yamsononesha Mengi

MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ameeleza kusononeshwa kwake na Serikali kutokana na yale aliyofanyiwa mara baada ya kutaja majina ya watu aliodai kuwa ni mafisadi papa.

Akizungumza wakati wa ibada iliyofanyika juzi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kisereny wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Mengi alisema baada ya kutaja majina hayo, aliandamwa na baadhi ya mawaziri, vyombo vya dola na taasisi za serikali.

Katika ibada hiyo ya Sikukuu ya Pentekoste, mgeni rasmi alikuwa Mhashamu Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shayo na iliambatana na hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Shule ya Msingi Kisereny, uzinduzi wa zahanati ya Ndekyo na Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) cha Kisereny.
Huku akishangiliwa na umati wa waumini wa kanisa hilo lililopo katika eneo la kijijini kwake, Mengi alimtaja waziri wa kwanza kumwandama kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba.

Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk. Norman Sigalla na Mbunge wa Hai, Fuya Kimbita (CCM), Mengi alimtaja waziri mwingine aliyemwandama baada ya kutaja mafisadi papa kuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, aliyesema alimwita mbaguzi wa rangi.

Mwenyekiti huyo wa IPP, alisema mbali ya mawaziri hao kutoa kauli hizo, pia wahariri wa magazeti yake anayoyamiliki ya Kulikoni na Nipashe, walihojiwa na Msajili wa Magazeti wa Idara ya Habari.

Huku waumini wa kanisa hilo wakiwa kimya kumsikiliza kwa makini, Mengi alisema yeye mwenyewe pia aliitwa na kuhojiwa na Mamlaka ya Mawasilino Tanzania (TCRA), ikidai alivunja sheria ya utangazaji kwa kutaja majina ya watu kuwa ni mafisadi papa, na kwamba hatua hiyo iliashiria ubaguzi wa rangi.

Mengi ambaye alikuwa mgeni mwalikwa kwenye hafla hiyo, alivitaja vyombo vya dola vilivyomwandama kuwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ikimtaka apeleke vielelezo.

Kwa mujibu wa Mengi, pia aliitwa na maofisa wa Jeshi la Polisi, linaloongozwa na IGP, Said Mwema, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, inayoongozwa na Laurence Masha, wakimtaka apeleke vielelezo vya tuhuma zake.
“Nimeitwa na Kamati Ndogo ya Ulinzi na Usalama wa Taifa ili kuhojiwa juu ya tamko langu kuhusu ufisadi. Yote haya yamefanyika pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani juu ya jambo hili.

“Tukumbuke kwamba Mh. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikwishatoa tamko bungeni kuwa wote waliotajwa, kama wanaona hawakutendewa haki, waende mahakamani. Sasa ni nani ana tamko la mwisho katika hili? Ni mawaziri, taasisi za serikali, vyombo vya dola ana Waziri Mkuu?

“Kama raia wa Tanzania, vyombo vya dola ni moja ya mategemeo yangu ya kunilinda mimi na mali zangu, kama raia wengine, lakini pamoja na kusakamwa na vyombo hivyo, nasema siogopi. Ulinzi wangu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, pili utatoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye naamini hatakubali kuona sitendewi haki, na tatu ulinzi wangu utatoka kwa Watanzania wanaochukia ufisadi, hasa masikini na wanyonge.

“Hawa hawana fedha nyingi, ama madaraka lakini wana nguvu ya sala na umoja bila kujali dini zao,” alisema Mengi na kushangiliwa kwa nguvu na waamini wa kanisa hilo.

Mengi alisisitiza kuwa, hatarudi nyuma katika msimamo wake wa kupiga vita ufisadi, kwani anaamini rushwa ikiachwa bila kukemewa, wananchi watagawanyika katika makundi mawili; la watu wenye kipato na madaraka na la watu masikini.

“Watanzania wenzangu wanaochukia umaskini, wanaochukia ufisadi, ndugu zangu waumini, nawaomba mniombee na tuimbe wimbo namba 59 katika kitabu cha ‘Mwimbieni Bwana’, usemao ‘Kazi ni yako Bwana’,” alisema.

Hatua ya Mengi kutoboa siri ya kusakamwa kwake mara baada ya kutaja majina ya aliowaita mafisadi papa, ilitokana na mahubiri ya Askofu Dk. Shao, aliyeunga mkono harakati zake katika vita dhidi ya ufisadi.
Askofu huyo alimtaka Mengi asikatishwe tamaa na wajanja wachache, ambao wamekusudia kurejesha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo.

“Taifa letu limegubikwa na mafisadi wachache, wapo Watanzania wenzetu kama Mengi, wamekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya kifisadi, lakini wanakwamishwa na baadhi ya viongozi walioko madarakani, tukemee kwa pamoja.

“Mwaka huu na mwaka ujao ni vipindi vya uchaguzi mbalimbali, kuna watu wamejaa choyo, wivu, chuki na ubinafsi miongoni mwetu, hakika watu hao ni wabaya kwa maendeleo ya taifa, msiwachague,” alisema.

Dk. Shao aliomba wananchi kutomchagua kiongozi asiye na ujasiri na uthubutu na kujitoa kwa ajili ya wengine.
Alisema, Mengi hataki urais wala hana nia ya kuwania kiti hicho, wala uongozi wa aina yoyote, lakini amejitoa kusaidia wanyonge, na rafiki zake ni masikini, walemavu, wajane, wanaoishi na virusi vya VVU pamoja na wenye matatizo mengine ya kijamii.

Mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo iliyodumu kwa zaidi ya saa sita, Mengi alitoa sh milioni 400 kwa ajili ya vikundi na miradi mbalimbali inayosimamiwa na kanisa hilo.

Kwanza alitoa sh milioni 100 kwa ajili ununuzi wa jengo linalotumika kama zahanati ya Ndeekyo, pia alitoa sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kisasa ya msingi ya Kisereny na sh milioni 100 kwa ajili ya Saccos ya Kisereny.

Pia alitoa sh milioni 100 kwa ajili ya kwaya ya kanisa hilo, akina mama wanaoishi na VVU, wajane na watoto yatima.

No comments:

Post a Comment