Busanda chambueni mchele na pumba
HARAKATI za kumtafuta mwakilishi wa wananchi yaani, Mbunge wa Jimbo la Busanda, zimepamba moto, macho ya wananchi yameelekezwa mkoani Mwanza, katika jimbo hilo.
Kila Mtanzania anataka kujua ukomavu na uelewa wa watu wa Busanda.
Uchaguzi huu utakuwa kipimo cha ukomavu na uelewa wa watu wa Busanda kutokana na hali ilivyo sasa.
Kwa sababu siku hizi unapoingia kwenye suala la uchaguzi siyo mchezo na si kama zamani wakati wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Siku hizi mpigaji kura ana kazi nzito kuliko anayechaguliwa, unapaswa kutumia busara za pekee na hekima katika kuamua nani akuwakilishe, ukiweka pembeni urafiki, uhusiano na undugu kati yako na mtu anayekuomba kura.
Suala la kumtuma mtu bungeni siku hizi ni la msingi sana kuliko ilivyokuwa zamani ambapo, watu wengi walikuwa na maadili, wakweli na wazalendo.
Siku hizi mtu anakuja kuonekana kijijini, wakati anapotaka madaraka, anataka kupewa nafasi akaishi Dar es Salaam.
Ukimuona mgombea anakupigia magoti ujue atakuja kukunyanyasa ili nawe umpigie magoti ukimwomba akusaidie.
Ninataka wananchi wa Busanda waamini kuwa maisha yao yatazidi kuharibika kama watakubali kuchagua mtu kwa kuangalia urafiki wake au mahusiano nje ya vitu nilivyovieleza hapo juu.
Uzalendo na uadilifu wa mtu binafsi na chama chake kinachomtuma unatakiwa kuangaliwa kwa makini ili kupata wabunge wasafi watakaomsaidia Spika wa Bunge, Samuel Sitta, wabunge wa upinzani na wachache wa CCM wenye uzalendo, ili kupigana na mafisadi waliokithiri kila kona ya nchi hii.
Watanzania wa Busanda, vita ya ufisadi ni ngumu, mafisadi ni wengi na wana nguvu, watawapa pesa nyingi ili mumchague mtu wanayeamini kuwa akiingia bungeni atawapigia makofi na kuwashangilia mafisadi wakati wanapoiba.
Kwa hiyo mkikubali na kumuingiza mtu anayewapenda mafisadi, maisha yenu ya miaka mitano au kumi yatakuwa ya mateso, kunyanyasika na hata kufa kwa kukosa huduma.
Lazima tuzionee huruma rasimali zetu zinavyoibiwa na hili kundi la wachache.
Wananchi wa Busanda, mnapaswa kuwasikiliza wagombea wa CHADEMA, CCM, UDP na CUF, na kuamua nani anakidhi viwango na anastahili kuwawakilisha, lakini mjue wakati huu tunahitaji mabadiliko ambayo mapinduzi yake hayaji kwa ngumi au kutumia silaha tu bali njia rahisi kabisa ni kupiga kura.
Hapo ndipo tutakapowapima uwezo wenu wa kuamua, tutaona kama Wanabusanda mnamacho na mnaona yanayotokea katika taifa hili.
Tutajua kama kweli mnatuunga mkono waandishi wa habari tunaotumia nguvu zetu, usiku na mchana kuandika na kupigana na kundi hili.
Angalieni utajiri uliopo Busanda, husasan Wilaya ya Geita na hata mkoa mzima wa Mwanza, rasimali zenu zinazidi mikoa mingine lakini hakuna maendeleo, miundombinu ni mibovu, hakuna umeme, barabara na hata maji ya kunywa ni shida wakati mnaishi kwenye Ziwa Victoria lenye maji lukuki.
Hakuna mtu anayejitoa kuwasaidia na kuwatetea ili mpate mabomba ya kuvuta maji hapo ziwani, hakuna anayewajali, tumieni akili sana kwa hili.
Tunalia nanyi kwa sababu mbunge mnayemchagua siyo wa Busanda pekee, kwani Mbunge anapokuwa kwenye jengo la Bunge ni kwa manufaa ya Watanzania wote kwani kama atakuwa fisadi, atawatesa Watanzania wote wanaokadiriwa kufikia milioni 40.
Tuangalie miswada isiyo na maslahi kwa taifa inavyopitishwa bungeni kiurahisi kutokana na kukosa wabunge wenye uzalendo, tuangalie makofi na pongezi zinavyotolewa na wabunge kwa kitu ambacho ni ufisadi mtupu.
Tuangalie baadhi ya wabunge wanavyojenga hoja na kutetea nyaraka za kifisadi au zinazotumika kuliibia taifa mabilioni ya fedha sizinaswe na vyombo vya habari au mtu yeyote kwa kigezo kuwa ni za siri.
Hapo Busanda, mtakuwa na kazi ya kutusaidia Watanzania wote kutuletea mbunge safi, ambaye mna uhakika atachukia ufisadi na hataunga mkono miswada na kutetea ufisadi bungeni.
Tunataka mbunge atayesimama na kujitoa mhanga, kwa ajili ya taifa zima, asimame awataje mafisadi waliosalia, chama chake kimuunge mkono, kimpe nguvu na siyo akipinga ufisadi chama kimtenge.
Hatuhitaji mtu anayepiga magoti kutuomba kura, tunataka mtu ajenge hoja atuambie anakwenda kufanya nini tukimpa nafasi, atuambie atawezaje kutetea wananchi wakati chama chake kinataka maslahi ya mafisadi yalindwe?
Mgombea huyo atuambie chama chake kama kinafadhiliwa na mafisadi, yeye atawezaje kukwepa kutimiza matakwa yao wakati watakapokuwa wanapitisha mikataba ya wizi.
Ni matumanini ya Watanzania kuwa wananchi wa Busanda, mtawafurahisha Watanzania wote kwa kuwaletea mtu safi na kuonyesha Mapinduzi ya kweli kama walivyofanya wananchi wa Tarime
Elimu ni kujifunza! Tunajifunza kwa kusoma! Karibu katika Blog hii ili tufundishane na kubadilishana Mawazo
Popular Posts
-
*alikubali kushindwa kwa siasa za Kijamaa *hakujilimbikizia mali Na Deogratius Temba WAKATI taifa linaadhimisha miaka 10 ya kifo cha mwasisi...
-
Na Deogratius Temba KWARESMA ni kipindi cha mfungo kwa waumini Wakatoliki. Mfungo huu ni wa siku hamsini. Kipindi hiki kinaanza na ibada ya ...
-
KAMPALA Uganda Dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ARVs, zikitumika sambasamba na dawa mseto aina ya (co-Trimoxazole), ...
-
Na Deogratius Temba. NI takribani miaka mitano tangu ililipo ibuika suala la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua sh. Bilioni ...
-
*Ilizamishwa ziwani na wakaoloni baadaye ikafufuka *Ina Umri wa miaka 98, mwaka 2013 itavunja rekodi ya dunia Na Deogratius Temba MV Liemba ...
-
Na Deogratius Temba SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigambo...
-
*Ni ajali iliyoweka historia kwa kuua *Bado usalama wa ziwani haujaimarika Na Deogratius Temba MEI 21, mwaka huu taifa limetimiza miaka 14 ...
-
, tutaendanayo mpaka uchaguzi Mkuu 2010 Na Deogratius Temba MWISHONI mwa wiki iliyopita Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha mapinduzi, (CCM), w...
-
TITLE OF THE PROJECT The effect of Water Conflict between Investor of VASSO Estate and Villagers in Kibosho Dakau, Moshi Kilimanjaro JOURNAL...
-
Taasisi ya mafunzo ya Jinsia (GTI) inayomilikiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) inaendelea na mafunzo ya kuwanoa wanaharakati kuanzia ...
No comments:
Post a Comment