Tamasha la Jinsia litujenge kudai haki ya kumiliki ardhi na demokrasia shirikishi
Na Deogratius Temba
ARDHI ni rasilimali na muhimili muhimu katika maisha ya wanadamu. Ardhi ya Tanzania ni mali yetu na ni lazima tuilinde na kuipigania. Kama kuna changamoto kubwa kwa jamii ya kitanzania katika kipindi hiki cha mfumo wa soko huria na kukua kwa utandawazi ni kukosekana kabisa kwa haki ya raia ya kumiliki ardhi, kuongezeka kwa migogoro ya ardhi ambayo ni matokeo ya kukua kwa soko huria.
Kilio kikubwa sasa ni uporaji wa ardhi kutokana na kuongezeka kwa kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo.
Uporaji wa ardhi ni adui wa usawa wa kijinsia, soko huria halina huruma wala ubindamu lengo lake ni kuongeza faida na mali. Sheria za ardhi tulizojitungia zimetamka bayana usawa wa kijinsia lakini hatuzifuati kutokana na kusukumwa na mfumo huu kandamizi.
Sheria zimeeleza wazi juu ya ugawaji wa ardhi na haki ya kila binadamu bila kubagua. Sheria hizi ni kama :Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya 1999. Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi namba 2 ya 2002, na Marekebisho ya sheria ya Ardhi namba 2 ya 2004.
Sheria nyingine muhimu ni Sheria ya Mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi ilipitishwa mwaka 2002 na kuanza kutumika rasmi mwezi Oktoba 2003.
Pamoja na changamoto ya udhaifu wa sheria hizi, ambazo baadhi ya vipengele havimpi fursa mwananchi masikini hasa yule aliyeko pembezoni.
Ni lazima tukuabali na kuamini kuwa raia wote wanawake na wanaume wana haki sawa ya kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi. Milki za ardhi zilizopo ikiwa ni pamoja na milki za kimila zinatambuliwa na kulindwa kisheria bila kubagua jinsia.
Ardhi itumike kwa manufaa yanayozingatia maendeleo endelevu, fidia kamili na ya haki ilipwe kwa mmilika bila kuchelewa pale ardhi yake serikali ina poitwaa kwa manufaa ya umma, na manufaa ya umma yasiwe ni kumpa mwekezaji bali ni huduma za kajamii ambazo zitamnufaisha mwananchi masikini anayeishi katika eneo husika.
Serikali inapaswa kuweka mfumo bora wa utawala na usimamizi wa ardhi ambao unawawezesha wananchi kushiriki katika kufanya maamuzi kuhusu masuala ya ardhi wanayokalia au kutumia.
Sheria hizi zinatamka bayana kuwa mwanamke ana haki sawa na mwanaume katika kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi. Kifungu 3(2) cha sheria ya ardhi na sheria ya ardhi ya vijiji za 1999. Leo hii taifa linakumbwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi ambapo tumefikia hatua ya uvunjifu wa amani na hadi umwagaji damu na pengine vifo kutokea katika maeneo kadhaa.
Hali hii imeondoa utamaduni wetu wa asili wa kuvumiliana na kumaliza matatizo yetu kwa njia mwafaka za mazungumzo. Ni muhimu serikali ikaelewa kwamba kupuuza migogoro hii ya ardhi nchini ni sawa na kuatamia bomu, hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe!
Migogoro, hasa ya wananchi na wawekezaji inakua kwa kasi na kuchukua sura mpya. Anapokuja ‘mgeni’, kwa jina la ‘Mwekezaji’ matendo ya Serikali yetu, yanapingana na usemi usemao ‘mgeni njoo mwenyeji apone’ bali imekuwa ‘mgeni njoo mwenyeji asulubike’ .tunahitaji umakini mkubwa katika kusimamia rasilimali ardhi bila kubagua na kuwanyanyasa wananchi wazawa.
Migogoro huu imesababishwa na tatizo kuwa la kukosekana kwa demokrasia shirikishi ambayo inampa kila mwananchi, mwanajamii fursa ya kuhoji, kuuliza na kusema juu ya rasilimali zinazomzunguka.
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mtandao wa mashirika watetezi wa haki za binadamu,usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake nchini (FemAct) na washirika wengine, wanaandaa Tamasha la Jinsia litalofanyika mwezi huu wa Septemba katika viwanja vya TGNP Mabibo Dar es salaam.
Mratibu wa tamasha hilo, Eluka Kibona, anasema kuwa tamasha hilo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 13 hadi 16 mwaka huu.
Malengo ya tamasha hilo la kumi ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili kuwa ni kuibua, kubadilishana na kuanzisha fikra, uchambuzi wa kutengeneza mikakati ya pamoja ya kudai rasilimali ziwanufaishe wanawake, wanaume na vijana walioko pembezoni.
Kusherekea nguvu zetu za pamoja, kupanua na kuimarisha ushirikiano katika vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi na haki ya uchumi katika ngazi ya sekta zote za kijamii na mengineyo.
Muktadha wa tamasha la mwaka huu kwa mujibu wa FemAct ni kulenga kwenye matamasha ya awali na kujikita katika kuendeleza kampeni kubwa ya haki ya uchumi: ‘Rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni’.
Pia ni kuimarisha mapambano dhidi ya mfumo dume, sera za kibeberu na mifumo ya utandawazi wakati huu muafaka wa uundaji wa katiba mpya na kusherehekea mika 50 baada ya uhuru wa Tanzania.
Mada kuu ya tamasha ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Ajira na Maisha Endelevu. Lakini vile vile kutakuwa na mada ndogo zitakazotolewa kila siku. Na washiriki ni watu binafsi,vikundi,mashirika,taasisi mbalimbali na mitandao iliyoko katika mapambano yanafanana.
Kupitia tamasha hili, sote tutapata fursa ya kukaa pamoja na kudajali changamoto za ardhi, maji, masoko, biashara, ajira, na demokrasia katika taifa letu. Uchambuzi huu utatuapa nafasi ya kupaaza sauti zetu na kudai kile tulichoporwa. Tuungane pamoja!!
Elimu ni kujifunza! Tunajifunza kwa kusoma! Karibu katika Blog hii ili tufundishane na kubadilishana Mawazo
Popular Posts
-
*alikubali kushindwa kwa siasa za Kijamaa *hakujilimbikizia mali Na Deogratius Temba WAKATI taifa linaadhimisha miaka 10 ya kifo cha mwasisi...
-
Na Deogratius Temba KWARESMA ni kipindi cha mfungo kwa waumini Wakatoliki. Mfungo huu ni wa siku hamsini. Kipindi hiki kinaanza na ibada ya ...
-
KAMPALA Uganda Dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ARVs, zikitumika sambasamba na dawa mseto aina ya (co-Trimoxazole), ...
-
Na Deogratius Temba. NI takribani miaka mitano tangu ililipo ibuika suala la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua sh. Bilioni ...
-
*Ilizamishwa ziwani na wakaoloni baadaye ikafufuka *Ina Umri wa miaka 98, mwaka 2013 itavunja rekodi ya dunia Na Deogratius Temba MV Liemba ...
-
Na Deogratius Temba SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigambo...
-
*Ni ajali iliyoweka historia kwa kuua *Bado usalama wa ziwani haujaimarika Na Deogratius Temba MEI 21, mwaka huu taifa limetimiza miaka 14 ...
-
, tutaendanayo mpaka uchaguzi Mkuu 2010 Na Deogratius Temba MWISHONI mwa wiki iliyopita Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha mapinduzi, (CCM), w...
-
TITLE OF THE PROJECT The effect of Water Conflict between Investor of VASSO Estate and Villagers in Kibosho Dakau, Moshi Kilimanjaro JOURNAL...
-
Taasisi ya mafunzo ya Jinsia (GTI) inayomilikiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) inaendelea na mafunzo ya kuwanoa wanaharakati kuanzia ...
No comments:
Post a Comment