Popular Posts

Friday, January 14, 2011

Udhaifu wa katiba,ukosefu wa maadili umelifikisha taifa hapa lilipo

Na Deogratius Temba
LIPO jambo moja ambalo limetufanya leo tuwe hapa tulipo katika hali tuliyonayo ambayo kwa wengine ni furaha lakini idadi kubwa ni huzuni na manung’uniko kila kukicha.
Wengi wetu tunajua, hali ya hali ya watanzania walio wengi, ni masikini, hawana uhakika wa kuendelea kuishi, njaa, maradhi vimekuwa ndio kila kitu. Watu wanapumua kwa shida kwasababu hawajui kesho itakuweje. Hii ndiyo Tanzania.
Mwenye nanchi anazidi kuongezewa, asiyenanchi ananyang’anywa hata kile alichonancho, chakula cha kutosha, matibabu mazuri, elimu nzuri, maji ya kunywa, barabara za kupita zimebaki ni haki ya wateule wachache huku mamilioni ya watanzania wakibakia wakiwa. Hili linaendelea ikiwa ni baada ya miaka 50 ya uhuru.
Ukosefu wa maadili na utawala bora, ambao kwa namna moja au nyingine sasa tunalazimika kuamini kuwa unatokana na mapungufu makubwa yaliyoko kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano yametusababishia aibu kubwa katika taifa letu. Hii ndiyo sababu ya kuongezeka kwa umasikini badala ya kupungua, ndio sababu ya kupotea kwa maadili, watawala hawabanwi na katiba wanashangalia na wanaipenda.
Tumeingia kwenye wimbi chafu la ulimwengu wa aibu uliokithiri vitendo vya rushwa, ufisadi, wizi wa wazi kwa watawala wetu kutokuona aibu pindi wanapoona rasimali za Taifa zikiibiwa na kupokwa na wachache.
Tumeona aibu ya ushirikina, mauaji ya albino, mapigano ya koo, mtu na mtu, ndugu na ndugu, wazazi na watoto wao, ujambazi na mengine ambayo hayafai kuyazungumzia katika jamii iliyostaarabika.
Baya zaidi na la aibu ambalo linalichafua Taifa letu ni jinsi ambavyo katiba tuliyonayo inavyoshindwa kutoa mwanya wa kidemokrasia kwa wananchi. Hakuna haki ya kidemokrasia tena wenye dola wanatumia madaraka na nguvu zao kung’ang’ania madarakani, Chama kinalazimisha ushindi, walioko madarakani wanaiba kura waziwazi na mfumo wa katiba unawalinda. Hii ni aibu, ni hatari na ni ukosefu wa maadili.
Yanayotokea tunayaona, tunayasikia, ya Arusha wiki hii ni mwendelezo tu kwani mengi tuliyaona makubwa zaidi wakati za zoezi la kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika oktoba 2010, bila mabadiliko ya katiba tena katiba itakayobadilishwa chini ya tume huru itakayoundwa na Bunge ni kazi bure.
Taifa hili linapita katika mfumo wa uongozi wa aina yake, ambao umekuwa mzigo kutokana na yale yanayofanyika ambayo mengine yanapoteza ubinadamu wetu, na undugu tuliouweka siku ya Azimio la Arusha Februari 5, 1967.
Ahadi mojawapo ya chama cha Tanganyika African National Union (Tanu), isemayo, “ Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja” iliridhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka 1967, chama cha Tanu kilitoa Maadili ya Viongozi ambayo wananchi wote waliamini kuwa zingeliwasaidia na kuzuia wimbi la wezi au wanyanganyi, kuingia ndani ya chama hicho ili baadaye waingie serikalini kwa lengo la kuivuruga serikali na chama; hiyo ilikuwa ndoto ya hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa sababu aliona maono ya kweli na akajua kuchukua tahadhari mapema kabla ya maafa.
Miaka 11 baada ya kifo cha Nyerere, hakuna mtu anayetaka au anayedhubutu kuyakumbuka maadili ya TANU, sasa yamegeuka shubiri kwao, wanataka kuiba tu. Wazawa wamegeuka kuwa mabeberu mamboleo, wanachuma kwa hasira ya ajabu.
Kanuni za maadili zilizowekwa na TANU na ASP, wakati huo zilikuwa ngumu na zenye msimamo wa kukataza na kuonya; zilimlenga zaidi kiongozi ili akue katika maadili na kanuni lakini pia ziliainisha adhabu kwa yeyote ambaye angelikwenda kinyume.
Lengo kubwa la Mwalimu na wenzake kutengeneza maadili hayo ndani ya Chama na Serikali, ilikuwa kuwaepusha viongozi wa serikali kujikusanyia mali kwa maslahi binafsi au kuwakusanyia ndugu zao mali kutoka katika ofisi walizokuwa wakizisimamia.
Kwa maneno mengine zilikuwa na nia ya kuwezesha au kuwafanya viongozi wachague kitu kimoja, kuwa viongozi wa umma, au biashara, yaani kujitafutia fedha kwa maslahi binafsi na familia zao.
Lakini hapo sipo tulipo, tumefika mbali, tuliyavunja na sasa tunashindwa kurudi katika mstari sahihi, tukiwataka wataje mali zao leo hawapo tayari, wanatukana na kusema, “Watu hawana adabu kwa viongozi wao wastaafu! Mara “…..watu wana wivu wa kike!” yote haya ni maneno ya kutaka kuwakatisha tamaa wananchi wazalendo wenye nia ya kupigania rasimali za Taifa.
Kwa hakika mipango ya Mwalimu Nyerere ilikuwa changamoto kubwa kwa viongozi wa serikali wakati ule, na hata waliokuwa ndani ya Chama, pamoja na kwamba Mwalimu alikorofishana na wenzake ndani ya TANU kutokana na sera zake hizo.
Hizi ndizo dalili za wazi kuwa tumekosa maadili, tumekosa viongozi na sasa nafasi za viongozi zipo wazi, kuna haja ya kutangaza nafasi mpya za kazi, ili tuwapate wenye sifa.
Ninaposema hatuna viongozi nina maana kuwa kuna ombwe kwenye uongozi unaotegemewa katika taifa hili watu wanapwaya, hawafiti kwenye nafasi hizo, sasa tuna jukumu la kutafuta viongozi.
Tukianza mchakato wa katiba mpya uende sambamba na kuwatafuta viongozi wa taifa hili, tujaze ombwe hili, ili taifa lisonge mbele, la sivyo tutaishia kubaki tunapiga kelele huku wenezetu wanasonga mbele.
deojkt@yahoo.com;0715686575

No comments:

Post a Comment