Popular Posts

Wednesday, May 26, 2010

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010

Makundi CCM yawatisha Membe,Chikawe
Na Mwandishi Wetu
Mawaziri wawili Bernadi Membe, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mathias Chikawe, Katiba na Sheria, wamewataka wananchi kutokukubali kujiingiza katika makundi ya kisiasa yaliyozuka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Wakihutubia zaidi ya wajumbe 800 wa Mkutano Mkuu wa Jimbo kutoka kata 27 za jimbo la Nachingwea, Mkaoni Lindi, Mawaziri hao, wamesema kila mwaka wa uchaguzi huibuka makundi ambayo ni hatari kwa afya ya CCM.
Membe ni mara yake ya pili kutoa kauli kama hiyo ya kuonyesha kutishwa na makundi ya uchaguzi. mara ya kwanza alitamka hivyo Disemba 8, 2008, katika Ukumbi wa Karimjee alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nawasihi muwe kitu kimoja. Msiwe mandumilakuwili wenye ndimi mbili, kwa huyu unasema nipo nawe na kwa yule unasema tupo pamoja, epukeni kujiingiza katika makundi haya,” amesema Membe.
Akisisitiza kuepuka makundi cha ndani ya chama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi Mzee Alli Mtopa, amesema kila mwaka wa uchaguzi huibuka makundi ambayo ni hatari kwa chama hicho kikongwe.
“Kila mwaka ukiingia uchaguzi, ni mwaka wa hatari, mwaka wa kusengenyana, kugombana, kujigawa…kwa sababu ya uroho wa madaraka. Kiongozi anayetugawa mzomeeni,” amesema Mtopa
“Mkihitalifiana kwa siasa tu mtachekwa kwasababu mtakuwa mkiwapa watu wengine faida, makundi yanasababisha kupatikana kwa viongozi wasio na sifa. …..” ameonya Mwenyekiti huyo.
Mzee Mtopa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, amewataka pia wanaCCM kupanga mikakati ya ushindi wa kishindo katika nafasi za Urais, Ubunge na Madiwani.
“Tofauti na zamani, sasa mkutano mkuu wa jimbo ni wa kupeana mikakati, sio kuchagua mgombea. Kupiga kura ni huko chini kwa wananchama…mpange mikakati ya ushindi,” amesema Mzee Mtopa.
Naye Chikawe amesema utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha ubunge wake umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuwataka wajumbe hao kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatakana katika kipindi cha miaka takribani mitano iliyopita ili CCM ishinde tena kwa kishindo.
“Nimewapa kijitabu kinachoeleza tumetekelezaje ilani ya CCM. Tuwaeleze wananchi na sina shaka tutashinda kwa kishindo kikubwa,” amesema Chikawe ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia mkoa wa Lindi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment