Popular Posts

Monday, February 8, 2010

DPP watumie ushahidi wa BAE mahakamani- Profesa Safari

Na Deogratius Temba
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini, Eliezer Feleshi, ametakiwa kutumia maelezo ya Kampuni ya British Aerospace Systems (BAE Systems) ya Uingereza, ya kukiri kufanya makosa kuwashtaki Watanzania walioishiriki katika mchakato wa kununua rada mbovu.

Kampuni ya BAE inatuhumiwa kwa kuiuzia Tanzania rada mbovu ya kuendeshea shughuli za kijeshi, mwaka 2002, yenye dhamani ya zaidi ya pauni 28 milioni.

Hadi sasa Watanzania wanaotajwa kuhusika katika ununuzi huo, ni aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati huo, Andrew Chenge, Gavana wa Benki Kuu, Dk. Idris Rashid na mfanyabiashara sanayedaiwa kuwa dalali wa rada Sailesh Vithlan, ambaye bado anatafutwa na polisi wa Tanzania na wale wa Kimataifa (Interpool).

Akizungumza jana na Tanzania Daima, katika mahojiano Maalumu ofisini kwake, Mwanasheria maarufu Profesa Abdallah Safari, alisema kitendo cha BAE kukiri kuwa imefanya makosa hata ni ya kimahesabu imeonyesha kuwa kulikuwepo na udanganyifu na DPP anatakiwa kutumia ushahidi huo kuwakamata wahusika na kuwafikisha mahakamani.

“BAE kukubali tu ni ushahidi na DPP analijua hilo, hatuhitaji kuendelea kupoteza muda katika uchunguzi wa suala hili, wanaotajwa wameshajatwa katika taarifa za Uingereza mara kadhaa. DPP anapaswa sasa kutumia uwezo wake kuwapeleka wahusika mahakamani,” alisema.

Alisema watu wote waliotajwa kuwa wamehusika katika kuliingizia taifa hasara kupitia ununuzi wa kifaa hicho wanapaswa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka, kwani hawezi kukwepa tena.

Alisema DPP anatakiwa kwenda mahakamani kwani viashiria vingine ni kama vile vya Chenge kuhusika na umiliki wa fedha nyingi, katika visiwa vya Jersrey, Uingereza ambapo hazielezeki alikozopata hadi leo.

“ Kama ningekuwa mimi ndiye DPP, huu ungekuwa ushaidi mkubwa sana wa kunifanya nishinde kesi hii. BAE inapokiri kufanya makosa walioshiriki nayo makosa wanatakiwa kukamatwa hakuna njia nyingine,” alisema

Aliongeza kuwa BAE ni mkosaji mkuu, lakini kuna washiriki wa tukio, hao wanatakiwa kuwajibika. Na ikiwezekana rais Kikwete awakamate kwasababu amekuwa akikiri mara nyingi kuwa wakati ukifika atawakamata wahusika.

Profesa Safari alizidi kueleza kuwa mara nyingi amekuwa akishangaa kitendo cha serikali kuwashtaki watuhumiwa wenye kesi kubwa za uhujumu uchumi, katika mahakama ndogo zenye adhi ya kiwilaya, wakati sheria inazitaka zipelekwe mahakama kuu na dhamana yake isimamiwe na mhakama hiyo.

Aliitaja sheria inayopaswa kutumia ambayo imekuwa haitumiki katika kuwashtaki watuhumiwa wa ufisadi kuwa ni namba 13 ya uhujumu uchumi ya mwaka 1984.
Sakata hili la rada limeibuka tena baada ya ofisi ya serikali ya Uingereza ya Serious Fraud Office (SFO) kuibana BAE na kukubali kulipa kifuta machozi kwa Tanzania Sh 37.8 bilioni kati ya Sh 60 bilioni, zilizonunulia rada hiyo ya kijeshi mwaka 2002.

Hatua ya BAE System kuuza rada hiyo kuukuu kwa Tanzania iliwahi kuikoroga serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair na kumfanya Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa Clare Short kujiuzulu na marehemu Robin Cook, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje baada ya kumshambulia waziri mkuu huyo, hadharani.

Rais Jakaya Kikwete, amewahi kunukuliwa akisema wataiomba serikali ya Uingereza kuangalia namna ya kurejesha sehemu ya fedha hizo za rada ambayo ilinunuliwa na mtangulizi wake Benjamin Mkapa.

Ijumaa wiki iliyopita, BAE ilipigwa faini ya zaidi ya Sh 400 bilioni kutokana hesabu zake za mauzo kujaa utata.

Mpango wa ununuzi wa rada hiyo ya Sh 52 bilioni ulianza mwaka 1999, lakini ukazua mjadala ambao uliingia hadi kwenye Bunge la Uingereza mwaka 2002 wakati lilipohoji nchi maskini kama Tanzania kununua chombo chenye thamani kubwa kiasi hicho na kuhisi kuwepo kwa ufisadi.
mwisho

No comments:

Post a Comment