SERIKALI imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu mkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) na Richmond, ikieleza kuonywa kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Edward Hosea kutokana na kutokuwa na umakini wa kutosha wakati taasisi yake ilipofanya uchunguzi wa mchakato wa mkataba huo.
Taarifa hiyo kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo uliwasilishwa jana bungeni kwa niaba ya serikali na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima.
Pamoja na Hosea mwingine aliyeonywa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Wataalam, Singi Madata.
Alisema Hosea alionywa kutokana na mamlaka yake ya nidhamu kuona kuwa sheria ya Takukuru kwa wakati huo ilikuwa na mapungufu katika kubaini viashiria vya rushwa kwenye mchakato wa zabuni ambavyo ndiyo wataalamu wa Takukuru walijikita kufanya uchunguzi wao.
“Hata hivyo ingawa sheria ilikuwa na mapungufu kwa upande mmoja, Mamlaka yake ya nidhamu imebaini kuwa wakati wa kupitia taarifa ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wake wa Takukuru na kabla ya kuitoa kwa Umma, alipaswa kujiridhisha kwamba kweli Kampuni ya Richmond Development Company LLC ilikuwa imeandikishwa hapa nchini au hapana”, ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa serikali taarifa ya Hosea haikuonyesha bayana tofauti baina ya Makampuni ya Richmond Development Company(LLC), RDEVO na Richmond Development Development Company(RDC) jambo ambalo lilijitokeza baadaye wakati Kamati Teule ya bunge ilipofanya uchunguzi wake.
“Mamlaka imeamua apewe onyo kwa kutokuwa makini katika uchambuzi wa taarifa zinazowasilishwa kwake na wataalamu wake, ili kuleta usimamizi wenye tija ndani ya Takukuru”, ilisema serikali.
Kuhusu Madata, serikali imesema katika utetezi wake, Mamlaka yake imeona kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya kazi waliyopewa ya kusaili makampuni nane yalioomba zabuni ya kufua umeme wa dharura alieleza kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa muda wa siku mbili.
“Pamoja na utetezi wake mamlaka yake ya nidhamu imeona kuwa muda huo ni mfupi na usingeewezesha kamati husika kukamilisha kazi hiyo kwa umakini na ufanisi, pamoja na kuwepo kwa hali ya dharura ya upungufu wa umeme nchini
Hata hivyo hapakuonekana dalili za mazingira ya rushwa wakati wa kufanya kazi hiyo hivyo mamlaka yake ya nidhamu imetoa onyo kwake kwa kutokuwa mwangalifu katika eneo hilo ”. Ilieleza taarifa hiyo.
“Kuhusu Mwanasheria Mkuu wa serikali ambaye Mamlaka yake ya nidhamu ni mheshimiwa Rais, kwa maelezo tuliyonayo ni kuwa hakuna kosa lolote la kisheria au kinidhamu ambalo alilifanya katika nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu wa serikali katika mchakato mzima ulioipa ushindi kampuni ya Richmond Development Company, LLC katika zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura
Kwa ujumla hadi sasa uchunguzi wa vyombo vya dola kuhusu watumishi wote wa umma waliohusika na suala hili, unaonyesha kuwa hakuna mtumishi yeyote aliyeonekana kutenda kosa la jinai lenye kuhitaji kuchukuliwa hatua za kisheria
Hata hivyo kwa kuwa yapo mashauri mbalimbali yanayoendelea mahakamani dhidi ya wamiliki na wawakilishi wa kampuni ya Richomond, iwapo mtumishi yeyote wa umma atatajwa na watuhumiwa hao kwamba alihusika katika makosa ya Jinai, serikali haitasita kumfikisha mahakamani”, ilisema taarifa hiyo ya serikali.
Katika maazimio ya bunge yaliitaka serikali kuwawajibisha watumishi wote wa umma waliohusika katika madajiliano ya mchakato mzima wa mkataba wa baina ya Tanesco na Richmond pamoja na wa Takukuru waliofanya uchunguzi wa suala hilo .
Kuhusu watumishi wa umma waliohusika katika majadiliano ya mchakato mzima wa makataba huo, serikali imewawajibisha watendaji wake wakiwemo maofisa waandamizi ambao ni Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, walifunguliwa mashataka ya nidhamu kwa mujibu wa kanuni namna 49(1) ya sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2002.
Serikali iliongeza kuwa vilevile watumishi waliofanya uchunguzi kuhusu suala hilo walifunguliwa mashtaka ya nidamu kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2002 na kuwa watumishi hao waliwasilisha utetezi wao kwa mamlaka zao za nidhamu.
Kuhusu azimio namba nane na 14 ya bunge kutaka serikali kuwawajibisha viongozi wenye dhamana ya kisiasa waliokuwa Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, taarifa hiyo ilisema kama ilivyoelezwa katika mkutano wa 18 wa bunge kwamba vyombo vya dola vimekuwa vinaendelea na uchunguzi wake kuhusu suala hilo hadi sasa suala hilo halijafikia tamati kwa kuwa linashughulikiwa zaidi na taasisi ya Takukuru pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashkata Nchini, DPP.
Kwa upande wa azimio namba 11 kuhusu sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995(The Public Leadership Code of Ethics Act) kufanyiwa marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa viongozi waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani jambi ambalo lina mgongano wa kimaslai
Na kuwa serikali ianze rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hilo ndani na nje ya bunge kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali, serikali ilibainisha kuwa kikundi kazi kilichoundwa na serikali kushughulikia azimio hili kimefanya utafiti na kupitia upya sheria ya maadili ya viongozi wa umma kubaini upungufu uliopo na kuainisha mapendekezo yatakayowasilishwa serikalini.
“Hivi sasa kikundi kazi kimeanza zoezi la kuandaa mapendekezo ya kurekebisha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995, kwa madhumuni ya kuwezesha viongozi na watendaji waandamizi kutenganisha shughuli za biashara na uongozi wa umma. Zoezi hili likikamilika mapendekezo ya kikundi kazi yatawasilishwa serikalini kwa uamuzi hatimaye muswada wa sheria husika kuwasilishwa bungeni”.
Kuhusu azimio namba tatu kutaka mikataba kati ya Tanesco na Richmond , LLC uliorithiwa na Dowans Holdings S.A) na ile kati ya Tanesco na IPTL, Songas, Aggreko na Alstom Power Rentals ipitie upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo mikataba ya madini ilivyopitiwa upya na serikali
Na kuwa bila kufanya hivyo mzigo mkubwa wa gharama za umeme utawaelemea wananchi na kushindwa kufikia azma ya serikali ya maisha bora kwa kila mtanzania, serikali ilitaka hatua ilizochukua na kusema kuwa kama alivyoeleza waziri mkuu katika mkutano wa bunge wa 15 mikataba baina ya Tanesco na Aggreko na Alstom Power Rentals, muda wa mikataba hiyo ulikwisha mwaka 2008 na serikali kupitia Tanesco ilikataa kuongeza muda wa mikataba hiyo.
“Kwa upande wa mikataba baina ya Tanesco na IPTL na Richmond Development Company ulioathiriwa na Dowans Holdings S.A, mikataba hii bado ina mashauri mbalimbali ambayo yapo mahakamani, kwa kuwa kanuni ya bunge na 64(1) (c) inazuia bunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama, taarifa ya serikali kunusu mikataba hii itatolewa baada ya Mashauri hayo kukamilika”, ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa serikali kuhusu azimio la bunge kutaka wamiliki wa Richmond LLC na Richmond Development Company(T) ltd, walifunguliwa kesi ya jinai mara moja kwa udanganyifu na ujanja wa serikali, ilieleza kuwa iliunda kamati maalumu ya vyombo vya dola ili kushughulikia uchunguzi na upelelezi kuhusiana na maazimio hayo mawili.
Pamoja na hilo ilieleza kuwa vyombo vya dola pia vilikamilisha upelelezi wa ndani wa suala hilo na kuwa hatua hiyo iliwezesha mmoja wa Wawakilishi wa kampuni ya LLC, Naeem Adam Gire kufikishwa mahakamani Kisutu, Dar es Salaam Januari 13 mwaka huu na kusomewa mashtaka matano ya makosa ya jinai na kuwa bado upelelelezi zaidi wa shauri hilo unaendelea nje ya nchi kwa kushirikiana na vyombo vya dola vya kimataifa.
MWISHO
Elimu ni kujifunza! Tunajifunza kwa kusoma! Karibu katika Blog hii ili tufundishane na kubadilishana Mawazo
Popular Posts
-
*alikubali kushindwa kwa siasa za Kijamaa *hakujilimbikizia mali Na Deogratius Temba WAKATI taifa linaadhimisha miaka 10 ya kifo cha mwasisi...
-
Na Deogratius Temba KWARESMA ni kipindi cha mfungo kwa waumini Wakatoliki. Mfungo huu ni wa siku hamsini. Kipindi hiki kinaanza na ibada ya ...
-
KAMPALA Uganda Dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ARVs, zikitumika sambasamba na dawa mseto aina ya (co-Trimoxazole), ...
-
Na Deogratius Temba. NI takribani miaka mitano tangu ililipo ibuika suala la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua sh. Bilioni ...
-
*Ilizamishwa ziwani na wakaoloni baadaye ikafufuka *Ina Umri wa miaka 98, mwaka 2013 itavunja rekodi ya dunia Na Deogratius Temba MV Liemba ...
-
Na Deogratius Temba SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigambo...
-
*Ni ajali iliyoweka historia kwa kuua *Bado usalama wa ziwani haujaimarika Na Deogratius Temba MEI 21, mwaka huu taifa limetimiza miaka 14 ...
-
, tutaendanayo mpaka uchaguzi Mkuu 2010 Na Deogratius Temba MWISHONI mwa wiki iliyopita Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha mapinduzi, (CCM), w...
-
TITLE OF THE PROJECT The effect of Water Conflict between Investor of VASSO Estate and Villagers in Kibosho Dakau, Moshi Kilimanjaro JOURNAL...
-
Taasisi ya mafunzo ya Jinsia (GTI) inayomilikiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) inaendelea na mafunzo ya kuwanoa wanaharakati kuanzia ...
No comments:
Post a Comment