Serikali inakwamisha kukua kwa elimu nchini
DHANA ya elimu bora ipo kwenye akili za watu wengi. Wadau wa sekta hiyo, yaani mzazi, mlezi, mwanafunzi na mwalimu ndilo lengo lao. Wanafikiria kuipata au kuitoa elimu bora kwa jamii.
Leo, naja na swali je, ni kweli kuwa Tanzania kuna elimu bora? Tangu taifa limeanza kuimba kutaka elimu inayotolewa nchini iwe na kiwango cha juu limefanikiwa? Je, wanaoimba wimbo huo wa elimu bora, serikali imeonyesha dhana ya kweli na utekelezaji katika kushughulikia masuala ya elimu kwa vitendo?
Je, wasomi wa Tanzania wamepata elimu bora inayostahili? Na kama wamepata inawasaidia kufikia malengo yao binafsi na taifa? Yote haya yanajibika endapo watu tutafikiri nini faida za elimu na mategemeo yetu katika matokeo ya sekta hii.
Tunaweza kuangalia elimu bora kama itamwezesha aliyesoma kuitumia katika jamii kwa manufaa yake binafsi na watu wanaomzunguka.
Ikimwezesha kufikiri kwa kina na kutatua matatizo yanayomzunguka kulingana na kiwango chake, ikiwemo kujiwezesha kimaisha kwa kuangalia njia mbadala ambazo zitamwezesha kupata kipato angalau kidogo kwa kutumia elimu aliyo nayo.
Sitaki kuamini kama serikali inaridhika na kiwango hicho, sitaki pia kuamini kuwa Watanzania wengine wanaridhika na kiwango cha wasomi Watanzania na mawazo yao. Ukitaka kujua kuwa hata kiwango cha leo kimeshuka, chukulia mfano wa msomi wetu wa chuo kikuu aliyehitimu mwaka huu na umfananishe na msomi wa miaka 20 ilitopita, wapo tofauti kifikra.
Msomi wa chuo kikuu leo hana habari kabisa na mambo yanayoendelea katika ulimwengu huu, hana mawasiliano ya nje ya vitabu na hii inachangia kukosa maarifa.
Inaeleweka wazi kuwa, uwezo wa kujenga hoja, kuzitetea na utendaji wa mtu katika hali ya kutatua matatizo, ndiyo unaotambulisha uelewa wa mtu siyo lugha wala kufaulu mitihani.
Sasa umefika wakati upimaji wa uwezo wa mwanafunzi kimasomo usitizamwe katika mitihani ya kuandika tu, kuna haja ya kuangalia ameelewa elimu ya vitendo? Anaweza kuitumia elimu aliyopipata kuisaida jamii inayomzunguka?
Utendaji na maarifa kwa wanafunzi viwe kipimo halisi badala ya mitihani ya kuandika. Tuchukue Mfano somo la historia, kwa shule za sekondari ambalo linahitaji kusoma kwa makini vitabu vingi ili kulielewa.
Siku hizi mwanafunzi akipata pesa ya kudurufu kitabu au kitini cha Nyambari Nyangwine, basi amefaulu mtihani, hata asipoingia darasani anaweza kufaulu na kupata alama ‘A’ waalimu na wanafunzi watakubaliana nami.
Kuna taarifa kuwa baadhi ya seminari kama St. James ya Kilema, Moshi, walimu wake wamewakataza wanafunzi kusoma baadhi ya vitini, hasa vinavyonakilika kwa urahisi wakati wa maandalizi ya mitihani. Hii nikuwawezesha wanafunzi kujijengea tabia ya kusoma kwa undani vitabu.
Hii ni kutokana na watu kuamini kuwa uwezo wao unapimwa kwa mitihani na hakuna njia nyingine isipokuwa kukariri tu na hili ni mpaka katikia vyuo vyetu vikuu. Hizi tunaweza kuziita changamoto zilizochangia kiwango cha elimu kushuka na dhana ya elimu bora kukwama na kupotea kabisa.
Ni changamoto kwa serikali ya sasa na mawaziri waliopo madarakani kuangalia udhaifu huu kwa kufanya utafiti na kushirikiana na wadau mabalimbali wa elimu ili kurudisha dhana ya elimu bora nchini.
Mpango Maalum wa Elimu ya Sekondari (MMES) na ule wa Elimu ya Msingi (MMEM), ulileta maendeleo mazuri lakini hayakulenga kwenye dhana ya elimu bora, ikakimbilia kwenye bora elimu, watoto wengi shuleni, vitabu, waalimu, madawati hakuna na vitendea kazi duni.
Wengi walisoma lakini kama hawakusoma, huko nyuma Mwalimu Nyerere alisema kuwa elimu bure, kila mtu akaenda shule, lakini tunakumbuka watu waliomaliza Darasa la Saba kati ya mwaka 1986 hadi 1995, baadhi hawajui hata kusoma. Inashangaza hawa walipitaje mitihani na walikuwa wanafundishwa je shuleni.
Tunakumbuka watu wangapi walisoma wakamaliza Kidato cha Nne, hawajui hata kusalimia au kujieleza kwa lugha ya Kiingereza, je hiyo ni elimu bora? Ni kiu ya kila mdau kujua hilo na kila Mtanzania anatamani kuona linafanyiwa kazi kwa makini na sekta zinazohusika ikiwepo serikali, waalimu, watunga mitaala, sera, mitihani na mabaraza ya wanafunzi, hawa ni wadau wa elimu ambao kwa pamoja wanapaswa kuelewa kile wanachokitafuta na wakifikie.
Ni ajabu kuwa kila taasisi au mdau niliyemtaja hapo juu anafanyakazi bila kumshirikisha mwenzake, hii ni hatari hatuwezi kupata elimu bora kwa namna hiyo.
Kinacholeta shida kwa Tanzania kwenye suala la elimu ni ushirikiano, shule binafsi zinaonekana za pembeni, shule za serikali ni mtoto wa nyumbani, Baraza la Mitihani (NECTA) ni hakimu hakuna mawasiliano na waalimu, wizara ni mwenye kuamua na kutoa amri kali huku mitaala ni watendaji ambao hawahitaji ushauri au mjadala.
Wakati taasisi ya mitaala inakimbizana kutengeneza mitaala mipya, walimu wanakimbizana kufundisha hawajaandaliwa kupokea mitaala mipya au kuingia kwenye mabadiliko kwa wakati.
Wakati huo huo Baraza la Mitihani linaandaa mitihani ambayo haiendani na mitaala mipya na wanafunzi wanakimbizana kusoma kile ambacho mwalimu ambaye hana mawasiliano au hajawahi kukaa pamoja na wadau wenzake anaitunga.
Kundi la wadau, lazima likae pamoja, vinginevyo elimu bora kwa Tanzania ni ndoto! Kwa muda mrefu sasa kila upande umekuwa ukirusha lawama kwa upande mwingine kuwa ndiyo chanzo cha kuharibika kwa kiwango cha elimu yetu.
Wakaguzi wa elimu kwa shule zetu nao ni kikwazo kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakionekana kama askari anayekuja kukamata watu mara wanapaoonekana katika mazingira ya shule, miundombinu mibovu yaani vijijini hawafiki.
Walimu hawana uhusiano mzuri na wakaguzi, hakuna muda wanaopewa kushauriana au kueleza matatizo yao, wanaishia kuandikiwa ripoti zinazowaumiza, hili linawafanya walimu waone taaluma hiyo sawa na adhabu kwao.
Serikali kupitia wizara inayoshughulikia elimu ilianza kuonekana kikwazo tangu serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani. Mwaka 1995, aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai, aliingia kwa namna yake na kuiingiza elimu katika siasa.
Kitendo cha Mungai kubadilisha mitaala ya shule za msingi na sekondari uliwakwaza walimu ambao hadi leo hawajasahahu.
Umefika wakati suala la elimu liachiwe wadau si wanasiasa ambao hukaa madarakani kwa muda wa miaka mitano na kubadilishwa elimu ni endelevu, inahitaji kubebwa pole pole ili ifike mahali elimu bora ipatikane Tanzania siyo bora elimu.
+255-784/715 – 686 575
Elimu ni kujifunza! Tunajifunza kwa kusoma! Karibu katika Blog hii ili tufundishane na kubadilishana Mawazo
Popular Posts
-
*alikubali kushindwa kwa siasa za Kijamaa *hakujilimbikizia mali Na Deogratius Temba WAKATI taifa linaadhimisha miaka 10 ya kifo cha mwasisi...
-
Na Deogratius Temba KWARESMA ni kipindi cha mfungo kwa waumini Wakatoliki. Mfungo huu ni wa siku hamsini. Kipindi hiki kinaanza na ibada ya ...
-
KAMPALA Uganda Dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ARVs, zikitumika sambasamba na dawa mseto aina ya (co-Trimoxazole), ...
-
Na Deogratius Temba. NI takribani miaka mitano tangu ililipo ibuika suala la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua sh. Bilioni ...
-
*Ilizamishwa ziwani na wakaoloni baadaye ikafufuka *Ina Umri wa miaka 98, mwaka 2013 itavunja rekodi ya dunia Na Deogratius Temba MV Liemba ...
-
Na Deogratius Temba SERIKALI imesema makazi ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Abdul Jumbe, yaliyoko Kigambo...
-
*Ni ajali iliyoweka historia kwa kuua *Bado usalama wa ziwani haujaimarika Na Deogratius Temba MEI 21, mwaka huu taifa limetimiza miaka 14 ...
-
, tutaendanayo mpaka uchaguzi Mkuu 2010 Na Deogratius Temba MWISHONI mwa wiki iliyopita Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha mapinduzi, (CCM), w...
-
TITLE OF THE PROJECT The effect of Water Conflict between Investor of VASSO Estate and Villagers in Kibosho Dakau, Moshi Kilimanjaro JOURNAL...
-
Taasisi ya mafunzo ya Jinsia (GTI) inayomilikiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) inaendelea na mafunzo ya kuwanoa wanaharakati kuanzia ...
No comments:
Post a Comment